HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 23, 2022

MACRA Yabainisha Utayari kushirikiana na Tanzania kufikisha ‘Data’ Malawi

 
Ujumbe wa Maafisa Waandamizi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Malawi (MACRA) ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Daud Suleman umeihakikishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuwa inayo nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikisha huduma za data zenye gharama nafuu na salama nchini Malawi.

Wakizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania aliewakilishwa na Kaimu wake Modestus Ndunguru kwenye ofisi za makao makuu ya TCRA jijini Dar es salaam hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa MACRA alibainisha kuwa huduma za data nchini Malawi ni rasilimali adimu hivyo wameazimia kuondoa changamoto za mtandao hasa upatikanaji wa intaneti nchini mwao kwa kushirikiana na Tanzania ili kufikisha huduma nafuu za data/intaneti nchini Malawi.

“Lengo la ziara yetu ni kuona namna tunavyoweza kushirikiana katika kuimarisha huduma za Mawasiliano nchini kwetu, Malawi matumizi ya intaneti yapo kiwango cha chini na ni watu wachache wanaofikiwa na huduma hizi” alibainisha Daud.

Ujumbe huo ulibainisha kuwa ni kiasi cha takribani watu milioni kumi pekee ndio wameunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti, hivyo lengo la ziara yao ni kujifunza na kwa kadri itakavyofaa kuona namna wanavyoweza kuingia makubaliano na Tanzania kupitia taasisi zake za Mawasiliano ili kufikisha huduma za Mawasiliano Malawi.

Huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi sasa zinazifikia takribani nchi nane zinazoizunguka Tanzania, ambapo hatua ya Malawi kuonyesha nia ya kuhitaji huduma hiyo kunaongeza idadi ya nchi jirani kwa Tanzania zinazofikishiwa huduma za Mawasiliano kupitia mkongo wa taifa wa Mawasiliano hadi kufikia tisa.

Haya yanajiri wakati serikali ikiwa tayari imebainisha kuboresha mbinu za kusambaza kwa haraka mkongo wa Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupitisha nyaya za Mawasiliano kupitia miundombinu ya Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye aliyebainisha haya wakati akiwasilisha bajeti ya wizara anayoiongoza hivi karibuni.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Modestus Ndunguru aliueleza ujumbe huo kuwa, TCRA ipo tayari kuwapa ushirikiano stahiki ili kufanikisha azma hiyo ya kufikisha huduma za data nchini Malawi kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania.

“Tayari tunashirikiana na nchi kadhaa jirani katika Mawasiliano na bila shaka suala hili litafanikiwa na tutaona nchi zetu hizi zikipiga hatua katika sekta ya Mawasiliano” aliongeza Ndunguru.

Katika ziara hiyo ambayo pia ililenga kujifunza masuala mtambuka ya Mawasiliano ujumbe huo ulipata fursa ya kuwatembelea watoa huduma za Mawasiliano kadhaa zikiwemo kampuni za simu na watoa huduma za data likiwemo shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL.

“Kwa kweli tumefurahia ziara yetu imekuwa yenye mafanikio kwa kuwa tumejifunza mengi na kuona uwezekano wa kuongeza ushirikiano baina yetu; tunakwenda nyumbani kubainisha uchaguzi na kipaumbele chetu kwa kadri tulivyojifunza na kuona ili turejee kukamilisha makubaliano ya ushirikiano huu muhimu” alinasbisha Andrew ACN mratibu wa ziara hiyo.


Ujumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi (MACRA) ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Daud Seleman (mwenye koti jeusi alieketi) ukiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dar es salaam ulipowasili kwa ajili ya mazungumzo yanayolenga kuipatia Malawi huduma za data kutoka Tanzania. PICHA NA TCRA


Ujumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi (MACRA) katika mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Modestus Ndugu wakati walipofika kwa ziara ya kujifunza na kudumisha ushirikiano. Malawi imeonyesha nia ya kuunganishiwa huduma za mtandao/data kutoka Tanzania. PICHA NA TCRA


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad