HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 26, 2022

DC MSAFIRI AWAPA AHUENI YA USHURU WAFANYABIASHARA WANAOTUMIA BODABODA KUSAFIRISHA MKAA

 Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Mkuu wa wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri ameshusha ushuru wa maliasili unaopaswa kulipiwa na wafanyabiashara na wabebaji wa mkaa wanaotumia bodaboda maarufu( WAKUBETI ),kutoka 37,500 Hadi 30,000 ili kupunguza utitiri wa tozo zinazowakabili na kuwasababishia kukwepa ushuru kwa kupita njia za panya.

Akiingilia kati mgogoro huo, huko Kwala baada ya wafanyabiashara wa mkaa kugomea ushuru mpya ya sh.37,500 kutoka ushuru wa zamani ya 25,000, Msafiri alilazimika kutoa maagizo manne yanayolenga kujenga mahusiano baina ya pande hizo mbili.

Agizo jingine Ni kuvunja uongozi uliopo wa wafanyabiashara wa mkaa kwa like alichodai umekiuka sheria kwa Kuwa miongoni mwa wanaofanya vurugu na kuisababishia hasara Serikali kutokana na kugomea kulipa ushuru wa Serikali.

Hatua hiyo imekuja kufuatia Wakala wa Misitu TFS Kibaha kuingia katika msuguano na wafanyabiashara hao ambao wamesusia kupita getini na kuamua kupita vichochoroni kukwepa ushuru ndani ya mwezi mmoja Sasa.

Vilevile aliwasihi ,wafanyabiashara hao kuunda vikundi ili vijisajili rasmi na kuanza kulipa kwa mwaka mpya wa fedha kiasi kinachotambulika kisheria sh.361,000 na walipe kwa awamu mbili .

Msafiri alitoa tamko kuanzia sasa kituo kikuu Cha kuuzia mkaa Ni Mlandizi badala ya kuhangaika na pikipiki kwenye barabara kukimbilia soko Mbezi na kwingine.

Mkuu huyo wa wilaya alisema ,hataki kusikia wanakwepa ushuru ,kutumia njia za panya kwani inasababisha hasara kwa Serikali kwa kupoteza mapato mengi.

Hata hivyo alielezea , tozo mbalimbali zilizokithiri 183,000 kwa mfanyabiashara huyu biashara hiyo haimlipi na hawawezi kutoboa kimaisha.

"Tunakimbilia ushuru mkubwa huku walengwa wanakwepa ushuru ,Ni vyema kuweka gharama rafiki ili kuongeza mapato,";Mwezi uliopita TFS mlipata milioni 38.8 kwa mwezi Sasa mwezi huu mapato yameshuka milioni 24 hiii inatokana na ushuru huu Kuwa mkubwa , na kupelekea msuguano ,"alifafanua Msafiri.

"Nakubali kuvunja sheria,kuingilia Mamlaka nyingine,navunja jongoo kwa meno ,kwa sababu yenu na viongozi mliopo madarakani ,nyie viongozi ndio Daraja Lakini mmegeuka Kuwa wafanya vurugu ,sitokubali nashusha ushuru na nyie mtoke madarakani,kuanzia sasa mchague viongozi wengine"

"Nimesikia hapa mbunge wenu wa Kibaha Vijijini Mwakamo ,alifika hapa mkapanga viongozi na kushauriana viongozi hao wachangiwe fedha waende Dodoma ili kukutana na kamati ya maliasili ya bunge "

Msafiri alisema kwamba ,kwa kushindwa kutekeleza Maamuzi waliojiwekea na Kuwa sehemu ya waliogoma ,nawawajibisha ,na kuanzia sasa wachaguliwe viongozi wapya.

Awali ,WAKUBETI akiwemo Hosea Paulo na Yasin Rajabu alisema , wamekuwa wakichanganywa na Uongozi wa TFS na kusababisha kukwepa ushuru.

"Tunapigwa na migambo , pikipiki zetu zinachujuliwa ,zipo pikipiki Kama 400 huko wanazotubebea na kutulipisha faini ,tozo nyingi zinatuzidia tunajikuta tunapata Faida sh.18,000 Hali hii Ni mbaya," Kutokana na hali hiyo tunaamua kupeana pikipiki unamlipa mwenye pikipiki ,Sasa hata Kama Ni wewe mkuu utapita getini kulipia au utachepuka kichochoroni !?alihoji Hosea.

Walieleza ,ushuru wa awali ulikuwa 12,500 baadae wakaanza kulipia 25,000 na Sasa Bei kandamizi Ni 37,500 ambayo ni kubwa .

Nae Yasini alibainisha kwamba ,licha ya hayo bei ya shamba nayo ni kubwa 90,000 wakati zamani walilipia 60,000 .

"Mimi Ni mwanaume , familia yangu inahitaji huduma nzuri , huwezi amini mkuu ushuru tunaolipa sisi Ni zaidi ya 180,000 ili kupeleka mzigo sokoni, kwa hali hii ya utitiri wa ushuru hatuwezi kutoboa,Tunashindwa na inabidi kufanya vurugu ili kuweza kujiendeleza kimaendeleo"alieleza Yasini.

Akijibu hoja hizo Meneja wa TFS Kibaha ,Mukama Kusaga alifafanua kila kikundi kilichojisali kina fomu na anaepewa adhabu ni yule ambae hajapata usajili.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya misitu na.14 ya mwaka 2002 na kanuni zake mfanyabiashara wa mkaa anatakiwa kulipa sh.250 kwa kila kilo ya mkaa au 12,500 kwa gunia lenye kilo 50.

Alisema , kwasasa wapo wafanyabiashara hao 250 ambao husafirisha mkaa kwa kutumia pikipiki na wameshakamata bodaboda 45 na sio 400 na faini ni milioni moja kukomboa pikipiki moja.

Kusaga alikana malalamiko ya kuambiwa wanapeleka mgambo shamba kwenye Misitu na kuwapiga baadhi ya wafanyabiashara wa mkaa , amesisitiza hawajawahi kupeleka mgambo kupiga watu labda iwe mhusika anafanya vurugu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad