Na. Catherine Mbena/Iringa
Bodi
ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA),tarehe 14
Septemba 2022 imefanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha
mkoani Iringa kujionea athari za uvamizi wa mifugo katika eneo la Bonde
la Ihefu . Katika ziara hiyo, Bodi ilishuhudia takribani mifugo zaidi ya
laki Mbili ikiwa ndani ya hifadhi.
Awali, akiwasilisha taarifa
ya Hifadhi kwa Bodi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Meing’ataki
alibainisha kwamba operesheni iliyofanyika kwa siku mbili ilifanikiwa
kukamata mifugo zaidi ya elfu moja na mia tisa katika eneo hilo la Ihefu
na itaendelea kwa siku 10 zaidi kuanzia tarehe 13 septemba 2022 hadi
tarehe 23 septemba 2022.
Akipokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya TANAPA,
Jenerali
(Mstaafu) George Waitara alisema “ leo tumejionea uvamizi mkubwa wa
mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha. Ikumbukwe hifadhi hizi ni mali
yetu sote watanzania na ni sehemu ya uchumi wa Tanzania, wakati mifugo
ni mali ya mtu mmoja mmoja. Hivyo ni jukumu letu kulinda hifadhi ambayo
ni ya Watanzania wote kwa faida ya sasa na ya baadaye”
Aidha,
Jenerali Waitara aliongeza kuwa mifugo itakuwa chanzo cha kufa kwa
hifadhi zetu, kwani inaua mifumo ya Ikolojia na kuhatarisha kutoweka kwa
wanyama na mimea. Hivyo ni muhimu hifadhi hizi zikalindwa kufa na
kupona.
Naye Prof. Wineaster Anderson ambae ni mmoja wa wajumbe
wa Bodi hiyo, alisema TANAPA ina wajibu mkubwa wa kulinda maliasili
zilizomo hifadhini kwa faida ya Watanzania wote.
“Tuna
wajibu mkubwa katika Taifa hili wa kulinda maliasili hizi pamoja na
miradi ya kimkakati kama Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere
ambalo linategemea maji kutoka vyanzo vilivyomo hifadhini Ruaha. Kiasi
kikubwa cha fedha kimekwishatumika kujenga bwawa hilo na wananchi wana
mategemeo makubwa ya kunufaika nalo.
Hivyo sisi tukishindwa
kulinda hivi vyanzo vya maji tutadaiwa na Watanzania sio tu leo, bali
hata baada ya maisha yetu hapa duniani” aliongeza Profesa Wineaster.
Kwa
upande wake Mjumbe mwingine wa Bodi, Kamishna wa Polisi Nsato Marijani,
alisisitiza kuongeza nguvu katika kufanya doria na kuendeleza
operesheni ya kuwaondoa wavamizi wote katika eneo la hifadhi hiyo.
Naye
Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema aliishukuru Bodi ya
Wadhamini kwa kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha kujionea changamoto
kubwa ya uvamizi wa mifugo ambayo ni tishio kwa uhifadhi nchini.
Alibainisha
kuwa endapo hapatakua na juhudi madhubuti na za dhati za kudhibiti
mifugo, itapelekea kufa kwa hifadhi zetu ambazo ni tunu kwa Taifa, na
zimekuwa zikituletea fedha, sifa na fahari ndani na nje ya nchi yetu.
Thursday, September 15, 2022

MIFUGO VAMIZI CHANGAMOTO YA UHIFADHI NCHINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment