HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 20, 2022

WASTAAFU DODOMA WAGUSWA NA KASI YA WAZIRI NDALICHAKO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Joyce Ndalichako, akiwasikiliza baadhi ya wastaafu jijini Dodoma


Baadhi ya Watumishi wa NSSF na PSSSF wakiwa wanawasikiliza wastaafu wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Profesa Joyce Ndalichako alipokutana nao Dodoma.

*Wamshukuru kwa kusikiliza na kutatua kero zao
Na MWANDISHI WETU
Baadhi ya wastaafu wa NSSF na PSSSF wamemshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako kwa kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wastaafu nchini.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa mkutano ulioitishwa na Waziri Profesa Ndalichako jijini Dodoma, wastaafu hao walipongeza juhudi zinazochukuliwa na Profesa Ndalichako za kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wastaafu hatua ambayo itapunguza changamoto za wastaafu.

Mzee Ramadhani Abdallah ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, alisema mkutano huo wa Waziri Ndalichako umedhihirisha kuwa kero na changamoto za wastaafu sasa zinaenda kupungua kutokana na namna wanavyosikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.

“Namshukuru Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumchagua Waziri Ndalichako ambaye ni msikivu, anayejali wazee, anayejali watumishi waliotumikia nchi hii kwa muda mrefu, hili alilolifanya leo ni jambo kubwa na zuri,” alisema.

Naye, Mstaafu Maria Kapande alimshukuru Waziri Ndalichako kwa kukutana na wastaafu na kusikiliza changamoto zao ili ziweze kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Akizungumza na baadhi ya wastaafu wa Mifuko ya PSSSF na NSSF ambao walijitokeza kusikilizwa kero zao, Waziri Profesa Ndalichako alisema lengo la mkutano huo ni kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wastaafu.

“Nimeona nitenge muda kusikiliza changamoto walizonazo wastaafu wa NSSF na PSSSF hivyo zile changamoto ambazo tunaweza kuzitatua papo kwa papo tunafanya hivyo na zile ambazo zinahitaji muda tunachukua vielelezo na kuzifanyi kazi,” alisema Profesa Ndalichako.

Waziri Profesa Ndalichako alisema kupitia mkutano huo wataendelea kujifunza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wastaafu hivyo aliwaomba watendaji wa mifuko hiyo kuweka utaratibu wakusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

“Ni jukumu na ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za wananchi wakiwemo wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii,” alisema.

Waziri Profesa Ndalichako alisema lengo la Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa wastaafu bila usumbufu wowote na kuwahudumia kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad