WANANCHI TABORA WATAKIWA KUJITOKEZA KUSAJILI NA KUPATA VYETI VYA KUZALIWA BILA MALIPO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 4, 2022

WANANCHI TABORA WATAKIWA KUJITOKEZA KUSAJILI NA KUPATA VYETI VYA KUZALIWA BILA MALIPO


Kabidhi Wasii Mkuu Bi. Angela Anatory akitoa maelezo kuhusu Mpango wa Usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano ambao umezinduliwa Juni 03, 2022 mkoani Tabora.


Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Canada Bi. Helen Fytche akitoa ufafanuzi jinsi Serikali yake kupitia shirika hilo linavyoendelea kuisaidia Tanzania katika uboreshaji wa huduma za kijamii.WANANCHI wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwasajili watoto wao ili wapate vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo kupitia Mpango wa Usajili na Kuwapatia Vyeti vya Kuzaliwa hivyo kupata haki yao ya msingi ya kutambuliwa.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo katika uzinduzi wa Mpango wa Usajili na Kuwapatia Vyeti vya Kuzaliwa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoani Tabora.

Amesema kwamba ni vyema viongozi katika ngazi zote wakafatilia kwa karibu utekelezaji wa Mpango huu ili kuhakikisha watoto wanaosajiliwa ni wale walioa na sifa stahiki na wazazi wanatambuliwa ipasavyo.

“Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa Mikoa iliyo na muingiliano mkubwa na raia wa nchi jirani hivyo ni vyema wazazi watambuliwe ipasavyo kwa hivyo kama Serikali tunaagiza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka nyingine za utambuzi zishirikishwe kikamilifu katika zoezi hili Vitambulisho vya Taifa vitumike katika utambuzi’’ alisema Bi. Makondo.

Ameongeza kuwa tangu kuzinduliwa mpango huu hapa nchini mwezi Juni, 2015 idadi ya Usajili wa Watoto wenye Umri wa Chini ya Miaka 5 imepanda kutoka 13% kwa takwimu za sensa ya mwaka 2012 hadi kufikia 65% kwa takwimu za mwaka 2021 hivyo ameipongeza RITA na wadau wote waliowezesha kupatikana kwa mafanikio hayo. Mpaka sasa Mpango huu unatekelezwa katika Mikoa 22 ya Tanzania Bara na zaidi ya watoto 7,549,878 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bila.

‘’Serikali inatambua mchango mkubwa wa Wadau wa maendeleo katika utekelezaji wa mpango huu. Nichue fursa hii kuwashukuru kwa dhati Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto - UNICEF, Serikali ya Canada na Kampuni ya Mawasiliano ya TIGO pamoja na wadau wengine kwa kuendelea kuwa sehemu ya utekelezaji wa mpango huu muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu’’. amesema Bi. Makondo

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt Batilda Buriani aliyewakilishwa na Katibu tawala wa Mkoa, Bw. Msalika Makungu amesema kuwa Mkoa wa Tabora una wilaya 7 na halmashauri 8 ambazo zitatekeleza Mpango huo kwa kutumia vituo vya Tiba na Ofisi za Watendaji Kata ambavyo jumla yake ni 542 na kutarajia kusajili watoto zaidi ya 549,167 walio na umri chini ya miaka mitano.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2011 ni asilimia 9 tu ya watoto katika Mkoa wa Tabora wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa hivyo idadi hiyo kuonesha wazi kuwa watoto wengi hawajasajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa na hivyo kushindwa kupata takwimu ili kuweza kupanga mipango sahihi ya huduma za afya na elimu.

‘’ Maandalizi yote ya Msingi yamekamilika na naamini vituo vyote tayari vimeanza kutoa huduma. Kama sehemu ya maandalizi, tulifanya semina ya viongozi wote kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya na halmashauri ambapo RITA walitupa elimu ya kina kuhusu mpango huu. Kwa ujumla tumeuelewa, tumeupokea na tutausimamia kikamilifu na nakuhakikishia kwamba malengo yalitowekwa yatafikiwa ambapo tulikubaliana ni watoto wote walio na sifa za kusajiliwa wapate huduma hiyo’’ Aliongeza Dkt Batilda Buriani.

Naye Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Angela Anatory alisema Mpango huo umesogeza huduma za usajili karibu na maeneo ya makazi ya wananchi na huduma kupatikana bure katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya Mama na Mtoto na kwenye ofisi za Watendaji Kata.

Bi. Anatory ameongeza kuwa Mpango huu umeweza kuimarisha mfumo wa kusajili, kutuma na kuhifadhi taarifa za waliosajiliwa kwa kutumia simu ya kiganjani (simu janja) iliyowekwa programu maalum ambapo taarifa hizo hutumwa moja kwa moja hadi kwenye kanzidata ya RITA Makao Makuu tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo nyaraka za taarifa za waliosajiliwa kusafirishwa kwa gari hadi Jijini Dar es salaam kutoka kila Wilaya kote Tanzania Bara .

‘’Kila kituo cha tiba kinachotoa huduma ya mama na mtoto na ofisi za watendaji wa kata wamekabidhiwa simu na vitendea kazi mbalimbali hivyo naamini kuanzia sasa taarifa za watoto wanaosajiliwa tutaziona moja kwa moja kupitia mtandao na tutaona nani anasajili na nani hafanyi kazi hiyo’’ alisema Bi. Anatory.


Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEEF,) Bi. Shalin Bahuguna akieleza ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania katika kuboresha kwa kuwezesha kusogeza huduma karibu na wananchi na hiyo ni pamoja na mpango wa usajili wa kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria akiongoza meza kuu kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mpango wa Usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto walio chini ya miaka mitano.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad