HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 7, 2022

MRADI WA MAJI MAKONDE MKOANI MTWARA WAANZA KUFANYIWA UKARABATI

 

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahil Geraruma wa pili kushoto,akikagua miundombinu ya maji ya Makonde wilayani Newala mkoa wa Mtwara inayofanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya kuongeza na kuboresha huduma ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa wilaya ya Newala.

Na Muhidin Amri, Newala
SERIKALI kwa kushirikiana na Shirika la CI Imate Resilient Infrasturcture Development Facility(CRIDF)la nchini Afrika Kusini,imeanza kufanya ukarabati wa mradi mkongwe wa maji Makonde wilaya ya Newala mkoani Mtwara kwa lengo la kuboresha uzalishaji na kuboresha huduma ya maji.

Akizungumza jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji Makonde wilayani Newala Mhandisi Seleman Kajete alisema,chanzo cha maji Mitema kilijengwa mwaka 1984 kwa ufadhili wa Serikali ya Finland kinahusisha visima virefu sita vyenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 11,800 kwa siku.

Alisema,mradi huo una vyanzo vitatu ambavyo ni Mkunya,Mahuta na Mitema kwa sasa unahudumia wakazi wapatao 490,948 wa wilaya ya Newala na Tandahimba,ambapo chanzo cha Mitema ndicho kinachotegemewa kuhudumia eneo lote la Makonde.

Aliongeza kuwa,chanzo hicho kina maji ya uhakika yanayotosheleza mahitaji ya wananchi wote na gharama za uzalishaji na uendeshaji wake ni nafuu ikilinganisha na vyanzo vingine.

Kwa mujibu wa Mhandisi Seleman,awamu ya kwanza ya ukarabati huo ulikuwa katika visima vyote sita kwa kufunga pampu mpya na marekebisho ya mfumo wa umeme na mfumo wa bomba toka kwenye visima hadi eneo la kutibu maji na kazi zote zimekamilika.

Alisema,katika awamu ya pili iliyoanza mwaka wa fedha 2018/2019 imehusisha kazi ya ulazaji wa bomba jipya umbali wa km 6 Mitema-Nanda,ulazaji bomba jipya umbali wa km2 kutoka Nanda hadi Mtopwe na ukarabati wa matanki 3 ya kuhifadhia maji kijiji cha Mitema.

Aidha alitaja kazi nyingine ni ukarabati wa mfumo wa umeme katika nyumba ya mitambo Mitema,kukarabati mfumo wa kutibu maji katika nyumba ya Madawa-Mitema,kufunga mita kubwa njia ya Mitema-Nanda na Mitema-Mtongwela na Mitema-Kilindu na kufanya ukarabati wa miundombinu ya bomba ndani ya nyumba ya mitambo Mitema.

Alisema,kukamilika kwa mradi huo kutasaidia sana kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Newala na vijiji vilivyopo katika Halmashauri ya wilaya Newala na Tandahimba.

Ameiomba Serikali tenga fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji Makonde,ili kumaliza kabisa tatizo la maji kwa wananchi wanaotegemea kupata huduma ya maji kupitia mradhi huo.

Amewaomba wananchi kuwa na imani kwa Serikali yao juu ya utatuzi wa shida ya maji katika wilaya ya Newala na Tandahimba, kwani kuna miradi inayoendelea kutekelezwa na mingine imepangwa kuanza kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha.

Alisema,Mamlaka ya maji Makonde kwa kushirikiana na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) wilaya ya Tandahimba na Newala, watasimamia mradi huo na kuhakikisha wananchi wa wilaya hizo wanapata huduma ya maji iliyo bora na endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad