HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 12, 2022

WAELIMISHENI WATUMISHI NA WAAJIRI KUFAHAMU HAKI NA STAHILI ZAO- JAJI KIONGOZI

 Na Mary Gwera, Mahakama


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa Wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi na Wawakilishi wa Waajiri nchini kuendelea kuwaelimisha watumishi na waajiri kuhusu haki na stahili za watumishi ili kupata ufahamu na hatimaye kuepuka migogoro ya kazi.

Akizungumza wakati akifungua rasmi Mkutano wa siku mbili wa Kamati ya Utatu leo tarehe 11 Julai, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amesema kuwa ni wajibu wa kila upande kuhakikisha kuwa unatimiza wajibu wake kwa mujibu wa matakwa ya kisheria huku wakizingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa kuna amani na utulivu katika maeneo ya kazi.

“Hakikisheni waajiriwa wanapewa mikataba ya kazi na kuongeza tija na uzalishaji utakaowezesha ukuaji wa uchumi, na vilevile mhakikishe mnatatua migogoro na madai yanayohusu stahili au haki za msingi za wafanyakazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa,” amesema Jaji Kiongozi.

Mhe. Siyani amewasisitiza pia wadau hao wa Kazi kutosahau kuheshimu sheria kwa kufanya kazi kwa umakini na uadilifu na kutokuwa sehemu ya dhuluma ama usumbufu kwa wale wanaowawakilisha.

Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amewakumbusha Wadau wa Mahakama kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania ili kutekeleza ipasavyo Dira ya Mahakama ya Tanzania ya ‘Utoaji Haki sawa kwa wote na kwa wakati’.

Mhe. Siyani ameongeza kuwa ili kufikia dira hiyo, Mahakama inategemea ushiriki wa wadau wote na vilevile nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2022-2024/2025) unasema: Upatikanaji wa haki sawa kwa wote na kwa wakati na kujenga Imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau. Hivyo ni muhimu kuzingatia ili azma ya Mahakama ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati iweze kufikika.

“Naomba niendelee kuwakumbusha wadau wote kuendelea kushirikiana na Mahakama kwa kuhudhuria mahakamani kwa tarehe zilizopangwa na kutokuwa na kikwazo cha uondoshaji wa mashauri mahakamani kwa wakati.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi amesema kuwa, katika Divisheni hiyo mashauri yaliyobaki hadi kufikia Desemba 2021 yalikuwa 1,526, huku mashauri yaliyosajiliwa toka Januari, 2022 hadi Juni mwaka huu ni 726, mashauri yaliyoamriwa kuanzia Januari mpaka Juni mwaka huu yalikuwa 1,391 sawa na asilimia 195 ya mashauri yaliyofunguliwa.

“Mhe. Jaji Kiongozi, kumekuwa na kasi kubwa ya uondoshaji wa mashauri katika Divisheni yetu, na hii ni kutokana na jitihada si tu za Maafisa na Watumishi wa Mahakama bali wadau wote waliopo hapa kwani wametoa ushirikiano na kila mmoja kwa nafasi yake amehakikisha mashauri ya kazi yanamalizika kwa kasi kupisha shughuli za kiuchumi kuendelea, kama ilivyokuwa lengo la uanzishwaji wa Mahakama hii ya kazi pamoja na Taasisi zingine za kazi,” alieleza Mhe. Salma.

Naye, Bw. Maridadi Fanuel, Mratibu Taifa Sheria za Kazi na Viwango vya Kazi vya Kimataifa kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO)-Tanzania ameipongeza Divisheni ya kazi kwa kasi nzuri ya uondoshaji wa mashauri na kusema kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Divisheni hiyo kwa kuiwezesha katika maeneo mbalimbali ikiwemo kutoa Mafunzo kwa watumishi wake.

“Takwimu zinaonyesha kuwa utendaji wa Mahakama ya Kazi ni mzuri sana hali hii inatupa moyo sisi ILO wa kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Mahakama ya Kazi maana tunaona ufanisi wa kazi unatekelezeka kiuhalisia,” amesema Bw. Fanuel.

Mkutano huu wa watumiaji wa Kamati ya Utatu hufanyika kila mwaka na unajumuisha sio tu uwakilishi wa utatu yaani ‘TUCTA’, ‘ATE’ na Serikali kupitia Wizara ya Kazi pamoja na Kamishna wa Kazi, Majaji pamoja na wadau wengine wakiwemo ‘CMA’ Mwanasheria Mkuu na Wakili Mkuu wa Serikali, Mawakili wa kujitegemea, wawakilishi binafsi na kadhalika unalenga kujadili mafanikio pamoja na changamoto mbalimbali ili kupata maoni ya pamoja ili kuboresha huduma hususani utatuzi wa migogoro ya kazi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua Mkutano wa sita wa Kamati ya Utatu leo tarehe 11 Julai, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Majaji Wafawidhi kutoka Kanda mbalimbali pamoja na wadau wengine wa Mahakama ya Kazi wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo katika picha) alipokuwa akifungua Mkutano wa sita wa Kamati ya Utatu katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama na wadau wengine wa Mahakama wakiwa katifuatilia hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa sita wa utatu kutoka kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi akizungumza katika Mkutano huo.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Elizabeth Nyembele akizungumza wakati wa Mkutano wa sita wa Utatu unaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam (JNICC).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi (waliosimama), wa kwanza kulia ni Mhe. Amir Mruma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wa pili kushoto ni Mhe. Salma Maghimbi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, wa kwanza kushoto ni Bw. Maridadi Fanuel, Mratibu Taifa Sheria za Kazi na Viwango vya Kazi vya Kimataifa kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO)-Tanzania na wa pili kulia ni Bi. Lilian Dennis, Kamishna wa Kazi kutoka Wizara ya Kazi na Ajira.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wadau walioshiriki katika Mkutano wa Kamati ya Utatu.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wastaafu (waliosimama) waliohudhuria katika Mkutano huo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Wasajili walioshiriki katika Mkutano wa kamati ya utatu.
Picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi walioshiriki katika Mkutano wa Kamati ya Utatu. (Picha na Mary Gwera, Mahakama)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad