HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 3, 2022

Jengo jipya la Mama na Mtoto kumpeleka Rais Samia Hospitali ya CCBRT jumanne

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua jingo jipya la Mama na Mtoto ambalo ni maalumu kwaajili ya kuboresha mfumo wa huduma ya afya ya mama na mtoto kwenye Hospitali ya CCBRT Msasani Jijini Dar es Salaam Jumanne.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyomnukuu Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Bi Brenda Msangi Jijini Dar es Salaam jana, Jengo hilo jipya linajumuisha maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje, vyumba vya dharura, vyumba nane vya kujifungulia, vyenye bafu na vyoo kwa ajili ya watu wenye ulemavu, vyumba sita vya upasuaji vya kisasa vilivyojengwa kwa teknolojia mpya na viwango vya kimataifa, sambamba na wodi ya wazazi.

“CCBRT inaunga kwa vitendo juhudi na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta afya kwa ujumla wake ikiwemo afya ya mama na mtoto,” alisema Bi Msangi.

Jengo hili jipya linalenga kukabiliana na tatizo la msongamano katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam, hali ambayo husababisha madhara kwa idadi kubwa ya akina mama wajawazito katika kundi maalumu kama vile wenye ulemavu na wengineo ambao huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbana na unyanyapaa, kutelekezwa na mwisho wa siku wao au vichanga vyao kupata madhara.

Alisema Jengo hili la kipekee limejengwa kwa nguzo kuu inayoungansisha majengo sita. vyumba vyote vya kutolea matibabu katika kila jengo (block) vimeunganisha ili kuweza kufikika kwa urahisi.

“Huu ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi unaofanya kazi kwa manufaa ya Watanzania kama sehemu ya ahadi yetu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu namba 3 (SDG 3) juu ya afya bora na ustawi,” alisema Bi. Msangi.

Bi Msangi alisema CCBRT itaendelea na mpango wake wa kuleta mapinduzi na kuboresha ubora wa huduma kwa watu wanaoongezeka katika Jiji la Dar es Salaam kupitia usanifu wa miundombinu yake.

Hospitali ya CCBRT kwa kushirikiana na wadau imezindua rasmi awamu ya pili ya mpango mkakati utakaohakikisha kunakuwepo na utekelezaji madhubuti wa mpango wa miaka 12 unaolenga kuboresha mfumo wa huduma ya afya ya mama na mtoto Mkoani Dar es Salaam.

“Jengo la kuvutia litakalozinduliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kesho ni zao la ushirikiano wa kipekee kati ya CCBRT, Wadau wa Maendeleo na Serikali ya Tanzania,” alisema Bi Msangi na kuongeza kuwa malengo CCBRT ya kuwahudumia watu wenye ulemavu yatazingatia kauli mbiu ya malengo ya maendeleo endelevu ya kutomwacha mtu nyuma.

Hospitali ya CCBRT imejumuisha programu maalumu kwa wanawake wajawazito wenye ulemavu, mabinti wanaopata ujauzito katika umri mdogo na wanawake Wajawazito wenye historia ya kuugua fistula.

Licha ya wanawake wengi Mkoani Dar es salaam kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, utafiti wa idadi ya watu wa mwaka 2015–2016 ulibaini kuwa maeneo ya mijini yana viashiria vibaya vya afya kuliko vijijini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad