HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 3, 2022

KATIBU MKUU UJENZI AAGIZA TBA KUWEKA MUONGOZO MKATABA WA UJENZI

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayesimamia Sekta ya Ujenzi Balozi Aisha Amour amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha mikataba inayotolewa kwa wapangaji ina ainisha masuala muhimu mbalimbali ikiwemo utunzaji wa nyumba na mazingira.

Hayo ameyasema Katibu Mkuu huyo wakati akikakagua miradi ya ujenzi wa nyumba na majengo ya Serikali jijini Dodoma inayotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania pamoja na vikosi vya ujenzi.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa mkataba unapaswa uelezee jinsi ya kutunza nyumba endapo mpangaji anataka kufanya mabadiliko yoyote aandike barua inayoelezea maeneo ambayo atafanya ukarabati huo.

"Ni vema mkataba mnaompatia mpangaji ueleze kwa kina namna ya utunzaji nyumba, ikiwemo aina ya miti inayoruhusiwa kupandwa katika eneo husika ili kulinda nyumba hizo" amesema Balozi Aisha.

Ameongeza kuwa kuruhusu kila mpangaji apande miti anayoijua inaweza kusababisha upandwaji wa miti inayoweza kuharibu kuta za nyumba kutokana na mizizi ya miti hiyo, hivyo ni vema watoe muongozo kwenye mkataba wa upangishaji.

Katika ziara hiyo Balozi Aisha amekagua nyumba 20 za viongozi eneo la Kisasa, nyumba 150 za watumishi eneo la Nzuguni ambazo zipo katika hatua ya mwisho ya kukamilika kwake pamoja na ofisi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliyopo mji wa Serikali Mtumba ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 33.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad