HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 15, 2022

Rais wa Zanzibar ameupongeza utayari wa uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Kiongozi wa Ujumbe wa Wafadhili kutoka Chuo Kikuu cha Hauklend kutoka Nchini Norway Bw.Trond Mohn, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 15-6-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway kujenga Hospitali ya kisasa ya maradhi ya moyo hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway ambao ulimuhakikishia Rais Dk. Miwnyi kwamba uko tayari kuanza ujenzi huo hivi karibuni.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba ujenzi wa Hospitali hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma za maradhi ya moyo hapa Zanzibar na kupunguza kuwasafirisha nje ya nchi wagonjwa wenye maradhi hayo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano kati yake na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland ambao ulianzishwa tokea mwaka 2007 ambao umeweza kuzaa matunda na iko tayari kuuendeleza.

Aliongeza kuwa ushirikiano huo umeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya Hospitali kwa ajili ya akina mama na watoto katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, kusaidia ujenzi na vifaa katika hospitali ya Kidongo chekundu pamoja na kusaidia vifaa tiba kadhaa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa uongozi wa Hospitali hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha na kuendeleza miradi mbali mbali katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuendeleza mafunzo kwa wauguzi na madaktari wazalendo sanjari na kubadilishana uzoefu.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuimarisha mifumo katika sekta ya afya hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Nao uongozi wa Wizara ya Afya ulieleza mahusiano na mashirikiano yaliopo kati ya Hospitali hiyo na Hospitali ya Mnazi Mmoja huku uongozi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja ukieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana baada ya kukamilika na kuanza kazi kwa Hospitali hiyo kutokana na maradhi ya moyo kuwa ni maradhi yalioshika kasi hapa nchini na duniani kwa jumla.

Nao uongozi huo wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hauklend cha nchini Norway ulimueleza Rais Dk. Mwinyi azma yao ya kujenga Hospitali kwa ajili ya kutoa huduma za maradhi ya moyo hapa Zanzibar.

Katika maelezo yao uongozi huo ulimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba wako tayari kuanza ujenzi huo ndani ya mwaka huu kwani wameshajipanga kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa.

Pamoja na hayo, uongozi huo ulisisitiza kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa juhudi zao wanazoendelea kuzichukua katika kuhakikisha wanaendeleza uhusiano na ushirikano uliopo ambao umeanzishwa maalum kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya hapa Zanzibar.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi za Kizazi chenye Usawa (GEF), ikiongozwa na Mwenyekiti wake Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki ambapo ameihakikishia Kamati hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaufikisha Mpango wa Utekelezaji wa Kamati hiyo katika Baraza la Mapinduzi ili Serikali nzima iuelewe kwa undani zaidi na kuufanyia kazi.

Alieleza kufurahishwa na utaratibu wa kupata matokeo yanayotarajiwa kwani ni njia nzuri ya kupata matokeo yanayotarajiwa na pia, ni njia nzuri za kufanya tathmini.

Aliupongeza Mpango wa Kamati hiyo kwa kujikita na mambo muhimu na kueleza kwamba juhudi za makusudi zitafanyika katika kuhakikisha bajeti maalum inawekwa kwa Wizara husika ili kufanikisha Mpango huo.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Angellah Kairuki alitumia fursa hiyo kuitambulisha Kamati pamoja na kumjuulisha Rais jitihada zilizofanyika tangu kuzinduliwa rasmi kwa Kamati hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Disemba 16, 2021 huko Jijini Dodoma.

Alisema kuwa katika kuhakikisha utekelezaji wa ahadi za nchi, Kamati hiyo ya Ushauri ya Kitaifa yenye wajumbe 25 kutoka Serikalini na Asasi za Kiraia, Taasisi za Elimu ya Juu, Taasisi za Utafiti na Sekta binafsi ambapo wajumbe 19 kutoka Tanzania Bara na 6 kutoka Zanzibar imeundwa ili kushauri jinsi ya kuhakikisha ahadi za nchi zinafikiwa.

Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuunda Wizara inayojitegemea inayoshughulikia masuala ya Jinsia, Wazee na Watoto kwani ni chombo muhimu sana katika haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake.

Aidha, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendelea kuwa kinara na mhamasishaji wa kampeni ya ‘He for She’ ambayo ni mkakati muhimu sana katika usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti Kairuki alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Kamati hiyo iko tayari kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha inapata matokeo tarajiwa.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar. OF RESPONSIBILITY

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad