Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imepokea msaada wa Madawa na Vifaa Tiba vyenye
thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 za kitanzania kutoka Shirika la Afya
duniani WHO. Vifaa hivyo vitatumika kusaidia kutatua changamoto
mbalimbali za kiafya nchini ikiwemo maradhi ya Uviko 19.
Akipokea
msaada huo Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto
Nassor Ahmed Mazrui amesema msaada huo umekuja muda muafaka kutokana na
Zanzibar kukabiliwa na uhaba wa baadhi ya dawa.
Amesema Shirika
la WHO limekuwa bega kwa bega na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuhakikisha linasaidia kuimarisha afya za wananchi. Ameishukuru WHO
kuendeleza mashirikiano yake kwa Zanzibar hasa katika mripuko wa Janga
la Korona uliotokea nchini.
Waziri Mazrui ameahidi kutoa kila
aina ya ushirikiano ili shirika hilo lifanye kazi zake kwa ufanisi.
Ameahidi msaada huo kutumika ipasavyo kama Shirika hilo lilivyoagiza ili
kutimiza malengo yaliyokusudia.
Akielezea hali halisi ya
Ugonjwa wa Uviko 19 Waziri Mazrui amesema kuanzia mwezi Januari mwaka
huu hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyebainika na maambukizi ya
maradhi hayo.Hata hivyo amesema juhudi mbalimbali zinapaswa kuchukuliwa
ili Zanzibar iendelee kuwa salama dhidi ya maradhi mbali mbali ikiwemo
ya Uviko 19.
Kwa upande wake Mwakilishi mkaazi wa WHO Tanzania
Dkt. Tigest Ketsele ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
ushirikiano mkubwa wanaoupata nchini.
Akielezea kuhusu msaada
walioutoa Dkt. Tigest amesema msaada huo ni mchango kutoka Nchi tofauti
duniani ikiwemo Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya. Awali Mkurugenzi
wa Bohari kuu ya Dawa Zahran Ali alisema Zanzibar kama ilivyo nchi
nyingine zinahitaji Dawa na Vifaa tiba mbalimbali ili kukabiliana na
maradhi.
Aidha ameishukuru WHO kwa kazi yao nzuri wanayoifanya
ikiwemo misaada mbali mbali ya Dawa na mafunzo kwa wataalam wa afya
nchini.
Mapema Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na
Watoto Nassor Ahmed Mazrui alifungua Mkutano wa pamoja kati ya Shirika
la Afya ulimwenguni WHO na Wizara ya Afya kuhusu masuala ya sekta ya
Afya. Alisema utoaji wa huduma zenye ubora zinakwenda sambamba na
kupanga mipango na mahitaji mapema katika sekta ya Afya.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akizungumza wakati wa makabidhiano ya dawa na Vifaa baina ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) huko Bohari kuu ya dawa Maruhubi Zanzibar.Mkurugenzi Bohari kuu Zahran Ali akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya makabidhiano ya msaada wa dawa na vifaa tiba baina ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani WHO,huko Bohari kuu Maruhubi Zanzibar. Picha na Fauzia Mussa-Maelezo Zanzibar
PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment