Wananchi 319 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika tamasha la Karibu Dodoma Festival - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 1, 2021

Wananchi 319 wafanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo katika tamasha la Karibu Dodoma Festival

Mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa sekya ya Afya mara baada ya kumalizika kwa tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali park. Tamasha hilo lilienda sambamba na zoezi la upimaji wa afya.

Mhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Illuminata Marimbo akiwaeleza wananchi gharama mbalimbali za matibabu yanayotolewa na Taasisi hiyo wakati wa tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali park. Wananchi hao walifika katika banda la taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa na wataalamu wa JKCI.
Afisa muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Lilian Peter akimsikiliza mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinazotolewa na wataalamu wa JKCI katika tamasha la Karibu Dodoma festival lililofanyika katika viwaja vya Chinangali park jijini Dodoma wakati akimpima kiwango cha sukari mwilini.
WANANCHI 319 walitembelea katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwenye tamasha la karibu Dodoma Festival lililofanyika katika viwanja vya Chinangali Park kuanzia tarehe 25-29/10/2021.

Watu wote waliotembelea katika banda la Taasisi hiyo walifanyiwa vipimo vya urefu na uzito, kiwango cha sukari mwilini, uwiano kati ya urefu na uzito, shinikizo la damu (BP) na walipata elimu ya magonjwa ya moyo ikiwemo lishe bora kwa afya ya moyo.

Waliofanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography- ECHO) na mfumo wa umeme wa moyo (Electrocardiography - ECG) walikuwa 230. Kati ya hawa 230 waliofanyiwa vipimo hivi 159 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na hivyo kupewa dawa za kwenda kutumia. Dawa hizi zilitolewa bila malipo yoyote yale na kampuni ya uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu ya Sun Pharmaceutical Industries Ltd.

Wagonjwa 26 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na hivyo kupewa rufaa za kwenda kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi pamoja na kutibiwa katika hospital ya mkoa ya Dodoma, hospitali ya kanda ya Benjamini Mkapa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Matatizo waliyokutwa nayo wagonjwa waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni kuziba kwa mishipa ya damu ya moyo hawa walikuwa 5, umeme wa moyo kupita katika njia ya ziada tofauti na ile ya kawaida (Wolff – Parkinson - White syndrome) alikuwa mmoja, mshipa mkubwa wa damu wa moyo umetanuka na valvu ya Aorta inarudisha damu nyuma alikuwa mmoja, mapigo ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida zaidi ya mapigo 100 kwa dakika moja na inafika wakati anazimia alikuwa mmoja.

Mgonjwa mmoja moyo wake ulikuwa umetanuka na ni mjamzito kitu ambacho kinahatarisha maisha ya mama na mtoto aliyepo tumboni na mgonjwa mmoja alikuwa na shida ya valvu ya moyo (Rheumatic Heart disease) ugonjwa huu unasababishwa na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo.

Asilimia kubwa ya wagonjwa tuliowagundua katika upimaji huu wakiwemo wagonjwa wote 26 tuiowapa rufaa hawakuwa wanafahamu kuwa na matatizo ya moyo.

Taasisi inaendelea kutoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara pia kujitokeza kwa wingi kupima magonjwa ya moyo wakati tunapotoa huduma mbalimbali za upimaji kwa wananchi. Kwani upimaji huwa unafanyika bila malipo yeyote yale na kama kutakuwa na malipo ni kwa ajili ya vipimo ambapo mwananchi anachangia kiasi kidogo cha fedha na kuna ambao hawachangii kabisa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad