RAIS SAMIA AMEENDELEA KUWAJALI WANYONGE KWA KUONGEZA BILIONI 5.5 KWENYE MRADI WA TASAF-Mhe. Ndejembi - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 19, 2022

RAIS SAMIA AMEENDELEA KUWAJALI WANYONGE KWA KUONGEZA BILIONI 5.5 KWENYE MRADI WA TASAF-Mhe. Ndejembi


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na walengwa wa TASAF (Hawapo pichani) Wilayani Nkasi wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya hiyo. Kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Mhe. Aide Kenan na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mhe. Peter Lijuakali.
Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Wilaya ya Nkasi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Mlengwa wa TASAF Bi. Scolastica Tinga wa Kijiji cha Kipundi, akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na TASAF kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi wa namna TASAF wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.


Na Veronica Mwafisi-Nkasi
NAIBUNaibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anawajali wananchi wanyonge ndio maana ameongeza shilingi Bil. 5.5 kwenye Mpango wa TASAF ili kaya zote maskini ambazo ni walengwa wa mpango huo zinufaike.

Mhe. Ndejembi amesema licha ya Mhe. Rais kuelekeza fedha nyingi kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, ameona ni vema kutenga fedha zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa unazisaidia kaya maskini kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kila kitu kuuongezea nguvu ya kiuchumi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili uweze kutekeleza vizuri Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini nchini, hivyo ni jukumu la kila mlengwa kuitumia vizuri ruzuku anayoipata kuboresha maisha yake,” Mhe. Ndejembi amefafanua.

Ili kuboresha zaidi maisha ya walengwa hao, Mhe. Ndejembi amewataka walengwa kuona umuhimu wa kuunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawawezesha kupata sifa kukopeshwa na Halmashauri.

“Ninatamani kuona baada ya kuanzisha vikundi vyenu vya ujasiriamali muende Halmashauri kuomba mkopo wa asilimia kumi (10%) utakaowawezesha kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitaboresha maisha ya familia zenu,” Mhe. Ndejembi amehimiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewaeleza wanufaika hao kuwa, kwa zile Kaya ambazo bado zinasubiri kuingia kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, utaratibu unafanyika na muda si mrefu wataingizwa katika Mpango huo.

Kwa upande wake mlengwa wa TASAF, Bi. Scolastica Tinga wa Kijiji cha Kipundi, amemshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mlengwa huyo ameishukuru pia TASAF kwa kumpatia ruzuku iliyomuwezesha kujenga nyumba bora ya kuishi, kwani kabla ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF hakuwa na nyumba bora ya kuishi.

Naye, mlengwa mwingine wa TASAF, Bi. Leticia Futakamba wa Kijiji cha Kipundi, amesema Mpango wa TASAF umemuwezesha kuwasomesha watoto yatima anaoishi nao, kulima shamba lililomuwezesha kupata chakula cha mwaka mzima ikiwa ni pamoja na kumuwezesha kufyatua tofali 2800 ambazo atazitumia kujengea nyumba yake iliyobomoka.

Mhe. Ndejembi amefanya ziara ya kikazi Wilayani Nkasi, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad