HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 22, 2022

FANYENI KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

 


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa Wizara hiyo imabeba taswira ya nchi.

Waziri Bashungwa amesema hayo kwenye Kikao kazi na Watumishi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikiwa ni Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambapo kila mwaka huadhimishwa kuanzia Juni 16 hadi 23 mwaka huu.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatunza siri za Serikali na kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma kwa kuwa TAMISEMI imebeba maisha ya watanzania.

Waziri Bashungwa ameendelea kwa kuwataka watumishi hao pia kufanyakazi kwa weledi na kujitoa katika kuwahudumia wananchi na kutojihusisha na rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“TAMISEMI tuna jukumu kubwa la kutoa huduma kwa wananchi niwatake watumishi suala la utoaji wa huduma ni ibada tusimamie katika utendaji wa haki pasina kujihusisha na rushwa Wizara hii ni kubwa ujue ukiwa humu unatakiwa ufuate maadili ya utumishi wa Umma na imani tuwe nayo sababu sisi tunatoa huduma moja kwa moja kwa wananchi wetu” amesema Waziri Bashungwa

Amesema kuwa baadhi ya vitendo vinatokea ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi wa Umma ambapo baadhi ya watu wanaharibu taswira na picha ya Ofisi hii kwa kushiriki kwenye vitendo ikiwemo kugushi barua za uhamisho wa watumishi hivyo, amemuelekeza Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe kulishughulikia kwa haraka suala hilo.

“Ninaelekeza wale wote ambao waliopata barua za uhamisho ambazo tumeshafanya uchunguzi na sio halali warudishwe kwenye vituo vyao vya awali na kama kuna stahiki zozote walipatiwa ambapo ni fedha za Serikali zirudishwa na wachukuliwe hatua” amesisitiza Waziri Bashungwa.
Kwa upande wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. David Silinde amewashukuru watumishi hao kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi hao kuweza kutekeleza majukumu yao ikiwa wao ni moja kwa moja wanawajibika na wananchi amewataka kuendelea kuwahudumia wananchi kwani wana imani na Wizara hiyo.

“Imani ya wananchi ni pamoja na kuwa na imani ya Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan na sisi TAMISEMI tunawajibika moja kwa moja kwa wananchi nitoe rai kwa watumishi wote kufanyakazi kwa weledi kwa kuwa tumeaminiwa hivyo tuaminike” amesema Mhe. Silinde
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe amemuhakikishia Mhe. Waziri kuwa, maelekezo yote aliyoyatoa anaenda kuyasimamia ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma amesema wao kama watendaji watahakikisha wanaendelea kushirikiana na viongozi wa ngazi zote za Wizara hiyo ili kuendelea kuwahudumia wananchi

Akiongea kwa niaba ya watumishi Bi. Namsifu Maduhu(Afisa Utumishi Mkuu) ameushukuru uongozi na kuahidi kutekeleza yale yote yaliyoagizwa kwa lengo la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad