HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 26, 2022

WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UFADHILI WA MASOMO ZINAZOTANGAZWA NA SERIKALI



Balozi Mndeme akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vijana 26 watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani MKURUGENZI wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme amewataka Watanzania kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zikiwemo za ufadhali wa masomo zinazotangazwa na Serikali ili kunufaika nazo.


Balozi Mndeme ametoa rai hiyo leo tarehe 26 Mei 2022 jijini Dodoma alipokutana na wawakilishi wa vijana 26 wanaokwenda nchini Marekani kushiriki mafunzo chini ya Program ya YALI kwa lengo la kuwaaga.

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea kutangaza fursa mbalimbali zikiwemo za ajira na ufadhili wa masomo zinazopokelewa nchini kutoka nchi mbalimbali lakini bado mwitikio wa Watanzania wa kuchangamkia fursa hizo ni mdogo.

“Wizara imekuwa na utaratibu wa kutangaza fursa nyingi za ufadhili wa masomo zinazopokelewa kutoka nchi mbalimbali tunazoshirikiana nazo. Hata hivyo, bado fursa hizi hazijachangamkiwa ipasavyo. Nawaomba Watanzania mzichangamkie fursa hizi pale zinapotangazwa ili zitunufaishe” alisema Balozi Mndeme

Aidha, Balozi Mndeme aliwapongeza vijana hao kwa kufanikiwa kuchaguliwa kushiriki program hiyo ambayo inaheshimika duniani na kuwaeleza kuwa ni fursa nzuri kwao kuitumia kwa ajili ya kujifunza masuala mbalimbali yakiwemo yanayohusu Uongozi ili kupitia wao vijana wengine wengi wa Tanzania wanufaike. Pia aliwaasa kuwa Mabalozi wazuri wa Tanzania, kuzingatia nidhamu na kutanguliza maslahi ya nchi mbele wakati wote wakiwa nchini Marekani.

“Nawapongeza sana kwa kufanikiwa kupata fursa hii. Wizara inafurahi kuona vijana wa Kitanzania mmepata fursa hii kwani pamoja na kuwajenga pia ni ushahidi wa uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani. Nawaasa mkawe mabalozi wazuri wa Tanzania mzingatie nidhamu ili kulinda heshima na taswira nzuri ya nchi yetu” alisema Balozi Mndeme.

Kwa upande wao vijana hao waliishukuru na kuipongeza Wizara kwa ushirikiano iliowapatia na kuahidi kuzingatia mafunzo yote watakayoyapata wakiwa Marekani kwa maslahi mapana ya nchi.

Program ya YALI (Young African Leaders Initiative) ilianzishwa na Serikali ya Marekani mwaka 2010 kwa lengo la kuwawezesha vijana kutoka mataifa ya Afrika kwenda nchini humo kujifunza masuala mbalimbali ya kuwajengea uwezo katika Uongozi. Vijana hao 26 wamechaguliwa kati ya Vijana wa Kitanzania 700 walioomba kujiunga na Program hiyo kwa mwaka 2022.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akizungumza wakati wa kikao kifupi cha kuwaaga Vijana 26 wa Kitanzania (hawapo pichani) waliopata fursa ya kushiriki mafunzo nchini Marekani kupitia Program ya Young African Leaders Initiative (YALI) kwa mwaka 2022. Pamoja na mambo mengine aliwaasa vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini Marekani ili kulinda heshima ya nchi. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma tarehe 26 Mei 2022.

Mmoja wa vijana watakaoshiriki program ya YALI Bi. Victoria akizungumza wakati wa mkutano kati yao na Balozi Mndeme (hayupo pichani)
Sehemu ya wawakilishi wa vijana 26 wa Kitanzania watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Mndeme (hayupo (ichani)
Sehemu nyingine ya vijana hao wakati wa mkutano kati yao na Balozi Mndeme

Vijana watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakifuatilia mazungumzo kati yao na Balozi Mndeme

Sehemu ya vijana hao wakati wa kikao cha kuwaaga

Vijana watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Mndeme alipozungumza nao kwa ajili ya kuwaaga

Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad