HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 29, 2022

Sensa imefikia asilimia 93.45 ya kaya zilizohesabiwa, watoa namba za simu kwa wasiohesabiwa

 *Asilimia iliyobaki ya ambao hawajahesabiwa wapewa utaratibu kufanikisha kuhesabiwa


Na Chalila Kibuda Michuzi TV
KAMISAA wa sensa ya watu na Makazi Spika Mstaafu Anne Semamba Makinda amesema zoezi la Sensa na Makazi na Makazi 2022 lililoanza usiku wa kuamkia Agosti 23, 2022 hadi kufikia Agosti 29, 2022 limefikia lina asilimia 93.45 kwa kaya zilizohesabiwa.

Sensa ya Watu na Makazi 2022 inakuwa na awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ni kwa ajili ya idadi na sensa ya pili kwa ajii ya makazi itayoanza kuanzia Septemba 1, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Makinda amesema kumekuwa mafanikio makubwa yaliyotokana na utayari wa wananchi kushiriki katika zoezi hilo kwa ajili ya maendeleo ya Nchi.

Amesema taarifa za watu waliohesabiwa zinaonyesha kuwa bado kuna asilimia 6.55 ya kaya hazijahesabiwa.

"Kuna uwezekano wa kutofikia kaya zote zilizobaki na lengo letu kila mtu anahesabiwa hivyo kutokana na hali hiyo wananchi wote ambao hawajahesabiwa wahakikishe wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa Sensa waliopo katika maeneo yao ili wahesabiwe." Amesema Makinda.

Amesema endapo itatokea kuna ambao hawajahesabiwa siku ya mwisho bado wanayo nafasi ya kuhesabiwa na kwamba wanashauriwa waende moja kwa moja kwenye Ofisi za Serikali za mitaa na kuonana na Mwenyekiti au Mtendaji wa Mtaa na kuwaachia namba ya mawasiliano ili kumrahisishia kazi karani amfuate alipo na kumuhesabu.

Makinda amesema kwa maeneo ya vijijini mwananchi ambaye hajahesabiwa aende kwenye ofisi ya mwenyekiti wa kitongoji anachoishi aache namba ya simu au kama hana atapewa utararibu wa wa karani kwenda kumhesabia hapo alipo.

Aidha amesesma Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeandaa namba maalumu ambao hawajahesabiwa kupiga simu moja kwa moja Makao Makuu Dodoma ili utaratibu wa kupeleka karani eneo husika ufanyike kwa wakati. Namba hizo ni:- 0753665491; 0764443873; 0626141515; 0784665404 pamoja na 0656279424

Amesema namba hizo zitaanza kutumika Agosti 30, 2022 hadi Septemba 5, 2022, ikiwa ni muda wa siku 7 wa ziada ili kumwezesha mwananchi kupata haki yake ya msingi ya kuhesabiwa. Namba hizo zitawekwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa anwani www.nbs.go.tz na zitasambazwa pia katika mitandao ya kijamii ili ziwafikie wananchi wengi iwezekanavyo.

Amewaomba wananchi kutanguliza busara katika matumizi ya namba hizo zitumike kwa lengo la Sensa na siyo vinginevyo na kuhimiza kamati za Sensa ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata, Kijiji na Mtaa kuhakikisha wanatoa namba za mawasiliano kwa ajili ya wananchi ambao watakuwa hawajahesabiwa ili waweze kupiga simu kueleza waliko ili utaratibu ufanyike wa kupeleka Karani wa Sensa awahesabu.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali ya imepanga pia kufanya Sensa ya Majengo mara tu baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu itakayojumuisha kukusanya taarifa za majengo yote ya makazi na yasiyo ya makazi nchi nzima kwa ajili ya kuboresha Sera na kupanga mipango ya kimkakati ya kuboresha sekta ya nyumba nchini.

"Wito wangu kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani waliowahesabu katika maeneo yenu kwa kutoa taarifa sahihi za majengo. Makarani waliofanya Sensa ya Watu na Makazi ndio hao hao watapita kwenye majengo yote yaliopo kwenye maeneo ya kuhesabia watu ili kukusanya taarifa za majengo."Amesema Makinda
Kamisaa wa Sensa Spika Mstaafu Anne Semamba Makinda (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la Sensa na Makazi 2022 linaloendelea nchini Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Masuala ya Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Emilian Karugendo akizungumza na waandishi habari kuhusiana na mwenendo wa ukusanyaji wa taarifa kwa makarani katika Sensa ya Watu na Makazi 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad