WANANCHI 437 WAMEFANYIWA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA MOYO NA KISUKARI AMBAPO ASILIMIA 60 WAMEKUTWA NA MATATIZO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 31, 2022

WANANCHI 437 WAMEFANYIWA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA MOYO NA KISUKARI AMBAPO ASILIMIA 60 WAMEKUTWA NA MATATIZO

 

Na Mwandishi Maalum – Chalinze, Pwani 
Wananchi 437 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari ambapo asilimia 60 wamekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu (Presha) na asilimia 20 ya waliokutwa na tatizo hilo tayari walishapata madhara ya shinikizo la juu la damu ikiwa ni pamoja na moyo kutokufanya kazi vizuri na kutanuka kwa misuli ya damu ya moyo.

Wananchi wengine walikutwa na matatizo ya matundu kwenye moyo, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake, matatizo kwenye vyumba vya moyo na mishipa ya damu ya moyo kushindwa kupitisha damu vizuri.

Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge wakati wa kufanya tathimini ya zoezi la upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari lililofanyika katika hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha mafunzo na utafiti wa Taasisi hiyo alisema wagonjwa 27 walikutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi na matibabu ya kibingwa na hivyo kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

“Katika upimaji huu tulifanya upimaji kwa watoto 22 ambapo watatu kati yao walikutwa na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake wa kawaida, watoto hawa tumewapa rufaa ya kuja kufanyiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi na kutibiwa katika Taasisi yetu”,.

“Zoezi la upimaji limeenda vizuri mwitikio ni mkubwa wananchi wamekuja kwa wingi na wamefurahia kupata matibabu kutoka kwa wataalamu wetu. Kwa kuwa tatizo la shinikizo la juu la damu ni kubwa nawashauri wananchi waepuke uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe uliopitiliza na kutokula vyakula vyenye mafuta mengi pia wazingatie lishe bora na ufanyaji wa mazoezi kwa kufanya hivi wataepuka kupata magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge alisema Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inaunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuwafuata wananchi mahali walipo kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na kisukari bila malipo yoyote yale kwa kufanya hivi wananchi wengi wataweza kufikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa hayo kwa haraka zaidi.

Naye Mganga mkuu wa Halmashauri ya Chalinze Dkt. Allen Mlekwa aliwashukuru wataalamu waliotoa huduma za upimaji na matibabu kwa wananchi na kusema upimaji huo ulihusisha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI pamoja na wenzao wa Hospitali ya Msoga.

Dkt. Mlekwa alisema waliokutwa na matatizo ya moyo wengine walikuwa na kliniki katika hospitali mbalimbali na walikuwa wanatumia dawa lakini waliacha kutokana na sababu mbalimbali na baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo wamekutwa mioyo yao imetanuka na wengine wamekutwa na ugonjwa sugu wa kisukari. Baadhi yao hawakuwa wanafahamu kabisa kuwa na tatizo la moyo na hivyo waliwaanzishia dawa za kutumia.

“Kuwepo kwa zoezi hili la upimaji kumetufanya tufahamu kunatatizo kubwa la watu wenye matatizo ya moyo na kisukari hivyo basi nasi tumejipanga kuboresha kliniki yetu ya moyo na kisukari iliyopo katika Hospitali ya Msoga kwa siku ya alhamisi ili wagonjwa waliokuwa wanakwenda kutibiwa Hospitali za Tumbi, Amana, Mwananyamala na Muhimbili waje kutibiwa hapa”,.

“Kwa kuwa tuna mashine za kupima vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) na kuchunguza mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) tutawafanyia wagonjwa wenye shida ya moyo vipimo hivi hapa hapa na kama tutawakuta na matatizo makubwa tutawarufaa kwenda kutibiwa katika Hospitali kubwa zaidi”,.

“Wananchi wengine wametoka kilomita zaidi ya 100 karibu kabisa na Tanga na Mvumero wamekuja hapa kwa ajili ya kufuata huduma hii ya upimaji, tutajipanga ili tuweze kufanya mobile kliniki za kwenda kutoa huduma za upimaji katika vituo vya afya vya Msata, Kibindu, Lugoba na Miono kwa kufanya hivi wananchi wengi watafikiwa na huduma za matibabu ya moyo na kisukari”, alisema Dkt. Mlekwa.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma hiyo walishukuru kwa huduma ya uchunguzi na matibabu ya bila malipo waliyoipata na kusema imewapunguzia gharama ya kusafiri na kuwafuata wataalamu Dar es Salaam pamoja na kulipia matibabu hayo.

Fredrin Ikumbera mkazi wa Lugoba alisema alipima vipimo na kukutwa moyo uko sawa lakini amekutwa na shida ya presha amepewada dawa za kutumia pamoja na ushauri wa lishe bora na kuambiwa apunguze matumizi ya vyakula vya wanga pamoja kupunguza kunywa pombe kwani ni hatari kwa afya ya moyo wake.

“Nilikuwa ninawasiwasi kuhusu moyo wangu kwani mazingira niliyokuwa naishi hayakuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu kutumia nafasi za upimaji pindi zinapotokea kwa kwenda kupima afya zao pia kwa upande wa Serikali iendelee kuhakikisha wananchi walioko vijijini wanapata huduma za matibabu ya kibingwa kwani kutokana na mazingira yao ni vigumu kufikiwa na huduma hizi”, alisema Ikumbera.
Afisa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aliston Jovin akiwagawia vipeperushi vinavyoelezea huduma za matibabu zinazotolewa na JKCI wananchi waliofika katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo Msoga kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI katika Halmashauri hiyo iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rahabu Tamba akimpima urefu na uzito mwananchi aliyefika katika Hospitali ya Halmshauri ya Chalinze iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo uliokua ukifanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Chalinze.
 Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Magreth Ng’ondya akimuelezea mwananchi umuhimu wa kutumia dawa za shinikizo la damu wakati wa upimaji wa magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka taasisi hiyo kwa wananchi wa Chalinze kwa siku mbili na kumalizika jana katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo msoga Wilayani Bagamoyo.
 Daktari kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akisoma majibu ya vipimo vilivyofanywa na mwananchi wa Chalinze baada ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kisukari wakati wa upimaji uliyofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi wa Halmashauri ya Chalinze iliyopo wilayani Bagamoyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Tafiti kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwetwe (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimpima mwananchi wa Halmashauri ya Chalinze kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) wakati wa upimaji uliofanywa na wataalam wa moyo kutoka JKCI kwa wananchi hao siku mbili katika Hospitali ya halmashauri hiyo iliyopo Msoga wilayani Bagamoyo.
Wataalam wa moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa upimaji maalum uliofanyika kwa siku mbili kwa wananchi wa Chalinze kuchunguza magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu katika Hospitali ya Halmashauri ya Chalinze iliyopo msoga wilayani Bagamoyo. Picha na JKCI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad