HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 6, 2022

MAAFISA UGANI WAAGIZWA KUTEMBELEA WAKULIMA

 

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewaagiza maafisa Ugani wote kuhakikisha wanawatembelea wakulima mara kwa mara ili kutoa elimu itakayosaidia kulima kilimo chenye tija.

Kanali Thomas ametoa maagizo hayo wakati anazungumza na watumishi wa Idara ya Kilimo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo hivi karibuni.

Amesema serikali imetoa pikipiki kwa maafisa ugani wote lengo kuu ni kuwawezesha kuwafikia wakulima katika Kata na vijiji vyote ili wakulima waweze kulima kilimo cha kibiashara badala ya kilimo cha mazoea.

Akizungumzia migogoro baina ya wakulima na wafugaji,RC Thomas amesema serikali imetoa maelekezo ng’ombe wote wawekewe heleni sikioni ili kuwatambua na kudhibiti ng’ombe wanaongia kwenye mashamba ya wakulima Pamoja na kudhibiti wizi.

“Ng’ombe wote wanatakiwa kuwekewa heleni sikioni na kuingizwa kwenye mfumo,ng’ombe ambao hawatawekewa heleni hawataruhusiwa Kwenda popote,hivyo waambieni wafugaji watekeleze maagizo hayo kabla ya tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa zoezi hili la kitaifa’’,alisisitiza Kanali Thomas.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewaagiza maafisa mazingira kusimamia usafi wa mazingira ili maeneo yote yawe safi na kuepuka magonjwa ya kuambukiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningu ameahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa hasa zoezi la ng’ombe wote kuwekewa heleni ambalo linatekelezwa na Halmashauri katika vijiji vyote wilayani humo kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Wilaya ya Namtumbo ni miongoni mwa wilaya tano zinazounda Mkoa wa Ruvuma,robo tatu ya wilaya hiyo imezungukwa na maeneo ya hifadhi ikiwemo hifadhi ya Taifa ya Nyerere na ushoroba wa Selous-Niassa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad