HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 15, 2022

WAFANYABIASHARA MKOANI DODOMA WAHIMIZWA KWENDA KUFANYA MAKADIRIO NA KULIPA KODI ZAO STAHIKI

 


Na. Mwandishi Wetu-DODOMA.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka Wafanyabiashara mkoani Dodoma ambao mpaka sasa hawajafanyiwa makadirio kufika mapema katika ofisi za TRA kwa ajili ya kufanyiwa makadirio na kulipa kodi zao za malipo ya kodi katika Awamu ya Kwanza.

Wito huo umetolewa jana mjini Dodoma na Afisa Mkuu Msimamizi wa Kodi wa TRA, Bw. James Ntalika wakati wa mwendelezo wa Kampeni ya Utoaji Elimu kwa Mlipakodi ya kuwatembelea Wafanyabiashara katika maeneo yao ya kazi maarufu kama “Mlango Kwa Mlango” yenye lengo la kuwapatia elimu ya kodi ikiwemo kusikiliza na kuzitatua kero zao.

Bw. Ntalika alisema kwamba, ili kuepuka kero na msongamano katika ofisi za TRA wakati wa makadirio ni vema wafanyabiashara wakafika mapema katika ofisi za TRA kupatiwa makadirio yao na kwenda kulipa kodi zao stahiki kabla au mnamo tarehe 31 Machi mwaka huu.

“Kwa sasa tunachokizangatia katika utoaji wa elimu ya kodi ni kuwakumbusha wafanyabiashara wote kwenda kupata makadirio ili waweze kulipa kodi zao stahiki kwa wakati, na tunawahimiza wafanya hivyo ili kuwaondolea usumbufu wa kulipa siku ya mwisho”, alisema Ntalika.

Kwa upande wao baadhi ha Wafanyabiashara wametoa maoni yao mbalimbali kuhusiana na zoezi la kupatiwa elimu ya kodi ikiwemo kukumbushwa kwenda kufanya makadirio na kulipa kodi ambapo wamesema kwamba, zoezi hilo ni zuri kwani linawajengea uwezo wa kielimu kuhusu masuala ya kodi na wengine wao wameiomba TRA kuwasogezea huduma ya kufanyiwa makadirio ili kuwapunguzia muda na umbali wa huduma hiyo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea na kampeni yake ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango ikiwa na lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kukuza wigo wa walipakodi nchini ambapo zoezi hilo kwa sasa lipo katika mikoa ya Dodoma na Manyara kuanzia tarehe 07 Machi, 2022 hadi tarehe 18 Machi, 2022.



Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Edwin Iwato (kushoto) akimuelimisha Mfanyabiashara wa vipuri vya magari na vilainishi kuhusu kwenda kufanya makadirio ya kodi mapema ikiwemo kutoa risiti za kodi za kielektroniki za (EFD) wakati alipomtembelea katika duka lake lililopo katika barabara ya Bahi mjini Dodoma wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo.



Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Maya Magimba (kulia) akimuelimisha Mfanyabiashara wa vipuri vya magari na vilainishi kuhusu kutundika Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) katika sehemu ya wazi wakati alipomtembelea katika duka lake lililopo katika barabara ya Bahi mjini Dodoma wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo.



Afisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Barnabas Masika (kulia) akiwaelimisha Wafanyabiashara wa vipuri vya magari na vilainishi wakati alipowatembelea katika maduka yao yaliyopo katika barabara ya Bahi mjini Dodoma wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo.



Afisa Msimamizi Kodi Mwandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Philipo Eliamini (kushoto) akichukua taarifa kutoka kwa Mfanyabiashara wa vipuri vya magari na vilainishi wakati alipomtembelea katika duka lake lililopo katika barabara ya Bahi mjini Dodoma wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo.




Afisa Msimamizi Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Enny Mwanga (kulia) akimuelimisha Mfanyabiashara wa vipuri vya magari na vilainishi kuhusu umuhimu wa kutoa risiti za kodi za kielektroniki za (EFD) kwa wateja anaowauzia bidhaa wakati alipomtembelea katika duka lake lililopo katika barabara ya Bahi mjini Dodoma wakati wa kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango inayoendelea mkoani hapo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad