HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 21, 2022

PROF. MBARAWA AZINDUA BODI YA TBA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Dk. Ombeni Swai (kushoto), na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro (katikati), wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo. 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Dk. Ombeni Swai mara baada ya kuizindua Bodi hiyo, katikati ni Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro akishuhudia.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati akizindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Dar es Salaam leo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi Mpya ya Ushauri na Menejimenti ya TBA jijini Dar es Salaam leo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakala huo jijini Dar es Salaam leo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akimkabidhi vitendea kazi Mjumbe wa Bodi mpya ya Ushauri ya TBA, Bi. Vicky Jengo mara baada ya kuizindua Bodi hiyo.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati akizindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Dar es Salaam leo, Wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu (Sekta ya Ujenzi), Bw. Rafael Nombo na Kaimu Mkurugenzi Huduma
 za Ufundi Qs. Optatus Kanyesi wakifuatilia.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuuwezesha Wakala huo kuwekeza kikamilifu katika viwanja vyake vilivyopo katika maeneo ya kimkakati ili kumaliza tatizo la upungufu wa nyumba za viongozi na watumishi wa umma lililopo nchini.

Akizungumza mara baada ya kuzindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema huu ndio wakati wa TBA kujiimarisha kimiundombinu na kiuchumi kwa kutumia fursa ya mahitaji ya nyumba kwa ajili ya watumishi wa umma na majengo ya kibiashara katika miji mikuu.

"..Hakikisheni mnakuja na mipango ya kutumia rasilimali ya viwanja na majengo mlio nayo kupata faida kwa kujenga majengo mazuri katika maeneo ya miji na kuhakikisha nyumba zenu zaidi ya elfu sita zilizopo zinakuwa katika viwango bora wakati wote na kuvutia wapangaji," amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa ameipongeza TBA, kwa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi 3,500 Nzuguni Jijini Dodoma na kuongeza kuwa mradi huo ukikamilika kwa wakati utawaongezea mapato kwa kuwa bado mahitaji ya nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo ya mijini ni makubwa.

"...Tengenezeni mikakati ya ubunifu itakayo wawezesha kushirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha sekta ya majenzi na makazi ya viongozi na watumishi wa umma inaimarika," amesisitiza Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Arch. Dk. Ombeni Swai amesema Bodi yake itafanya kazi kwa uadilifu na ubunifu ili kuiwezesha TBA kupata faida na kutoa huduma ya kuaminika kwa Watanzania.

Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa miongozo anayoitoa na kusisitiza kuwa TBA itaendelea kusimamia mifumo, nidhamu, udhibiti na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya nyumba na majengo ya Serikali nchini kote kwa kuzingatia mahitaji na faida ili kukuza mtaji ikiwemo ujenzi wa nyumba 3,500 jijini Dodoma.

Wajumbe wapya wa Bodi ya Ushauri ya TBA itakayohudumu kwa miaka mitatu ni pamoja na Arch. Dk. Ombeni Swai (Mwenyekiti), Qs. Optatus Kanyesi (Mjumbe), Bw. Shaban Kabunga (Mjumbe), Qs. Joseph Mkali (Mjumbe), na Bi. Vicky Jengo (Mjumbe). IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad