HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 6, 2022

BoT YAENZI MIAKA 100 YA MWALIMU NYERERE KWA KUANDAA KONGAMANO MAALUM, WAGUSIA MFUKO WA UFADHILI WA MASOMO

 
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

WADAU mbalimbali wakiwemo , viongozi na watu mashuhuri wamekutana kwenye Kongamano maalumu ambalo limeandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa lengo la kuenzi miaka 100 ya Mwalimu Julius Nyerere hasa katika kutambua mchango wake katika masuala kadhaa yakiwemo ya kiuchumi.

Wakizungumza wakati wa Kongamano hilo lililofanyika Ukumbi wa BoT ,wadau mbalimbali wamepata nafasi ya kumuelezea Mwalim Nyerere na harakati zake katika kukuza na kuimarisha uchumi wa Tanzania kupitia sekta ya fedha.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luwoga pamoja na mambo mengine ameeleza kwa kifupi sababu za kuandaa Kongamano hilo ambapo amesema katika kufanikisha majadiliano katika kongamano hilo waliamua kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo waandishi wa vitabu vya Mwalimu Nyerere.

“Kwa sababu kwanza wakati Rais Samia Suluhu Hassan anavizindua vitabu vya Mwalimu Nyerere kule Kibaha, hivi vitabu vilikuwa havijatambulishwa na wananchi wengi walikuwa wanaona tu yale majuzuu matatu lakini kwa kawaida unapoona majuzuu namna ile mtu wa kawaida inampa uvuvi wa kununua asome

“Lakini ukivitambulisha wananchi wanajua nini kilichomo na kuna nini kinaweza kupatikana kwenye hicho kitabu, hivyo benki kuu imeona iandae huu mjadala katika moja ya kumuezi Mwalimu Nyerere.

“Benki kuu kwa namna ya pekee imekuwa ikihakikisha inamuenzi Mwalimu Nyerere kwanza kwa kuweka mfuko wa ufadhili wa masomo kwa ajili ya kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana ambao wengi wana uwezo na wanaweza kuendelea kuihudumia nchi hii kupitia Benki Kuu ya Tanzania au kupitia taasisi nyingine za umma.

“Kupitia ufadhili huo vijana wetu wa kitanzania wanasoma fani mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, sayansi na fani nyingine .Hivyo kupitia kongamano hili imekuwa nafasi nzuri kuujulisha umma kuhusu Mfuko wa Ufadhili wa masomo wa Mwalimu Nyerere ambao uko hapa Benki Kuu, lakini kama ratiba ilivyo litatolewa tamko hukusu mfuko huu,”amesema Gavana .

Ameongeza wakati wanatambulisha vitabu vya aina ya pekee kwa jinsi vinavyomuelezea Mwalimu Nyerere kwa nafasi yake kama Kiongozi na nini alipitia na jinsi gani aliweza kuhakikisha nchi inaelekea kwenye malengo ambayo Mwalimu alikuwa nayo.

Kuhusu mahusiano kati ya Mwalimu Nyerere na BoT, Gavana Luwoga amesema huwezi kuizungumzia Benki Kuu ya Tanzania bila Mwalimu kwa sababu kabla ya benki hiyo kuanzishwa masuala yote yaliyohusu fedha yalikuwa chini ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.

“Lakini baada ya kupata uhuru Mwalimu aliona umuhimu wa kuhakikisha kuwa na Benki Kuu ya Tanzania ili Serikali iwe na uwezo mkubwa wa kuendesha uchumi wake. Huwezi kuendesha uchumi bila kuwa na Sera yako ya fedha na kutoa sarafu yako mwenyewe.

“Kwa hiyo Mwalimu hata kabla ya Uhuru mazungumzo yalishaanzishwa kwamba tukipata uhuru tuwe na Benki Kuu yetu .Utashi wa kiongozi unahitajika vinginevyo unaweza kuwa na Benki Kuu ambayo haina uhuru wa kusaidia katika kuimarisha ama kuwa na uchumi imara.

“Hivyo kuanzia mwaka 1965 wakati inaanzishwa Benki Kuu majukumu yake yalipewa kwa kushirikisha uongozi wa nchi na baada ya pale kila sheria ilipobadilika ilikuwa ni kuongeza majukumu na Serikali kuheshimu ule uhuru wa Benki Kuu.

“Ili kuhakikisha uchumi unaimarika, sarafu yetu inaimarika, thamani ya fedha, uhimilivu wa bei, riba na mambo yote hayo Benki Kuu inatakiwa kuyatekeleza kwa weledi bila muingiliano mkubwa na Serikali.Hivyo huwezi kuizungumzia Benki Kuu bila kuzungumzia maono ya kiongozi aliyeanzisha benki hii,”amesisitiza.

Kwa upande wake Profesa Issa Shivjj amesema uamuzi wa BoT kuandaa mdahalo kupitia Kongamano hilo la kuenzi miaka 100 ya Mwalimu Nyerere ni mwanzo mzuri sana kwani huwezi kutengenisha sekta ta fedha na mambo mengine ya hali ya nchi.

“Na huwezi kutenganisha sekta ya fedha bila kujua histori , na kongamano la leo ingawa limejikita katika historia ya Mwalimu lakini ni muhimu kwani linafundisha mambo muhimu. Kama nilivyochangia kwenye mchango wangu kuna mambo katika sekta ya fedha lazima tuyafahamu kwa mfano tulipotaifisha benki wakati ule leo tunahitaji kujua ilivyotokea na benki kutoka nje walivyopambana hadi wakasalimu amri.

Hata hivyo amesema kuwa unaposoma vitabu vya Mwalimu Nyerere kwa sehemu kubwa unaona wananchi na watu wa Tanzania walivyopambana wakiongozwa na Mwalimu Nyerere , kwa hiyo mapambano bado yanaendelea.

“Kwa upande wangu nawasihi vijana wasome hiyo historia ili wasione nchi wanayoitaka itapatikana kama zawadi bali itapatikana kwa mapambano na hii naaminisha sio watu wengi tutafaidika lakini lazima tupambane ili vizazi vijavyo vifaidike kwa kuwa na nchi wanayoitaka,”amesema




Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga akitazama na kununua baadhi machapisho ya vitabu mbalimbali vya Mwalimu Nyerere baada ya kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi pamoja na uchambuzi wa vitabu lililofanyika kwenye ukumbi wa benki hiyo jana Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo liliandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Taasisi ya Mkuki na Nyota na nyinginezo.Katika Kongamano hilo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo vitabu vitatu vilivyoandika wasifu Mwalimu Nyerere, vilivyozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MMG



Baadhi ya Wadau mbalimbali wakiangalia na kununua machapisho ya vitabu mbalimbali vya Mwalimu Nyerere


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga akizungumza na Wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Taaisisi mbalimbli jana Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Profesa Florens Luoga akizungumza wakati akifungua kongamano la kumbukizi ya miaka 100 ya Mwalimu Nyerere iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa BoT.


Prof. Saida Yahya-Othman akimuelezea Hayati Mwalimu Nyerere kwenye Kogaamano hilo, anasema Baba wa Taifa alikuwa muasi tokea akiwa mdogo ambapo alijikitia kupinga ukandamizaji na dhuluma zilizokuwa zimewekwa na wakoloni katika maeneo mbalimbali ya shule,makanisani na vyuoni.Amefafanua kuwa, uasi ambao aliufanya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere haukuwa kwa manufaa yake, bali kwa manufaa ya jamii na ustawi bora wa Taifa likiwemo Bara la Afrika kwa ujumla.


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mkuki na Nyota, Walter Bgoyaakieleza alivyobahatika kufanya kazi katika miaka miwili ya mwisho wa maisha yake ya Baba wa Taifa, anasema Mwalimu Nyerere alilipa kipaumbele suala la utu, usawa na haki katika kukuza amani na utulivu nchini, kwa sababu kusipozingatiwa kunaweza kuleta uvunjifu wa amani au vita katika Afrika. Alisema kutokana na kuendelezwa maono ya Mwalimu Nyerere, Tanzania imekuwa mahali salama na kimbilio la nchi rafiki za Afrika wakati wanapopata shida kwao kama nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na nyinginezo.

Dkt. Ng’wanza Kamata kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam akieleza mambo mbalimbali aliyoyapitia Hayati Baba wa Taifa kwenye Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 100 ya Kuzaliwa Mwalimu Nyerere katika mtazamo wa kiuchumi pamoja na uchambuzi wa vitabu lililofanyika kwenye ukumbi wa benki hiyo jana Mei 5,2022 jijini Dar es Salaam. Kamata amesema kuwa, Hayati Baba wa Taifa alipitia nyakati nyingi kabla na baada ya Uhuru na kote huko alishinda."Mwalimu Nyerere alikuwa anapata upinzani mkubwa na vitisho vingi. Wakati mwingine alijibu kwa ukali na alifanikiwa kushinda kwa sababu alikuwa na uwezo wa kipekee,"amesema.

Sehemu ya Meza Kuu, Kutoka kulia ni Prof. Saida Yahya-Othman,Gavana wa Benki Kuu Prof Florens Luoga pamoja na Prof.Issa Shivji wakifuatilia mijadala iliyokuwa ikiwasilishwa kwenye kongamano hilo.




Wadau mbalimbali wakifuatilia kwa makini yaliyokuwa yakijiri kwenye Kongamano hilo .
PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MMG

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad