MAHAKAMA YA RUFAA YABATILISHA ADHABU YA KIFO YA MFANYABIASHARA J4, KESI KUSIKILIZWA UPYA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 6, 2021

MAHAKAMA YA RUFAA YABATILISHA ADHABU YA KIFO YA MFANYABIASHARA J4, KESI KUSIKILIZWA UPYA

 Na Baltazar Mashaka Mwanza

MAHAKAMA ya Rufaa imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya Mabasi ya J4 Express, Jumanne Mahende au J4 baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu ya Mwanza kwa kosa la mauaji ya kukusudia.

Mahakama hiyo ya Rufaa baada ya kubatilisha adhabu na kutengua hukumu ya Mahakama Kuu Mwanza,imeagiza kesi hiyo jinai namba 131/2017 isikilizwe upya.

J4 alitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ya Ali Abeid na Claude Sikarwanda, hukumu iliyotolewa Machi 13, 2020 na Jaji Mfawidhi wa Makahama Kuu Mwanza, Sam Rumanyika.

Mfanyabiashara na Mkurugenzi huyo wa kampuni ya Mabasi ya J4 Express,alidaiwa kuwaua kwa kuwapiga kwa risasi Ally Abeid Mohamed,mkazi wa Igoma na Claud Sikarwanda, mkazi wa Nyasaka Ilemela, Julai 13, 2015, majira ya saa 4:00 usiku, eneo la Nyakato Boma kwenye ofisi na karakana ya magari ya mfanyabiashara huyo.

Akitoa hukumu hiyo ya kurasa 12,Jaji Rumanyika katika kesi hiyo Jinai namba 131 ya 2017, alisema Mahakama hiyo ilijiridhisha kuwa Jamhuri ilithibitisha mashitaka yao bila kuacha shaka kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi 12.

Mahakama ya Rufaa chini ya jopo la majaji watatu katika uamuzi wake Ijumaa ya wiki iliyopita (Disemba 3,2021) ilieleza kubaini kasoro kadhaa kwenye hukumu hiyo ya Mahakama Kuu Mwanza na hivyo kuitengua na kusitisha adhabu ya kifo dhidi ya mfanyabiashara huyo.

Rufaa hiyo ya jinai namba 204/2020 iliyosikilizwa na Jaji Rehema Mkuye,Jaji Issa Maige na Jaji Kwiliko na kusomwa na Msajili wa Mahakama hiyo Mtelamia,iliekeza kesi hiyo ya mauaji isikilizwe upya kwa Jaji mwingine akisaidiwa na wazee wa baraza.

Majaji hao baada ya kupitia hukumu hiyo waliamua kesi hiyo isikilizwe upya kutokana na dosari za kisheria kwamba Jaji aliyesikiliza shauri hilo aliweka maoni yake bila kuzingatia ushauri wa wazee wa baraza na kwamba waliondolewa haki yao ya kutoa na kueleza maoni yao inavyotakiwa kisheria.

Mahakama hiyo ya Rufaa ilisema iliona mahakama kuu haikuendesha kesi kwa msaada wa wazee wa baraza kwa mujibu wa sheria ambapo athari za tatizo hilo huufanya mwenendo wa kesi na matokeo yake yaani hatia na adhabu vyote kuwa batili.

Kwamba aliweka maoni yake kuhusiana na ushahidi na mahakama hiyo iliona hakuwa anawaagiza bali alitaka kuwashawishi jambo ambalo mahamaka imeona ni kinyume cha sheria.

Majaji hao katika hukumu hiyo walieleza kwa kufanya hivyo kuliathiri mwenendo wa shauri, hivyo mahakama hiyo iliona haina haja ya kuendelea na sababu hizo kwa mujibu wa kifungu 4 (2) cha sheria ya CPA na hivyo kubatilisha hukumu na kutengua adhabu ya kifo dhidi ya Jumanne Mahende au J4.
Kesi hiyo ya mauaji itasikilizwa upya kwa jaji na wazee wengine wa baraza ambapo mtuhumiwa ataendelea kukaa mahabusu muda wote wa shauri hilo.ssss
Jumanne Mahende au J4 ambaye Mahakama ya Rufaa imebatisha hukumu ya kifo dhidi yake na kuagiza kesi hiyo ya mauaji inayomkabili isikilizwe upya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad