HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 3, 2022

AFANDE RTO MANYARA APIGA MARUFUKU VING'ORA

 Na Mwandishi wetu, Babati

MKUU wa kikosi cha askari wa usalama barabarani Mkoani Manyara (RTO) Georgina Richard Matagi ametoa onyo kwa madereva wanaoweka ving'ora kwenye magari yao ikiwemo madereva wa magari ya Serikali na kusababisha usumbufu barabarani.

Matagi akizungumza eneo la Bonga kwenye barabara kuu ya Babati-Dodoma amesema amepiga marufuku madereva hao hata wanaoendesha magari ya serikali kutotumia ving'ora mkoani Manyara.

Amesema magari yanayopaswa kupita na msafara na yenye ving'ora yanajulikana hivyo mengine yasiyohusika yasiwekwe ving'ora.

"Polisi ndiyo wanapaswa kuongoza msafara wa viongozi na kuweka ving'ora siyo dereva anakwenda kumchukua Naibu Waziri anawasha king'ora na kusababisha taharuki," amesema Matagi.

Amesema msafara wa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar na Makamu wake, Spika wa Bunge, Jaji Mkuu ndiyo wanapaswa kuongozwa na ving'ora au viongozi wengine wawe na kibali maalum.

Amesema magari ya hospitali, zimamoto, kampuni za ulinzi, migodini au yanayosindikiza fedha benki pia yanaweza kuwa na ving'ora na siyo kila dereva wa gari la serikali anafunga king'ora katika gari lake.

"Dereva anayeingia Manyara kama ana king'ora akitoe akaweke kwenye mkoa mwingine kwani hakuna haja yakusababisha taharuki, wafuate sheria ya usalama barabarani," amesema Matagi.

Amesema serikali ilikataza na kupiga marufuku magari ya watu binafsi na magari ya serikali yasiyo na vibali maalum, ukiacha yale yenye uhalali wa kuwa na ving'ora kuvitumia barabarani.

Mmoja kati ya madereva wa mjini Babati, Vincent Salao amepongeza hatua hiyo kwani ving'ora vilikuwa kero kutokana na baadhi ya madereva kuvitumia ovyo.

"Nampongeza afande RTO wa Manyara kwa hatua hiyo ametimiza wajibu wake kwani madereva wengi hawasiki hadi wapigwe faini," amesema Salao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad