HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 30, 2022

JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI (EAC) YARIDHIA DRC KUWA MWANACHAMA KAMILI WA EAC

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wakuu wengine wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa pamoja wameridhia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa mwanachama kamili wa jumuiya hiyo

Tukio hilo la kihistoria lililofanyika kwa njia ya mtandao wakati wa mkutano wa dharura wa 19 uliongozwa na Mwenyekiti, Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta, na kuhudhuriwa na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni pamoja na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame.

Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais wa Burundi, Mhe. Prosper Bazombanza kwa niaba ya Rais Evariste Ndayishimiye huku Waziri wa masuala ya Rais, Dkt. Barnaba Marial Benjamin akimwakilisha Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Rais Samia amesema kulikuwa na biashara kubwa ya kubadilishana bidhaa enzi na enzi baina ya DRC na pwani ya Afrika Mashariki ikiwemo chumvi, pembe za ndovu, na dhahabu. Hivyo kuidhinisha DRC kujiunga na Jumuiya hiyo ni sawa na kurejea kwenye familia.

Mkutano huo umesisitiza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni kwa minajili ya kuimarisha maisha ya watu kupitia ushindani, kuongeza thamani za bidhaa, biashara na uwekezaji kwa uchumi endelevu.

Wakati huo huo, Rais Samia amepokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Malawi nchini Tanzania Mhe. Andrew Posyantos Efron Zumbe katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amekutana na kuzungumza na Balozi wa Uganda aliyemaliza muda wake nchini Tanzania Mhe. Tumusiime Kabonero na kuagana na Balozi wa Tanzania nchini Austria Mhe. Celestine Mushy anayekwenda kuiwakilisha nchi ambapo kumefunguliwa Ubalozi mpya wa Tanzania kwa mara ya kwanza.

 ZuhuraYunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad