WANANCHI WA KIJIJI CHA BOKWA WILAYA YA KILINDI WAFURAHIA UJENZI WA BARABARA YA LAMI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 2, 2021

WANANCHI WA KIJIJI CHA BOKWA WILAYA YA KILINDI WAFURAHIA UJENZI WA BARABARA YA LAMI

 


Wananchi wa Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa, Tarafa ya Kwekivu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wametoa shukrani zao za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupata barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita 5.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kutengeneza barabara ya lami na barabara za changarawe katika Wilaya yao ili kuwezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi.

Mkazi wa Kijiji cha Bokwa Bw. Mohamed Chambo amesema, katika umri wake alioishi hajawahi kuona lami ikiwekwa kwenye wilaya hiyo, lakini sasa ameshuhudia ikiwekwa kwenye kijiji chake, na kusifu Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha kuwatengenezea barabara za vijijini ili ziweze kuwasaidia kwenye shughuli zao za kila siku.

"Mimi nina miaka 83, lakini sijawahi kuona lami kwenye Wilaya hii ya Kilindi, lakini sasa naona barabara ya lami inapita kijijini kwetu hivyo, tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kutuletea lami", amesema Chambo.

Naye, Bi. Habiba Yassin ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Bokwa amesema kuwa pamoja na kujengewa barabara ya lami, pia mradi huo wa barabara umewapa ajira hasa wanawake, kwani walishiriki kwenye ujenzi huo kwa kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuchimba mitaro pamoja na kuokota mawe makubwa ambayo hayatakiwi kuwepo kwenye ujenzi ambayo wananchi waliyachukua na kuponda na kupata kokoto.

"Mradi huu wa barabara pamoja na kwamba umeletwa ili tuwe na barabara nzuri, lakini sisi wakazi wa Kijiji cha Bokwa tumepata neema nyingi ikiwemo kufanya kazi mbalimbali. Sisi kama wanawake tuliweza kuchimba mtaro uliopo pembeni ya barabara, kuokota mawe pamoja na kusaidia mafundi”, amesema Habiba.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Martin Mwashambwa amesema, mradi wa barabara kwa kiwango cha lami wa Bokwa wilayani Kilindi hadi Kata ya Lengatei, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ni wa kilomita tano na unatekelezwa kwa awamu.

Mhandisi Mwashambwa amesema kuwa, awamu ya kwanza ya mradi unajengwa kwa mita 400, ambapo utekelezaji wake unafanywa chini ya Mkandarasi JP Traders Ltd kutoka mkoani Dar es Salaam, na unagharimu sh. milioni 315, ambapo mradi umeanza tarehe 3 Septemba, 2021 na unatarajia kukamilika tarehe 3 Machi, 2022.

"TARURA hii ni mara yetu ya kwanza kuweka lami katika Wilaya ya Kilindi na tutaendelea kuboresha barabara zetu kila tutakapopata fedha kutoka serikalini ili tuendelee kufungua barabara sehemu ambazo hazipitiki kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii”, amesema Mhandisi Martin.

Mhandisi Mwashambwa ameongeza kuwa, TARURA Wilaya ya Kilindi ina mtandao wa barabara wa kilomita 871.59. Kati ya hizo, kilomita 59.72 ni za kiwango cha changarawe, na kilomita 811.8 ni za udongo. Lakini kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kufungua barabara na kufanyia maboresho zile za udongo kuwa za changarawe. Pia Serikali imetoa shilingi milioni 500 ambazo nazo zitafanya kazi ya kutengeneza maeneo korofi na makaravati ili barabara zipitike mwaka mzima.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad