HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 8, 2022

KIDATO CHA SITA, WALIMU KUFANYA MTIHANI KESHO MEI 9 HADI 27, 2022

 JUMLA ya watahiniwa 95,955 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2022 ambao unatarajiwa kuanza kesho Mei 9 hadi Mei 27 ukihusisha shule 841.


Mtihani huo unakwenda sambamba na mitihani ya kuhitimu ualimu ambapo jumla ya watahiniwa 9670 wa vyuo 70 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo kwa ngazi ya stashahada na cheti.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Mei 8, 2022 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde amesema maandalizi yote yameshakamilika na wamejipanga kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika bila kuwepo udanganyifu.

Amesema kati ya waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, kati yao watahiniwa 85,531 ni watahiniwa wa shule na 10,424 ni wa kujitegemea.

Ngazi ya stashahada waliosajiliwa ni 4560, wanaume ni 2960 sawa na asilimia 64.91 wanawake wakiwa 1600 sawa na asilimia 35.09 wakati ngazi ya cheti waliosajiliwa ni 5110 wakiwemo wanaume 2336 na wanawake 2774 huku watahiniwa wa ngazi ya cheti wenye uoni hafifu wakiwa wawili na wasioona wawili.

Dkt. Msonde ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya taifa zinazingatiwa.

Amesema mitihani ya kidato cha sita ina umuhimu mkubwa kwa kuwa licha ya kupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi ndiyo unaowezesha wanafunzi kwenda vyuo vikuu ambako wanazalishwa wataalam.

Dk. Msonde ametoa wito kwa wasimamizi wote wa mitihani kufanya kazi kwa weledi wa hali juu huku wakizingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa na wa wahakikishe wanatenda haki kwa watahiniwa wenye mahitaji maalum.

Katibu huyo amesema, wamiliki wa shule wanatakiwa kutambua shule ni kituo cha mtihani hivyo kwa namna yoyote ile hawatakiwi kuingilia majukumu ya usimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mitihani hiyo.

Pia Dk. Msonde amewaasa wamiliki wa shule, walimu, wasimamizi wa mitihani na wananchi kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mitihani, kwani Baraza halitasita kuwachukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kujihusisha au kusababisha udanganyifu wa mtihani hii.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza kuanza kwa mitihani ya Kidato cha sita 2022

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad