HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 23, 2022

Wakulima wanufaika na Vifaa 11, 000 vya kuhifadhia mazao ya Viungo na Mbogamboga

 


Na Gaspary Charles - TAMWA ZNZ

JUMLA ya vifaa 11, 000 vya kuhifadhia mazao ya Viungo na Mbogamboga vimetolewa kwa wakulima 666 wanufaika wa Mradi wa Viungo, Mboga na Matunda kisiwani Pemba unaotekelezwa kwa mashirikiano ya taasisi za People’s Development Forums (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya chini ya mpango wa AGRI-CONNECT Tanzania.

Utolewaji wa vifaa hivyo ambao ni sehemu ya utekelezaji mradi huo katika kufungua mnyororo wa thamani kwa wakulima wa mazao hayo Zanzibar unalenga kuwawezesha wakulima kukabiliana na tatizo la upotevu na uharibifu wa mazao ya chakula unaosababishwa na wakulima kukosa mbinu na zana bora za kuhifadhia mazao wakati na baada ya mavuno.

Miongoni mwa vifaa vilivyogaiwa kwa wakulima ni pamoja na chupa maalum za kuhifadhi na kusarifu mazao ya mboga 9,600, mifuko midogo ya kuhifadhi mboga 500 pamoja na viroba 300 kwaajili ya kutunzia mazao ya Viungo baada ya kuvuna.

Akizundua zoezi hilo, mkuu wa mkoa wa Kaskazini Pemba, Mhe. Salama Mbarouk Khatib, alipongeza juhudi za mradi wa VIUNGO kwa kusaidia kuinua shughuli za kilimo Zanzibar na kuagiza wakulima kutumia fursa za mradi kujikwamua kiuchumi kutokana na uwezeshaji unaotolewa kwenye mradi huo.

“Niwapongeze sana watekelezaji wa mradi huu, PDF, CFP na TAMWA ZNZ, kwa kuja na mbinu hii muhimu ya kuwapatia elimu wakulima kuhusu uhifadhi wa mazao kwasababu haya yote yanasaidia wananchi kuondokana na umasikini katika familia zao,” alieleza mkuu wa Mkoa huyo.

Aidha Salama aliagiza watekelezaji wa mradi kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima ya namna bora ya kusarifu mazao yao kwa kuzigatia vigezo sitahiki vya ubora wa chakula.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa alitoa wito kwa mradi kuongeza nguvu kuhamasisha wakulima kuzalisha mazao bora kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kuondokana na suala la uagizaji wa mazao ya vyakula kutoka nje ya kisiwa cha Pemba.

Alisema, “agizo langu kwa mradi, ni lazima tufike pahali wakulima tuzalishe mazao ambayo tunakidhi soko la ndani. Tunao uwezo wa kulima Vitunguu, Mbatata, Karoti na mazao mengine ambayo tunayaagiza nje ya kisiwa. Hiyo ndiyo kiu yangu kuona kwamba soko la ndani linadhibitiwa na wakulima wetu na uwezo huo tunao.”

Mapema mkurugenzi wa taasisi ya CFP, Mbarouk Mussa Omar alieleza kuwa zoezi hilo ni awamu ya kwanza ya ugawaji wa vifaa hivyo kwa wakulima, ambapo unatarajia kuwanufaisha wakulima 1,332 kwa Unguja na Pemba katika zoezi hilo.

Nae Afisa Lishe wa mradi huo Mkombozi Nzoya alisema, utoaji wa vifaa hivyo imekuja kufuatia mradi kubaini kuwepo kwa upotevu wa mazao ya chakula hasa wakati wa mavuno jambo ambalo hupelekea hasara kwa wakulima wengi kutokana na kukosa zana bora za kudhibiti mazao yao.

Alieleza, “katika utekelezaji wa mradi huu, tumebaini kumekuwa na upotevu mkubwa wa mazao ya chakula hasa katika kipindi cha mavuno na uchakataji, hivyo mradi ukaona uje na vifungashio hivi ambavyo ni rafiki kwa wakulima na mazingira ili viwasaidie kuondoa tatizo hili ambalo linawarejesha nyuma kwa kuwasababishia hasara.”

Kwa upande wake Lalo Kayanda ambaye ni afisa uwezeshaji kiuchumi, alisema mradi umegawa visanduku 130 kwenye vikundi vya hisa ili kuwezesha wajasiriamali kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi kupitia vikundi vya hisa wakati wakiendelea na shughuli zao za kilimo.

“katika awamu hii ya mwanzo jumla ya visanduku 130 kwaajili ya vikundi vya hisa vimetolewa kwa wanavikundi 3,900 kwa lengo la kuviwezesha vikundi hivyo kuongeza uwezo wa kujiimarisha kiuchumi kupitia vikundi vya kuweka na kukopa,” alifahamisha Lalo.

Hivi karibuni mradi ulifanikisha zoezi la ugawaji wa miche 25,000 kwa wakulima na mbegu kilo 1,707 sawa na tani 1.5 kwa wakulima 2,500 wa kanda za Unguja na Pemba kutoka shehia ambapo mradi unatekelezwa kwaajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao kwa wingi.

Mradi wa Viungo, Mboga na Matunda ni mradi ambao unalenga kufungua fursa katika myororo wa thamani kwenye mazao hayo Zanzibar kwa kuwawezesha wakulima kuongeza wingi na uzalishaji wa mazao bora yenye kuzingatia kilimo himilivu ambao unatekelezwa kwa mashirikiano ya taasisi za People’s Development Forums (PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya chini ya Mpango wa AGRI-CONNECT Tanzania.
Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba, Mhe. Salama Mbarouk Khatib akimkabidhi kisanduku cha hisa mmoja wa wanavikundi vya hisa wakati wa wagawaji wa vifaa kwa wanufaika wa mradi wa VIUNGO kisiwani Pemba unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya. (Picha na TAMWA ZNZ)
Lalo Kayanda ambaye ni afisa uwezeshaji kiuchumi akielezea namna mfumo wa kuweka na kukopa kwenye vikundi vya ujasiriamali utakavo fanya kazi kwa wanavikundi.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad