HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 13, 2022

Wadau wa kilimo waeleza mafanikio yao kwa Wafadhili wa SAGCOT

 

Na Mwandishi Wetu Iringa
WADAU wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi katika kongani ya Ihemi inayoshughulikia mikoa ya Iringa na Njombe wameeleza mafanikio waliyopata kwa Wafadhili wa Kituo cha kuendeleza kilimo nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) mara walipotembelea katika kongani hiyo kujionea shughuli zinazofanyika katika kukuza na kuendeleza kilimo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kutembelewa na wafadhili hao ambao ni Serikali ya Tanzania, ofisi ya Ubalozi wa Ufalme wa Norway, USDA/USAID, FCDO (zamani UK AID), Wanufaika kutoka Kiwanda cha kuzalisha maziwa cha Asas Dairies ltd, GBRI Business Solutions (T) Ltd, na Tamu Tamu Tanzania wameeleza namna SAGCOT ilivyoweza kushirikiana nao katika kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo kwenye ukanda huo na kuleta mchango chanya katika pato la Taifa.

Afisa ugani wa Kampuni ya Tamu Tamu Tanzania, Bw. Gibson Kalyetekela alisema toka waanze kufanya kazi na SAGCOT mwaka 2019 kama wabia wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwafikia wakulima zaidi ya elfu kumi ambao wamenunua miche ya tufaa inayozalishwa na kampuni hiyo sambamba na kuwapa na kutoa elimu kwa wakulima juu ya kilimo cha zao.

“Kupitia Sagcot tumeweza kuwafikia wakulima 10,000 ambapo tumekuwa tukiwapa elimu juu ya usimamizi wa kilimo cha zao hilo, sambamba na kuwaelimisha juu ya kupima afya ya udongo ili kubaini mapungufu yaliyopo kwenye udongo ili kuurutubisha na kutoa mavuno mazuri,” alisema Bw.Kalyetekela

Aliwaeleza wageni hao kuwa kampuni yao imejipanga kuwafikia wakulima 30,000 kwa mwaka huu kwa kuwapa elimu juu ya maandalizi ya ardhi kwa kilimo, umuhimu wa kupima afya ya udongo na matumzi sahihi ya chokaa mazao na kuwapatia miche bora ya tufaa ili waweze kupata mavuno mazuri na kupiga hatua kiuchumi na maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS, Bw. Fuad Abri alisema Kituo cha Sagcot kimekuwa ni kiunganishi kati ya wakulima, wafugaji na masoko pamoja na watoa huduma za ugani kama pembejeo, mbegu na zana za kilimo jambo lilopelekea mafanikio makubwa kwa wakulima na wafugaji katika ukanda huu.

“SAGCOT imetuwezesha kuwafikia wafugaji wengi katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya jambo lililowezesha kiwanda kupata maziwa mengi kwa ajili ya kusindika na kuwapa uhakika wa soko la maziwa ya wafugaji katika kongani ya Ihemi,” alisema Bw.Abri

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya GBRI Business Solutions ltd, Bi.Hadija Jabir anayejihusisha na kilimo cha mboga na matunda mkoani Iringa alishukuru kutembelewa na wabia hao na kusema Sagcot ni nguzo muhimu katika mafanikio ya kampuni yake kwa kuiwezesha kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi.

‘’Kupitia SAGCOT mpaka sasa nimeweza kufanya kazi na wakulima zaidi ya Elfu tano wamboga na matunda na wauzaji kwenye magenge 840 katika mikoa ya Iringa na Dar es salaam, jambo ambalo limeweza wakulima wengi kupiga hatua kimaendeleo kupitia biashara hii,” alisema Bi.Jabir

Bi. Jabir alisema SAGCOT imeweza kuwakutanisha na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na wadau wa maendeleo, mabenki pamoja na kuwajengea uwezo kwenye upande wa biashara kwa kuwaunganisha na wadau ambao wameshafanikiwa kwenye biashara.

Taasisi ya SAGCOT inafadhiliwa na Serikali ya Tanzania, Mashirika ya Misaada ya kimataifa hususani Ubalozi wa Ufalme wa Norway, USDA/USAID na FCDO (zamani UK Aid), Pia wamekuwa wakishirikiana na wadau wengine wa maendeleo ya kilimo AGRA na kuunda ubia namashirika ya WWF na IUCN.
Daktari wa Mifugo,Sikili wa ASAS DAIRIES FARM LTD (kushoto) akiwawaelezea Wafadhili wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) namna ufugaji unavyofanywa kwenye shamba lilopo Nyang'olo Wilayani Iringa waliokuwa kwenye ziara ya siku tatu kujionea maendeleo kwenye Kongani ya Ihemi mwishoni mwa wiki (katikati) ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi SAGCOT, Bw. Ally Laay, kushoto kwake ni Mkuu wa Kongani na Maendeleo ya Ubia, Bi. Maria Ijumba wapili kulia ni Mkurugenzi wa Fedha Bi. Anna Mtaita.
Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS, Bw. Fuad Abri katikati akizungumza na wabia, Menejimenti ya SAGCOT mara baada kutembelea Shamba linalomilikiwa na kampuni hiyo lililopo kitongoji cha igingilagwa mwishoni mwa wiiki Mkoani Iringa Ikiwa ni ziara ya siku tatu ya Wafadhili wa Kituo cha kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), wa kwanza kushoto ni Meneja Kongani ya Ihemi Bw. Hkalid Mgalamo , Wapili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Bw. Geoffrey Kirenga na watatu kulia ni Mkurugenzi wa Fedha Bi. Anna Mtaita.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad