HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 22, 2022

MDEE NA WENZAKE WATUPILIWA MBALI

 

Na Karama Kenyunko Michuzi TV
MAHAKAMA Kuu Masijala Kuu imeyaondoa maombi ya wanachama wa zamani 19 wa Chadema wakiongozwa na Halima Mdee waliokuwa wakiomba kibali cha kufungua kesi mahakamani hapo kupinga mchakato wa kuwavua uanachama kwa sababu ya kasoro za kisheria.

Maombi hayo ya kina Mdee, yaliyowasilishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Mei 12, 2022 yameondolewa leo Jumatano, Juni 22, 2022 na Jaji John Mgeta baada ya kukubaliana na Mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na mawakili wa Chadema wakiongozwa na Peter Kibatala kupinga maombi hayo ya kina Mdee.

Akisoma uamuzi huo Jaji Mgetta alikubaliana na baadhi ya mapingamizi ya Chadema na kusema kuwa maombi ya kina Mdee yalikuwa na dosari ambazo zinaweza kurekebishwa.

Amesema katika maombi yao, Mdee na wenzake walikosea jina la mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Chadema na kwamba wamemshtaki mtu ambaye kisheria hayupo.

"Mdee na wenzake walipaswa kufungua maombi hayo kwa kutaja jina sahihi la bodi hiyo kwa mujibu Sheria ambapo walitakiwa kuandika “Registered Body of Trustees” badala ya Body of Trusties, waliyoandika wao".

Amesema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa kifunga 21 (1) ambacho kinaitaka chama chochote cha siasa kikishapata usajili wa kudumu kiwateue na kuwasajili hao Trustees kwa mujibu wa sheria ya wadhamini.

Pia amesema taarifa hiyo ilisainiwa na mawakili wa waleta maombi kinyume cha sheria na hivyo kufanya iwe na dosari.Hata hivyo alieleza kwamba dosari hiyo wanaweza kufanyia marekebisho.

Katika hatua nyingine mahakama hiyo pia imeondoa mahakamani hapo maombi ya zuio la kutochukuliwa hatua yoyote ikiwemo wabunge hao kubaki na hadhi zao kwakuwa maombi hayo hayana miguu ya kusimamia.

Hoja ambazo jaji alizitupilia mbali ni pamoja na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na hoja kwamba viapo walivyoambatanisha katika shauri hilo havina hadhi kisheria.

Katika kesi hiyo Mdee na wenzake walifungua shauri hilo dhidi ya Bodi ya wadhamini ya Chadema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)

Awali, Kibatala aliwasilisha hoja za mapingamizi ya awali akidai kuwa, Chadema zilikuwa ni maombi ya waleta maombi kuwa batili, mahakama hiyo haina mamlaka ya kuifanyia uchunguzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), nyaraka zilizotumika kufungua maombi kuwa batili.

Viapo vya waleta maombi kuwa batili ikidaiwa zimesainiwa na mawakili badala ya waleta maombi, mahakama haina mamlaka ya kutoa ruhusa kwa qaleta maombi kuleta hoja zao dhidi ya mlalamikiwa WA kwanza (Chadema), sababu haikuwa inafanya kazi ya umma.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad