HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 4, 2022

KIWANDA CHA TUMBAKU MORO KUFUNGULIWA

 Mmiliki na Mwenyekiti Mtendaji Mkuu wa Kampuni mpya ya tumbaku nchini Bw. Ahmed Mansoor Huwel(kushoto) na Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw Richard Sinamtwa(Kulia) wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa soko la tumbaku kwa msimu huu lililofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

MKURUGENZI wa kampuni mpya tumbaku nchini iitwayo Amy Holdings, Ahmed Mansoor Huwel ambaye pia ni mnunuzi wa tumbaku nchini kupitia kampuni yake tanzu ya Mkwawa Leaf amesema atakifungua kiwanda cha tumbaku kilichopo Morogoro kwa ajili ya kuchakata zao hilo.

Amesema hayo jana mjini Tabora wakati wa ufunguzi wa soko la tumbaku inayonunuliwa na kampuni hiyo soko hilo limefunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Batilda Buriani.

"Tumelazimika kukifungua kiwanda cha TTPL kilichopo Morogoro ambacho kilikuwa kimefungwa kwa miaka mitatu, na tumefanya hivyo ili kunusuru wakulima wetu hasa baada ya serikali kutuomba tufanye hivyo," alisema.

Huwel amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kufunguliwa mwezi Julai au Agosti na watafanya hivyo mara baada ya kumaliza ununuzi wa zao hilo wanaoendelea nao hivi sasa na lengo ni kukusanya kilo zisizopungua milioni kumi kwa kuanzia.

Kuhusu utunzaji wa Mazingira, Huwel alisema kampuni yake kwa kuanzia na kwa hali ya dharula, kwa kushirikiana na serikali, Torita na wadau wa tumbaku, itawekeza kwenye tafiti ya udongo kwenye maeneo yote nchini yanayolima tumbaku.

"Tutashirikiana na Torita ili kubaini vionjo halisi vya pembejeo maalum ya tumbaku tofauti ya hali ilivyo sasa, ambapo nchi nzima inatumia aina na idadi ile ile mifuko ya mbolea ya NPK/UREA kwa miaka zaidi ya kumi sasa huku mazingira ya udongo ni tofauti na yanazidi kubadilika," alisema.

Aliongeza kuwa kwa pamoja watafanya kazi bega kwa bega na wakulima kupitimia mfumo wa ushirika na Bodi ya Tumbaku ili kusukuma juhudi za serikali za kubadilisha mabani ya zamani ya kukaushia tumbaku yanayotumia nishati ya miti kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na mabani ya kisasa.

Alisema kwa kufanya hivyo nchi itaweza kuzalisha tumbaku bora na sio bora tumbaku inayoendana na viwango vya kimataifa yaani compliant crop.

Alisema kampuni yake kwa kuanzia itaajiri wafanyakazi wa kuajiriwa wasiopungua 900 na huku wale wa msimu ambao mara nyingi hufanya kazi viwandani watakuwa kati ya 3000 hadi 5000 kutegemeana na msimu ulivyo.

Kampuni ya kitanzania Amy holdings imenunua mali zote za kampuni ya kimarekani Tanzania Leaf Tobacco Company(TLTC) kikiwemo kiwanda cha tumbaku cha Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL).

Kampuni ya TLTC ilifunga biashara zake hapa nchini miaka mitatu iliyopita na hivyo kuwarejesha majumbani zaidi ya wafanyakazi 600, athari ambayo pia iliwakumba maelfu ya wakulima na familia zao ambao walikosa soko la tumbaku yao huku maelfu ya watu wengine kwenye mnyororo huo wa thamani wa zao hilo wakiathirika.Mkuu wa mkoa wa Tabora Dk. Batilda Buriani (wa pili kushoto) akitamka daraja la tumbaku (tobacco grade) kuashiria uzinduzi wa soko la ununuzi wa zao hilo kwa kampuni ya mpya ya tumbaku nchini iitwayo Amy Holdings.Wanaoshuhudia tukio hilo ni Mmiliki na Mwenyekiti Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw Ahmed Mansoor Huwel(wa pili kulia), Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw Richard Sinamtwa(Kulia) na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku nchini Bw Hassan Wakasuvi (kushoto)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad