HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 27, 2022

WATAALAMU WA MOYO WAONGEZEWA UJUZI WA JINSI YA KUFANYA KIPIMO CHA KUANGALIA MOYO UNAVYOFANYA KAZI KWA KUTUMIA MASHINE YA ECHOCARDIOGRAM (ECHO).

 

Na  Mwandishi Maalum – JKCI

26/05/2022 Dar es Salaam Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo 28 kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao watatu kutoka Hospitali ya Rabininsia na Saifee zilizopo jijini Dar es Salaam wameshiriki mafunzo ya siku moja  upimaji wa moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine hiyo  ya Mindray iliyopo nchini China.

Mafunzo hayo yalifanyika jana katika ukumbi wa JKCI ambapo madaktari hao wamefundishwa njia maalum ya kuwachunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mishipa ya damu ya moyo kuziba.

Akizungumzia mafunzo hayo Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti  wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  Dkt. Peter Kisenge  alisema wataalam hao wamefundishwa njia mpya ambayo sasa hivi inatumika duniani kote kujua uwezo wa utendaji kazi wa moyo kwa kutumia njia iitwayo kitaalam “Sparkle tracking”.

“Mafunzo tuliyoyapa leo yametolewa na daktari bingwa kutoka Misri ambaye amewasilisha mafunzo yake kupitia njia ya mtandao ya zoom pamoja na daktari bingwa kutoka nchini Ethiopia ambaye alitumia mashine ya Echocardiogram kutufundisha kwa vitendo”,

“Kupitia mafunzo haya madaktari wetu wataweza kuwasaidia wananchi wenye uhitaji wa kufanyiwa uchunguzi kwa wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi na hii ni njia ambayo serikali ya awamu ya sita inatumia kuongeza ujuzi mkubwa kwa madaktari wake ili wananchi waweze kufaidika”, alisema Dkt. Kisenge.

Aidha Dkt Kisenge aliwaomba madaktari nchini kujitokeza pale wanaposikia kuna mafunzo ya kibobezi yanapotolewa ili kurahisisha utendaji wao wa kazi lakini pia kuweza kuendana na kasi ya teknolojia kwa kupata mbinu mpya za kitabibu kama ambavyo wataalam walioshiriki mafunzo hayo wamepata na kuweza kujua utendaji kazi wa moyo kwa kutumia njia ya “Sparkle tracking”.

“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutuwezesha kununua mashine hizi zenye uwezo wa  hali ya juu tunazozitumia kuwatibu wagonjwa, matarajio yetu ni kufikisha ujuzi tulioupata hapa leo kwa wataalam wengine wa afya waliopo katika hospitali zetu za mikoa, na wilaya”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Meneja mfumo wa picha za matibabu kutoka kampuni ya usambazaji wa mashine za Echocardiogram  ya Mindray iliyopo nchini China Li Li aliipongeza JKCI kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawafanya madaktari wanaowafanyia upimaji wa kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography - ECHO) kwa wagonjwa kuendana na kasi ya maendeleo ya dunia.

“Kampuni ya Mindray inayotengeneza mashine za ECHO  ina jukumu la kutoa mafunzo pia kwa wadau wake kama tulivyofanya hapa leo ili wadau hawa waweze kuzitumia mashine hizi kwa ufanisi na kupata majibu sahihi ya mgonjwa kwa kumchukuza kila kitu katika moyo wake”,.

“Hii ni mara yetu ya kwanza kuja hapa JKCI kwa ajili ya kutoa mafunzo haya, tunaahidi kuendelea kutoa mafunzo kama haya mara kwa mara kwa kuwaleta madaktari mabingwa tunaofanya nao kazi kutoka pande mbalimbali za dunia ili waweze kubadilishana uzoefu”, alisema Li.

Naye fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist) kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  Paschal Kondi alisema mafunzo yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine za ECHO ya Mindray yamekuwa na faida kubwa kwake kwani ameweza kujifunza njia mbalimbali ya upimaji wa moyo kwa kutumia mashine hiyo hivyo kuongeza ujuzi utakaomsaidia katika utendaji kazi wake wa kazi za kila siku.

“Naushukuru uongozi wa JKCI pamoja na Kitengo cha Mafunzo na Utafiti cha JKCI kwa kuweza kutuandalia mafunzo haya ambayo yatanifanya nifanye kazi zangu kwa ufanisi zaidi na kuwasaidia wagonjwa ambao wanahitaji huduma hii ya uchunguzi wa moyo kupitia mashine ya Echocardiogram”, alisema Kondi.

 

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akizungumza na washiriki wa mafunzo ya upimaji wa moyo wa kuchunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kwa kutumia mashine ya Echocardiogram yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine za Echo ya Mindray iliyopo nchini China. Mafunzo hayo yalitolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Meneja mfumo wa picha za matibabu kutoka kampuni ya usambazaji wa mashine za Echo ya Mindray iliyopo nchini China Li Li akiwafundisha madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) namna ya kuwachunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kwa kutumia mashine ya Echocardiogram wakati wa mafunzo maalum ya siku moja yaliyotolewa kwa madaktari.  
Baadhi ya Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mafunzo ya namna ya kuwachunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri yaliyokuwa yakitolewa na Meneja mfumo wa picha za matibabu kutoka kampuni ya usambazaji wa mashine za Echocardiogram (ECHO) ya Mindray iliyopo nchini China Li Li (hayupo pichani) wakati wa mafunzo maalum yaliyotolewa kwa madaktari hao na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo jana Jijini Dar es Salaam.   
Mtaalam wa Radiolojia kutoka nchini Somalia Dkt. Hassan Abdinur akiwafundisha madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) namna ya kuwachunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine za ECHO ya Mindray iliyopo nchini China. Mafunzo hayo yalitolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akitoa neno la shukrani baada ya kumalizika kwa mafunzo ya upimaji wa moyo wa kuchunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECCHO) yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine za Echo ya Mindray iliyopo nchini China. Mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa jana katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.

  Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambao ni washiriki wa mafunzo ya upimaji wa moyo wa kuchunguza wagonjwa ambao mioyo yao imeshindwa kufanya kazi vizuri kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yaliyotolewa na kampuni ya usambazaji wa mashine za ECHO ya Mindray iliyopo nchini China wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo jana jijini Dar es Salaam.

Picha na: JKCINo comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad