Serikali imewataka wanafunzi kuwa wabunifu ili waweze kuingia katika soko la ajira - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, December 11, 2021

Serikali imewataka wanafunzi kuwa wabunifu ili waweze kuingia katika soko la ajira

Mwenyekiti wa Baraza la  Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ( TEWW) Dkt. Naomi Katunzi, akizungumza wakati wa mahafali ya 57 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika katika viwanja vya TEWW leo Desemba 10,2021 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Naomi Katunzi wa katikati waliokaa,  Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya watu Wazima (TEWW), Dkt. Michael Ng’umbi (wa pili kushoto  waliokaa) wa kwanza kushoto waliokaa ni Mary Watugulu Kaimu Naibu Mkurugenzi Taaluma, Utafiti na Ushauri na kulia ni Majid Mjengwa na Eusella Bhalalusesa wajumbe wa Baraza la usimamizi TEWW wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakufunzi wa TEWW walioshiriki kwenye Mahafali ya 57 ya TEWW yaliyofanyika Jijini Dar es Salaaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Michael Ng’umbi akizungumza na wahitimu (hawapo pichani) wakati wa Mahafali ya 57  ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, yaliyofanyika tarehe leo Desemba 10,2021 jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wahitimu  walioshiriki kwenye Mahafali ya 57 ya TEWW yaliyofanyika Jijini Dar es Salaaam Desemba 10,2021 wakisilikiza hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani)  wakati wa mahafali hayo.

Na Karama Kenyunko Michuzi TV 
MWENYEKITI wa Baraza la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dk Naomi Katunzi, amewataka wahitimu 1,505 kutoka mikoa ya Mwanza, Dear es salaam na Morogoro kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi na kuongeza nguvu katika sekta ya elimu katika Halmashauri mbalimbali. 

Aidha, ameitaka taasisi hiyo kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia taratibu za uendeshaji wa elimu kwa njia ya masafa.
 Akizungumza katika mahafali ya 57  ya taasisi hiyo leo, Desemba 10,2021 Dkt. Katunzi  amesema wahitimu 443 ni wale waliosoma kwa njia ya kawaida na 1,062 ni wale waliohitimu kwa njia ya Ujifunzaji Huria na Masafa kutoka katika Vituo 61 vya mafunzo.

Amesema licha ya changamoto zilizopo watumie uzoefu wao  kuboresha zaidi ufundishaji wa masafa wanapoendesha program  za ngazi ya Stashahada na shahada.

"Muendelee kuhamasisha jamii na wadau na kuzitangaza program zenu ili kuweza kupata wateja wengi zaidi na hatimaye kukabiliana na changamoto mliyoitaja awali ya kutokuwa na fedha za kutosha," amesema Dkt Katunzi.

Ameeleza kuwa atahakikisha anafanyia kazi suala la taasisi hiyo kutopata fedha za maendeleo kutoka serikalini na kuhamasisha mikakati mbalimbali ya kujiongezea kipato ifanyike ili kusaidia kutekeleza malengo waliyojiwekea.

 Naye, Mkurugenzi wa TEWW  Dk Michael Ng’umbi, amesema amewataka wahitimu hao kuendelea kuwa raia wema kwa kuwa mfano wa utendaji kazi ulio bora zaidi katika maeneo yeo ya kazi kwa kufanya kazi kwa weledi na kuepuka uzembe, udanganyifu, rushwa na ufisadi kwani vitendo hivyo havikubaliki.

Pia amewaasa wahitimu hao kujikinga na ugonjwa hatari wa ukimwi pamoja na magonjwa mengine hatarishi ili kusaidia kuilinda nguvukazi ya Taifa.

Dk Ng'umbi amesema TEWW pia imepiga hatua kubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, kwa kuongeza idadi ya wasimamizi na wawezeshaji wa elimu ya watu wazima nchini kutoka 29  hadi kufikia wataalam takribani 12,800 waliohitimu programu mbalimbali za TEWW hadi sasa. 

"Mafanikio katika sekta ya elimu ya watu wazima pamoja na ya sekta mbalimbali nchini katika kipindi cha miaka 60 baada ya Uhuru wa Tanzania Bara yametokana na kazi iliyotukuka iliyofanywa na serikali za awamu zote sita pamoja na wadau mbalimbali wenye nia njema na maendeleo ya nchi yetu," amesema Dk Ng'umbi.

Pia amesema  TEWW imeanza utekelezaji wa mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari unaojulikana kwa jina la SEQUIP ambapo TEWW inatekeleza mradi huo upande wa elimu ya sekondari kwa njia mbadala.

 Amesema kupitia Mradi huo, TEWW itadahili jumla ya wasichana 12,000 katika kipindi cha miaka mitano cha mradi, ambapo kila mwaka TEWW inalenga kudahili wasichana 3,000 waliokatisha masomo ya elimu ya sekondari. 

"Nimatarajio yetu kuwa mradi huu utakwenda kuondoa changamoto kwa wasichana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo kupata ujauzito kurudi tena na kuendelea na masomo ili kutimiza ndoto zao," amesisitiza.

TEWW kama moja ya wadau muhimu katika kujenga uchumi wa Taifa letu, pamoja na kuendeleza kisomo na elimu kwa umma nchini, pia inatekeleza programu ya IPOSA ambayo inalenga kutoa mafunzo ya ujasiriamali, stadi za maisha, ufundi wa awali na stadi za kisomo kwa vijana walio nje ya shule katika mikoa tisa ya Tanzania Bara ambayo ni  Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mbeya, Njombe, Songwe, Tabora na Rukwa. Kati ya vijana 12,000 waliodahiliwa mwaka 2019,  jumla ya vijana 4,067 walihitimu Mafunzo. 

Amesema mradi huu umewajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajiriwa hivyo kujiongezea kipato wao, familia zao na kuchangia pato la taifa na hivyo kuweza kuyafikia na kuyaishi  malengo ya uchumi wa kati nchini. 

Amesisitiza kuwa katika kuendeleza juhudi za kupanua wigo wa fursa za elimu na kuendelea kuongeza idadi ya wahitimu mwaka hadi mwaka, TEWW imeanza kutoa shahada kwa njia ya ujifunzaji huria na masafa mwaka huu 2021/2022. Mafunzo haya ni kwa programmu za  Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi na Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii. Hii ni fursa kwa wahitimu waliomaliza stashahada kuweza kuendelea na shahada popote watakapokuwa. Kwa sasa vituo vya kutolea mafunzo ya ana kwa ana yatakuwa katika Kampasi za Dar es salaam, Mwanza na Morogoro.

Dkt Ng'umbi amesema kuna  changamoto mbalimbali zinazoikabili TEWW ikiwemo, uboreshaji wa miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).  hivyo ili kuimarisha utoaji huo wa elimu,  mikakati thabiti ya uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA inahitajika. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad