Serikali ya awamu ya Sita Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mpango wa kununua ndege mpya na kuifanyia matengenezo nyingine moja kwa lengo la kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao ya wakulima.
Hayo
yamesemwa leo tarehe 28 Mei, 2022 na Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony
Mavunde alipotembelea shamba la Soya na kukabidhi rasmi zana za kilimo
za Chama cha Ushirika cha Msingi cha Wakulima Wanawake Dodoma Mjini
(CHAUWAWADO) katika kijiji cha Narakauo, Kata ya Loiborsiret, Wilayani
Simanjiro, Mkoani Manyara.
Zana
za kilimo ambazo CHAUWAWADO wamezizindua leo zimetokana na mkopo kutoka
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Zana hizo ni Trekta, jembe la
kusawazishia, mashine ya kupanga na jembe la kulimia.
"Nimeisikia
changamoto kubwa mliyoisema juu ya uharibifu wa mazao kutokana na
wadudu wasumbufu,tumejipanga kuimarisha kilimo anga kwa kununua ndege
mpya ya kunyunyiza na kuifanyia matengenezo moja iliyopo ili tuwasaidie
wakulima wa nchi hii kutopata hasara ya uharibifu wa mazao unaofanywa na
wadudu waharibifu.
Tunamshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake wa kuikuza sekta ya
kilimo,hivi sasa bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka Bilioni 294 mpaka
Bilioni 751,haya ni mapinduzi makubwa sana kwenye sekta ya kilimo.
Nimefurahishwa
sana na jinsi ninyi akina mama, mmetoka Dodoma na kuja kufanya kilimo
hapa kijiji cha Narakauo, mmeonesha udhubutu mkubwa. Nawapongeza sana
kwani mmeonesha kwa vitendo namna mnavyounga mkono juhudi za Serikali ya
Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" Alisema Mavunde.
Katika
hatua nyingine, Mwenyekiti wa CHAUWAWADO AMCOS, Bi. Winifrida Kario
alieleza kuwa wameweza kulima ekari 160 za soya, ambazo wameingia
mkataba wa masoko na kampuni ya Dar Lyon na kwamba, wana malengo ya
kuendelea kuongeza eneo la kulima mwaka hadi mwaka. Aidha, alibainisha
moja ya changamoto kubwa ni chama Chao kukosa ardhi, hali inayowafanya
kukodi eneo la kuendesha shughuli zao za kilimo.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt. Suleiman Serera amemuhakikishia
Naibu Waziri Mavunde kuwa atahakikisha CHAUWAWADO wanapata ardhi, na
kuahidi kuendelea kuwasaidia ili waendelee kuzalisha kwa tija na
hatimaye kukuza uchumi wa Kijiji cha Narakauo na wilaya ya Simanjiro kwa
ujumla.
No comments:
Post a Comment