HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 6, 2022

DART ,TANTRADE Watiliana saini Makubaliano kupeleka Mabasi Sabasaba

 Na.Mwandishi Wetu.

WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka DART umetiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano na Mamlaka ya Bisahara Tanzania TanTrade kwaajili ya kupeleka usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka katika maonyesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama sabasaba ili kuwarahisishia wananchi usafiri katika msimu wa maonyesho.

Akizungumza katika hafla kutiliana saini makubaliano hayo iliyofanyika katika Ofisi za Tantrade Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa DART Dkt.Edwin Mhede amesema uamuzi wa kupeleka Mabasi katika viwanja vya sabasaba ni muendelezo wa kutatua kero ya usafiri wa umma katika jiji la Dar es Salaam hasa katika eneo la Mbagala na maeneo ya jirani.

Aidha Dkt.Mhede amesema kupeleka Mabasi katika viwanja vya sabasaba pia ni kutekeleza maagizo ya Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa USEMI ambayo ilifanya ziara hivi karibuni katika Wakala kujionea shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na kutoa agizo hilo.

“Uamuzi wa kuleta Mabasi huku sabasaba ni wa kimkakati kabisa na ni mwanzo wa kuelekea kuleta huduma kamili ya mabasi katika Barabara ya Kilwa itakapokamilika mwezi Machi mwakani, na niwahahakikishie wakaazi wa Mbagala na maeneo ya jirani kuwa usafiri unaanza kuja wakati wa sabasaba na muda si mrefu mkandarasi akikamilisha barabara tutaanza huduma rasmi na kwa viwango vya kimataifa kuliko ilivyokuwa katika awamu ya kwanza” Alisema.

Amesema maonyesho ya sabasaba ni sehemu ambayo inakutanisha watu wengi kutoka sehemu mbali mbali za jiji hivyo Wakala umeona ni vyema kutumia fursa hiyo kuwarahisishia usafiri lakini pia kutangaza huduma.

Katika siku za usoni Taasisi hizo pia zimekubaliana kuendeleza ushirikiano ikizingatiwa maboresho ya miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka yanakwenda sambamba na kuboresha miundombinu na makazi yanayaopakana nayo kwaajili ya kutumia fursa zitokanazo na miundombinu hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Bi.Latifa Mohamed Hamis amesema makubaliano baina yake na DART ni mwanzo wa kuendeleza kutangaza shughuli za biashara katika viwanja vya sabasaba lakini pia ni mwanzo wa kupanua wigo wa shughuli za uchumi katika maeneo yanayozunguka viwanja hivyo.

“Kuendelea kupanuka kwa maendeleo katika eneo hili ni Dhahiri kuwa hata shuighuli za kiuchumi hususan biashara zitaongezeka hivyo wenzetu wakileta Mabasi huku kwetu wataongeza thamani katika ustawi wa jamii inayotuzunguka kwani usafiri karika eneo hili ni changamoto kubwa” Alisema.

Katika kipindi cha maonyesho yam waka huu DART itapeleka Mabasi zaidi ya kumi ambayo yatatoa huduma kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa mbili usiku na wananchi wataweza kununua tiketi za kuingia kwenye maonyesho ya sabasaba wakiwa katika vituo vya mwendokasi vya Kimara, Kivukoni, Morocco,Gerezani, na hata Kibaha, Mloganzila na Mbezi kama kutakuwa na uhitaji huo.

Watumiaji wa Mabasi Yaendayo Haraka kutoka maeneo mbali mbali ya Jiji la Dar es Salaam wamerahisishiwa pia namna ya kuingia katika viwanja vya sabasaba ambapo kimeandaliwa kituo maalum ambacho kiko nje ya viwanja hivyo na wananchi watakaposhuka tu hawatalazimika kukata tiketi watatumia tiketi walizokatia karika vituo mbali mbali vya DART.

Sambamba na wananchi kurahisishiwa ukataji tiketi za kuingia sabasaba pamoja na kuwepo na huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka wametengenezewa pia mlango wao maalum ambapo wakishuka tu kwenye Mabasi wanaingia uwanjani moja kwa moja bila usumbufu wowote, kadhalika kutakuwa na Huduma ya bure ya WiFi katika Mabasi na Katika maeneo yote ya viwanja vya sabasaba.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART Dkt.Edwin Mhede wapili kushoto na Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade Bi.Latifa Mohamed Hamis wapili kulia wakisaini hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo hafla iliyofanyika katika ofisi za Tantrade Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART Dkt.Edwin Mhede wapili kushoto na Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade Bi.Latifa Mohamed Hamis wapili kulia wakionyesha hati za makubaliano kwa waandishi wa Habari (Hawapo pichani )wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano kati ya taasisi hizo iliyofanyika katika ofisi za Tantrade Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad