HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 25, 2022

UJENZI WA DARAJA LA JP MAGUFULI WAFIKIA ASILIMIA 40.2


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, amesema ujenzi wa Daraja la JP Magufuli lenye urefu wa kilometa 3.2 unaoendelea jijini Mwanza umefikia asilimia 40.2 kazi zinaendelea usiku na mchana.

Eng. Kasekenya amezungumza hayo jijini Mwanza, wakati alipokuwa akikagua hatua zilizofikiwa katika mradi huo unaotarajiwa kukamilika tarehe 24 Februari, 2024 na kumuagiza Mkandarasi kuleta vifaa vilivyobakia ili kuongeza kasi ya ujenzi.

 “Maendeleo ya ujenzi yanaridhisha na ninakagua mradi mara kwa mara kwasababu uwekezaji wa hapa ni mkubwa sana ukilinganisha na madaraja mengine yanayojengwa nchini pia teknolojia inayotumika hapa ni ya kipekee hivyo ni jukumu letu sisi kulisimamia kwa karibu”, amesema Eng. Kasekenya

Eng. Kasekenya ameeleza kuwa mradi huo ambao unagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa shilingi Bilioni 716 ambapo Serikali inaendelea kumlipa mkandarasi huyo kwa wakati na imedhamiria kukamilisha daraja hili ili wananchi wa jiji hili na mikoa jirani waanze kunufaika na kurahisisha shughuli zao za kiuchumi.

Ameongeza kuwa daraja hilo pindi litakapokamilika litaweza kupunguza muda wa kuvusha watu na magari si zaidi ya dakika nne kulinganisha na hali ya sasa wanapotumia muda mrfu kusubiria kivuko ili kiweze kuwavusha takribani dakika 15.

“Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inafungua fursa nyingi sana kati ya mkoa wa Mwanza na mikoa jirani na baadhi ya nchi tulizopakana nazo ukanda huu”, amesisitiza Eng. Kasekenya.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya, ametoa pole kwa familia ya mfanyakazi aliyepoteza maisha akiwa sehemu ya kazi katika daraja hilo na kusisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama eneo la kazi.

Ametoa rai kwa wasimamizi na wafanyakazi wote wanaoshiriki katika mradi huo kuzingatia taratibu na sheria za usalama mahala pa kazi ili kuweza kujilinda wao wenyewe na kuepusha hatari zozote zinazoweza kujitokeza.

“Hii sehemu si salama kwani imezungukwa na maji kila kona hivyo niwaombe wasimamizi kuzingatia usalama wa wafanyakazi wa eneo hili hasa nyakati za usiku na kuhakikisha wafanyakazi wako vizuri kiafya na kuwepo na taa zenye mwanga mkali ili kuepuesha majanga yanayowezajitokeza”, amefafanua Eng. Kasekenya.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mwanza Eng. Boniface Mkumbo, ameleza kuwa mradi huo unaendelea vizuri na mkandarasi amekwisha ongeza mitambo na wafanyakazi na hadai malipo yoyote kwa kazi zilizokwishafanyika.

Eng. Mkumbo, amesema kuwa mradi umeshatoa ajira 801 na kati ya hao wazawa ni 745 sawa na asilimia 93 na wafanyakazi wa kigeni 56 sawa na asilmia 7.

Ujenzi wa Daraja la JP. Magufuli ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kulifanya Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa Makuu.

Muonekanano wa baadhi ya nguzo za msingi wa Daraja la JP Magufuli zinazoendelea kujengwa ambapo tayari nguzo 348 kati ya 801 zimekwishakamilika katika mradi huo ambao umefika asilimia 40.2, jijini Mwanza.
Kazi za usukuaji nondo katika Daraja la JP Magufuli (km 3.2) linaloendelea kujengwa zikiendelea jijini Mwanza. Ujenzi wa Daraja hilo umefikia asilimia 40.2
Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo - Busisi), Eng. Abdulkarim Majuto (kulia), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, wakati akikagua maendeleo yaliyofikiwa katika daraja hilo, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Eng. Godfrey Kasekenya, akisisitiza jambo kwa Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo - Busisi), Eng. Abdulkarim Majuto (kushoto), wakati alipokuwa akikagua maendeleo yake, jijini Mwanza.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad