WALIMU WALEZI WA SKAUTI KITETO WAPATIWA MAFUNZO NA TAKUKURU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 2, 2022

WALIMU WALEZI WA SKAUTI KITETO WAPATIWA MAFUNZO NA TAKUKURU

 Na Mwandishi wetu, Kiteto

WALIMU walezi wa skauti wamepatiwa mafunzo kwenye shule za msingi 112 na sekondari za Wilaya ya Kiteto, yaliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu ameyasema hayo kupitia taarifa yake ya miezi mitatu ya kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Desemba mwaka jana.

Makungu amesema TAKUKURU ilipanga utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kutoa elimu kwa vijana wa skauti ili waweze kuzuia na kupambana na rushwa.

“Ili wawe washiriki wa kuzuia na kupambana na rushwa hatimaye waje kuwa msaada kwa Taifa letu kuanzia ngazi yao binafsi, familia na jamii inayowazunguka,” amesema Makungu.

Amesema mwezi Oktoba mwaka jana mpango huo ulizinduliwa kwa ngazi ya Mkoa kupitia Mkuu wa Mkoa huo Charles Makongoro Nyerere na uzinduzi ukaendelea katika ngazi za Wilaya.

“Aidha wilaya ya Kiteto ushirikiano wa Mhe DC Alhaji Mbaraka Batenga, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri John John Nchimbi, ulisaidia kutoa elimu kwa walimu walezi wa skauti katika shule zote 112 za msingi na sekondari zilizopo Kiteto,” amesema Makungu.

Amesema kila mwalimu aliyewezeshwa kupitia mafunzo hayo atakuwa mwezeshaji kuhusu kupambana na rushwa kwa skauti shuleni kwake.

Amesema mafundisho ya uadilifu, uwajibikaji, uzalendo na utaifa yatasisitizwa ili kuwafanya vijana hao wawe mfano wa uadilifu na msaada wa mapambano dhidi ya rushwa kuanzia kwa kijana mwenyewe, familia yak, jamii inayomzunguka na Taifa kwa ujumla.

“Tunatarajia zoezi la kuwezesha walimu kwenye mkoa wa Manyara, litakamilika katika wilaya zote za mkoa huu ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2022,” amesema Makungu.

Amesema mikakati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu ni kuendelea na mafunzo ya walimu watakaowafundisha vijana na skauti kuhusu elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa na kuendelea na jukumu la kudhibiti vitendo vya rushwa kwa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkoa huo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad