HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 8, 2022

VIJIJI VINNE MKINGA MKOANI TANGA KUPATA MAJI SAFI NA SALAMA

 

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga, Mhandisi Kaijage Mzee akikagua tenki la maji la Mradi wa Maji Parungu Kasela.

Fundi Fred Masawe akiendelea na ujenzi wa tenki la maji la Mradi wa Maji Parungu Kasela, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary akielezea waandishi wa habari namna fedha za ustawi zinavyotekeleza miradi ya maji mkoani humo.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkianga Mkoa wa Tanga, Mhandisi Kaijage Mzee akielezea hatua waliyofikia Mradi wa Maji Parungu Kasela.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkinga Mkoa wa Tanga, Mhandisi Kaijage Mzee akiwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Manza (Katikati) na Mkandarasi wa Mradi wa Maji Parungu Kasela, Mhandisi Fanuel Gasper.
Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Manza Salum Hassan akielezea namna mradi wa Maji Parungu Kasela utakavyowanufaisha wananchi wa Tarafa ya MkingaNa Selemani Msuya, Mkinga


VIJIJI vinne vya Manza, Vuo, Parungu Kasela na Mkinga Leo wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga vinatarajiwa kupata maji safi na salama ifikapo Juni 2025.

Vijiji hivyo vinne vimefanikiwa kupata maji safi na salama kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa fedha za mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Fedha hizo zimetolewa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuomba ili kuhakikisha Sera ya Maji na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayotaka kila mwananchi anachota maji kwa umbali wa mita 400.

Akizungumzia mradi huo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Kaijage Mzee amesema jimbo hilo limepata mradi mmoja unaogharimu Sh.milioni 500 fedha za ustawi ambao utanufaisha vijiji vinne vya Manza, Vuo, Parungu Kasela na Mkinga Leo.

Amesema mradi huo una sehemu kuu nne ambazo ni ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 50,000, kusambaza mabomba ya maji kilomita 12, kujenga chujio na ujenzi wa vituo tisa vya kuchotea maji.

Mhandisi Mzee amesema mkandarasi anatekeleza mradi wa Sh.milioni 383 na zaidi ya Sh.milioni 120 zimetumika kununua mabomba na koki.

“RUWASA Mkinga tumepokea Sh.milioni 500 kupanua Mradi wa Maji Parungu Kasela, ili kuwapatia maji safi na salama wananchi wa vijiji vya Manza, Vuo, Parungu Kasela na Mkinga Leo ambao wana changamoto ya maji,” amesema.

Meneja huyo amesema mradi huo ukikamilika utanufaisha wananchi 6,332 sawa na asilimia 6.7 hivyo kuitaifanya Mkinga kupata maji safi na salama kwea asilimia 66.7 kutoka asilimia 60 ya awali.

Mhandisi Mzee amesema Wilaya ya Mkinga inakabiliwa na changamoto ya vyanzo vya maji hali ambayo inawapa wakati mgumu kusambaza huduma ya maji.

Amesema RUWASA Mkinga wana mpango wa kutumia chanzo cha maji Mowe kusamba katika eneo lote la Horohoro na matarajio yao ni ifiakapo 2025 lengo la kufikisha maji vijijini kwa asilimia 85 litafanikiwa.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Manza Salum Hassan amesema mradi wa maji ambao wamepatiwa utakuwa umekomboa Tarafa ya Mkinga kwa kiasi fulani.

Mtendaji huyo amesema eneo kubwa la Mkinga mjini linakaribiana na Bahari ya Hindi, hali ambayo inasababisha vyanzo vingi vinavyopatikana kuwa na maji ya chumvi.

“Mkinga inashindwa kuendelea kutokana na shida ya maji, imani yetu ni baada ya kukamilika kwa mradi huu wa Parungu Kasela tutapata maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Namshukuru Rais Samia kwa kutuletea mradi huu, ila naomba atusaidie kutoa maji kwenye chanzo cha maji Mto Zigi ili Mkinga yote iwe na uhakika wa maji safi na salama,” amesema.

Hassan amesema RUWASA wanafanya kazi nzuri hivyo wanapaswa kuungwa mkono ili lengo lao la mkutua ndoo mama kichwani liweze kutimia.

Mkandarasi wa Mradi wa Maji Parungu Kasela Mhandisi Fanuel Gasper amesema mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 61 na matarajio yao ni kumalizia asilimia 39 iliyobakia kwa wiki tatu zijazo.

“Mradi huu utamalizika ndani ya muda ambao umepangwa, kazi iliyobakia ni ujenzi wa chujio ambalo naamini ndani ya wiki tatu litakuwa limekamilika na wananchi wa Manza, Vuo, Parungu Kasela na Mkinga Leo kuchota maji bombani,” amesema.

Naye Fundi Fred Masawe amesema mradi huo umemsaidia kupata fedha za kuhudumia familia yake katika mahitaji mbalimbali.

“Nichaoweza kusema ni kumuomba Rais Samia kuendelea kutoa miradi kwa wakandarasi wazawa, ili kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na wananchi wa vijijini,” amesema.

Akizungumzia miradi hiyo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga, Mhandisi Pendo Omary amesema miradi ya maji mkoani hapo inagharimu zaidi ya Sh.bilioni 6.7 na itanufaisha wananchi 80,000.

Mhandisi Omary amesema zaidi ya vijiji 21 vitanufaika na fedha hizo katika majimbo 12 ya uchaguzi ya mkoa huo, hivyo lengo la mkoa kufikisha maji vijijini asilimia 85 na mijini asilimia 95 litatimia ifikapo 2025.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad