HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 30, 2022

UZINGATIAJI WA SHERIA YA SERIKALI MTANDAO NI MSINGI WA MATUMIZI BORA YA TEHAMA SERIKALINI

 Afisa Habari eGA

UTEKELEZAJI wa Serikali Mtandao unategemea kuwepo kwa Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Mikakati Madhubuti ili kuongoza utekelezaji sahihi na kulinda maslahi ya utekelezaji na watumiaji wa huduma zitolewazo na Serikali kupitia TEHAMA.

Sheria ya Serikali Mtandao Na 10 ya mwaka 2019 inaelekeza Taasisi za Umma nchini kuzingatia matakwa ya Sheria na kuishirikisha Mamlaka ya Serikali Mtandao kabla ya kuanzisha au kujenga mifumo na miundombinu ya TEHAMA ili kuepuka urudufu wa jitihada za Serikali Mtandao.

Sheria nyingine zinazoratibu matumizi sahihi ya TEHAMA ni pamoja na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015 (Electronic Transactions Act, 2015) na Sheria ya Makosa ya Mitandao, 2015 (Cybercrimes Act, 2015). Sheria hizi zinalenga kuimarisha udhibiti na kuboresha utekelezaji wa masuala yanayohusu TEHAMA nchini.
Sheria ya Serikali Mtandao inazitaka Taasisi za Umma kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kabla ya kujenga au kuanzisha mradi wowote wa TEHAMA. Hii ina maana kwamba taasisi inawajibu wa kutoa taarifa ya kuanzishwa kwa mfumo wowote au miundombinu ya TEHAMA kwenye taasisi husika.

Kwa mujibu wa Sheria hii, mamlaka ina jukumu la kutoa ushauri wa kuendelea kwa mradi husika na kuitaka Taasisi hiyo kutoa taarifa ya utekelezaji mara kwa mara. Aidha, miradi yote inatakiwa kuripotiwa kupitia mfumo wa Government ICT Service Portal (GISP).

Pia Sheria inasisitiza kujenga na kusimamia mifumo kwa kutumia wataalamu wa ndani, haya yote yanafanyika ili kuwawezesha wananchi kupata huduma mahali popote bila kujali muda.

Aidha, ili kuhakikisha Utekelezaji wa Sheria ya Serikali Mtandao hasa katika ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA unafanyika katika viwango vinavyotakiwa, Serikali imetengeneza miongozo na viwango vya utekelezaji ili kuhakikisha kuwa Taasisi za Umma zinatekeleza jitihada hizo katika viwango na ubora unaotakiwa.

Miongozo hiyo hulenga kutoa maelekezo kwa watekelezaji kufuata utaratibu sahihi katika matumizi ya TEHAMA Serikalini. Miongozo hiyo inatoa pia maelekezo na ufafanuzi wa taratibu zinazotakiwa kufuatwa katika utekelezaji wa juhudi mbalimbali zinazohusu TEHAMA katika taasisi za umma.

Dhana ya Serikali Mtandao imejengwa katika nguzo kuu nne ambazo ni Sera, Sheria na Kanuni; Usimamizi naUtawala; Mifumo Tumizi na Miundombinu. Nguzo ya kwanza ya Usimamizi ndio nguzo inayosimamia uwepo wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Eng. Benedict Ndomba anasema ili Teknolojia ya Habari na Mawasiliano itumike Serikalini lazima kuwe na Usimamizi. Uwepo wa nguzo hii hutoa mwelekeo wa kuhakikisha teknolojia hii ya Habari inayotumika Serikalini inaratibiwa na kuainisha matumizi sahihi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma.

Vilevile Ndomba amesema kuwa, Taasisi zote za Umma nchini hazina budi kuzingatia kanuni, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika utendaji kazi wao ili kujenga mifumo yenye tija.

Aidha, Ndomba anabainisha kuwa, Sheria inazitaka na kuzielekeza taasisi za umma kuwasiliana na Mamlaka ili kuweza kushirikiana na kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanakuwa yenye tija kwa taasisi husika na serikali kwa jumla.

“Mamlaka ya Serikali Mtandao ipo kwa ajili ya kuhakikisha matumizi ya TEHAMA Serikalini yanakuwa yenye tija na faida kwa Serikali na Wananchi sio kwa ajili ya kuzibana taasisi za umma au kuzuia matumizi ya TEHAMA” Alisisitiza.

Naye, Meneja wa Huduma za Sheria Mamlaka ya Serikali Mtandao, ACP Raphael Rutaihwa anasema, uwepo wa sheria ya Serikali Mtandao na kanuni zake unasaidia kuwezesha matumizi sahihi ya TEHAMA katika taasisi za umma yanayopelekea kuboresha kwa utendaji kazi na kutoa huduma bora zinazopatikana kwa urahisi na haraka, na hivyo kuwa na Serikali ya Kidigitali iliyo imara na endelevu.
ACP Rutaihwa anasema sheria ya Serikali Mtandao inazitaka na kuelekeza kuwa taasisi za umma zinazohusika na ujenzi wa miundombinu ya Serikali kama vile barabara, reli na majengo kuhakikisha kuwa yanawekewa mazingira wezeshi kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya TEHAMA kuanzia wakati wa kuandaa michoro ya ujenzi wa miundombinu hiyo.

Pia, ameongeza kuwa, kulingana na Sheria ya Serikali Mtandao taasisi za umma zinatakiwa kuwasilisha mapendekezo na nyaraka zote zinazohusu miradi ya TEHAMA kabla ya kuanza utekelezaji kwa ajili ya kuhakikiwa na kupitishwa na Mamlaka na baadae kuwasilisha taarifa za maendeleo ya utekelezaji pamoja na taarifa ya mwisho baada ya kukamilika kwa mradi husika.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019. Mamlaka ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.

Kuanzishwa kwa Mamlaka hii mwaka 2019 kunaendeleza afua za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) iliyoundwa Aprili 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 Sura ya 245 ya mwaka 1997 na kuchukua sehemu ya mipango yake kwa sababu majukumu ya taasisi hizi yanafanana ingawa yanatofautiana katika mamlaka ya utendaji.

Sheria ya serikali mtandao inapatikana kupitia tovuti ya mamlaka ya serikali mtandao ambayo ni www.ega.go.tz , tovuti ya Bunge ambayo ni Bunge.go.tz na online Tv ya Mamlaka eGA online TV.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad