HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 20, 2022

SAYANSI NA TEKNOLOJIA YASAIDIA KUFIKISHA ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
WAKALA wa Vipimo (WMA) wamesema ujio wa Sayansi na Teknolojia umesaidia kufikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kuwafikia kwa kiasi kikubwa wananchi mbalimbali wanaotumia vipimo hivyo katika Sekta ya Biashara tofauti na siku za nyuma.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Meneja wa WMA, Mkoa wa Ilala, Lilian Mwombeki katika maadhimisho ya siku ya Vipimo duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Mei 20. Lilian amesema elimu ya matumizi sahihi ya vipimo imehamasishwa zaidi na ujio wa teknolojia hiyo na kuikomboa sekta hiyo ya biashara kwa vipimo sahihi.

"Mfano hapa mkoa wa Ilala, katika tafiti zetu kwa sasa kwa mwezi mmoja WMA inaweza kuhakiki vifaa ambavyo vipo mtaani ambavyo ni Mizani, Pampu na vifaa vingine mbalimbali zaidi ya Elfu 7 (7000) hadi Elfu 8 (8000) tofauti na miaka ya nyuma tulikuwa tunakusanya na kuhakiki vifaa hivyo kutoka mtaani mia 5 (500) hadi mia 6 (600)", amesema Lilian.

Amesema idadi kubwa ya wananchi wameelimika kutokana na ujio wa digitali, idadi kubwa inafahamu wajibu wao kuhusu vipimo ili kunufaika wao na mtumiaji au mlaji wa mwisho wa bidhaa hizo zilizopimwa katika vipimo sahihi.

"Zamani watu walikuwa wanapima bidhaa mbalimbali bila kuwa na Mizani inayotumika kwa vipimo sahihi, wengi walikuwa wanapima bidhaa kama Nyanya, Dagaa kwa kutumia Kopo, lakini kwa sasa ujio wa teknolojia watu wengi wameelimika wanatumia vifaa hivyo katika vipimo", ameeleza Lilian.

Kwa upande wake, Afisa Vipimo - WMA, Mkoa wa Ilala, Dennis Mtatilo amesema WMA inafanya kaguzi mbalimbali kuhakikisha Sheria na taratibu za vipimo sahihi zinafuatwa ili kumnufaisha watumiaji wa vipimo hivyo sanjari na matumizi sahihi ya vifaa kisasa ambavyo vimerahisisha upimaji wa bidhaa mbalimbali kwa kiasi kikubwa.

Mtatilo amesema "Sisi huwa tunahakiki namna bora ya ufungashaji kwa mujibu wa Sheria, kuna viwango vimewekwa lazima vifuatwe ili kuwa na biashara shindani".

Naye, mmoja wa watumiaji wa vipimo hivyo katika bidhaa mbalimbali za Sekta ya Ujenzi, Afisa Mauzo wa Kampuni ya FMJ Hardware Limited, Athumani Kanyelele amesema wanahakikisha wanatumia vipimo sahihi na vyenye ubora ili kunufaika wao na Wateja wanaotumia bidhaa zao.

Siku ya Vipimo duniani iliasisiwa mwaka 1875 baada ya Mataifa mbalimbali duniani kukubaliana kuwa na vipimo sawa na kutotofautiana katika vipimo hivyo.

Kwa mwaka huu wa 2022, Kaulimbiu ni Vipimo katika Karne ya Kidigitali.
Meneja wa WMA, Mkoa wa Ilala, Lilian Mwombeki (Wa kwanza kutoka kushoto) akishuhudia upimaji wa bidhaa ya Chuma , katika Kampuni ya FMJ Hardware Limited iliyopo jijini Dar es Salaam, wanaopima bidhaa hiyo ni Afisa Vipimo - WMA, Mkoa wa Ilala, Dennis Mtatilo (Kushoto) na Afisa Vipimo - WMA, Mkoa wa Ilala, Alfred Mbena (Kulia) wengine ni Afisa Mauzo wa Kampuni ya FMJ Hardware Limited, Athumani Kanyelele (Aliyevaa Miwani).
Afisa Vipimo - WMA, Mkoa wa Ilala, Alfred Mbena (wa kushoto) akipima bidhaa ya Bomba kwa kutumia vifaa vya kisasa, katika Kampuni ya FMJ Hardware Limited iliyopo jijini Dar es Salaam, anayeshuhudia kulia ni Meneja wa WMA, Mkoa wa Ilala, Lilian Mwombeki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad