HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 29, 2022

RITA YAPIGA KAMBI VIWANJA VYA SABASABA, YAJIPANGA KUSAJILI NA KUTOA VYETI VYA KUZALIWAMsajili msaidizi mwandamizi Rehema Ludovick (Kulia,) akitoa huduma kwa mmoja wa wateja waliotembelea banda RITA katika maonesho ya Sabasaba yanayoendelea, Bi. Rehema  amesema katika maonesho hayo watasajili na kutoa vyeti kwa wahitaji ambao hawajawahi kupata vyeti hivyo pamoja na kutoa elimu kwa Umma
Afisa Mawasiliano kutoka RITA Jafari Malema (Kulia,) akikagua baadhi ya nyaraka za mmoja ya wateja waliofika kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa kupitia maonesho ya  kimataifa ya Sabasaba, Malema amesema wamejipanga kutoa huduma mbalimbali  zinazotelewa na wakala hiyo ikiwemo kutoa elimu kwa Umma pamoja na kutoa msaada wa kisheria wa namna ya kuandika na kuhifadhi Wosia.

 

 

WAKALA Wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) wameendelea kuwahudumia wananchi kwa kuwasajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa kwa gharama ya shilingi elfu kumi kwa kila mwombaji kupitia maonesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandshi wa habari katika maonesho hayo  Afisa Mawasiliano kutoka RITA Jafari Malema amesema kuwa, katika maonesho hayo ya kimataifa wamejipanga kutoa huduma mbalimbali  zinazotelewa na wakala hiyo ikiwemo kutoa elimu kwa Umma pamoja na kutoa msaada wa kisheria wa namna ya kuandika na kuhifadhi Wosia sambamba  na masuala ya ndoa na talaka na kubwa zaidi ni kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa.

Amesema, wamejipanga katika kuhakikisha wananchi wote watakaojitokeza wakati huu wa maonesho wanapata vyeti vya kuzaliwa kwa wakati.

''Utaratibu ni uleule tunaoufanya katika ofisi zetu wahitaji wa huduma hii wanatakiwa kuja na viambatanisho au kielelezo kinachomtambulisha yeye,  Kama ni mtoto anatakiwa kuwa na aidha  tangazo la kuzaliwa au kadi ya kliniki pamoja  barua ya Afisa mtendaji wa mtaa anapotokea, kwa mtu mzima anaweza kuja na aidha tangazo la kuzaliwa kama analo, kadi ya kliniki, cheti cha ubatizo, cheti cha kumaliza elimu ya Msingi, kitambulisho cha utaifa au kadi ya kura  pamoja na barua kutoka kwa Afisa mtendaji wa mtaa anapotoka ili tuweze kupata taarifa zake na sehemu anapotoka...Hapo atakuwa na sifa ya kusajiliwa na kupatiwa cheti cha kuzaliwa kwa mujibu wa sheria.'' Amesema.

Aidha amesema baada ya wananchii kusajiliwa wataalam watachakata taarifa hizo na wahitaji kupewa vyeti vya kuzaliwa katika maonesho hayo ya Sabasaba yanayoendelea kwa gharama ya shilingi elfu kumi kwa kila mwombaji bila kigezo cha umri.

''Niwasihi wananchi kufata kanuni na vigezo wakati huu wanapokuja katika maonesho haya na kupata huduma katika banda la RITA,unapokuja kupata huduma wahakikishe wanakuja na vielelezo vinavyoonesha wapi alipozaliwa, tarehe aliyozaliwa na wazazi wake.'' Amesema.

Aidha kuhusiana na watoto wasio na viambatanisho hivyo Malema amewashauri wazazi kurudi mahali walipozaliwa ili kupata barua ya utambulisho na kwa watoto wanaosoma  kuna fomu maalumu ambayo wataiwasilisha katika shule wanazosoma na Mwalimu mkuu kutoa taarifa ambayo Wakala hiyo itakuwa na jukumu la kufuatilia katika Zahanati na hospitali walizozaliwa.

 Kwa upande wake Msajili msaidizi mwandamizi Rehema Ludovick amesema, katika maonesho hayo watasajili na kutoa vyeti kwa wahitaji ambao hawajawahi kupata vyeti hivyo pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya masuala mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kuandika na kuhifadhi Wosia na msaada wa sheria kwa masuala ya ndoa na talaka.

Amesema kwa wahitaji waliozaliwa maeneo ya mipaka Wakala hiyo ipo tayari kuwasaida ili waweze kupata nyaraka hiyo muhimu.

''Kwa waliozaliwa mikoa ya pembezoni ikiwemo Tarime, Kigoma, Namanga, Tanga- Horohoro, Mpanda lazima wawe na viambatanisho vya wazazi na watapata vyeti vyao baada ya kukidhi vigezo kwa kuwa ni haki ya kila mmoja wetu na tupo hapa kwa ajili ya kuwasaida.'' Amesema.

Bi. Rehema amewataka wananchi kutembeleea banda hilo ili waweze kupata huduma na elimu kutoka kwa wataalam ambao wamepiga kambi katika viwanja vya Sabasaba kwa kuwahudumia watanzania.

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la RITA wamepongeza kasi na juhudi za wataalamu wa Wakala hiyo katika kuwahudumia pamoja na kutoa elimu ambayo watanzania wengi wanatakiwa wafahamu ili kila mmoja aweze kumiliki nyaraka muhimu ya cheti cha kuzaliwa na kupata elimu juu ya  umuhimu wa kuandika na kuhifadhi Wosia pamoja na kupata msaada wa kisheria katika masula ya ndoa na talaka.

Wananchi wakipata huduma.Wananchi wakipata elimu na huduma katika banda la RITA katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad