Na Karama Kenyunko Michuzi TV
VIJANA wawili wakazi wa Jijini Dar es Salaam, Said Shewali na Salum Athumani wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo leo Desemba 15,2021 na wakili wa serikali Yusuf Aboud mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Romuli Mbuya imedai kuwa, Novemba 25, 2021 hull katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere washtakiwa hao kwa nyakati tofauti walitenda kosa hilo.
Imedaiwa mshtakiwa Shewali alikutwa akisafirisha kilogramu 3.85 za dawa hizo za kulevya huku Athumani yeye alikutwa akisafirisha kilogramu 3.6 za Heroine.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu.
Kesi hizo zimeahirishwa hadi Desemba 29,2021 zitakapokuja kwa ajili ya kutajwa, kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.
No comments:
Post a Comment