WAJIKI YAENDELEA NA KAMPENI YA 'SAFIRI SALAMA BILA RUSHWA YA NGONO' - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 8, 2021

WAJIKI YAENDELEA NA KAMPENI YA 'SAFIRI SALAMA BILA RUSHWA YA NGONO'


Afisa mchunguzi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Temeke Ester Mkokota akitoa mada kwa wadau wakati wa mafunzo maalumu kwa madereva wa daladala na bodaboda kupitia kampeni ya 'Safiri Salama bila Rushwa ya Ngono.'' yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
* Yajipanga kwenda Temeke kutoa elimu hiyo nyumba kwa nyumba, vituo vya basi na bodabodaSHIRIKA la Wanawake katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI,) Iimeendelea na Kampeni ya kupiga vita rushwa ya ngono ya '' Safiri Salama bila Rushwa ya Ngono,'' kwa wanawake na wanafunzi kampeni iliyofadhiliwa na wa Women Fund Tanzania (WFT,) na kuwahusisha madereva wa daladala na bodaboda kupitia umoja wao kwa malengo ya kuungana na Serikali katika kuhakikisha jamii inafahamu namna ya kuripoti na kuwaumbua wanaofanya vitendo hivyo ili kujenga jamii ya wanawake wanaosema hapana pindi wanapokutana na vitendo hivyo wanapotafuta fursa mbalimbali ikiwemo ajira na mkopo na huduma mbalimbali ikiwemo usafiri waa Umma.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mwendelezo wa kampeni hiyo Mkurugenzi wa taasisi hiyo Janeth Mawinza amesema kuwa mafunzo hayo ya uelimishaji rika ni mwendelezo wa kampeni ya kupiga vita rushwa ya ngono kwa wanafunzi na wanawake kwa kuwezesha makundi hayo ya madereva wa daladala na bodaboda kuwa mabalozi kwa jamii kwa kuifanya ipaze sauti dhidi ya vitendo hivyo.


'' Women Fund Tanzania (WFT,) imeendelea kutuunga mkono katika kuhakikisha tunaisaidia jamii kuvunja ukimya dhidi ya vitendo vya rushwa ya ngono na hiyo ni pamoja na wanafunzi wa kike kuwataja na kuwaaibisha wote wanaotaka kutenda na kutenda vitendo hivyo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, tunafanya kampeni hizi kwa kushirikiana kwa ukaribu na Serikali na wadau mbalimbali wakiwemo TAKUKURU na kuwashirikisha madereva wa bodaboda na daladala ambao wanatajwa sana katika hili...kupitia mafunzo haya madereva hawa pia watatoa elimu kwa wengine kupitia mafunzo waliyoyapata na stika za kupinga ukatili huo zitabandikwa katika vyombo vyao vya usafiri ili kuelimisha zaidi.'' Amesema.


Amesema ili kufanikisha kampeni hiyo kwa kushinda vita dhidi ya rushwa ya ngono kwa wanawake na wanafunzi wa kike lazima jamii ishiriki kwa kuhakikisha viashiria vya vitendo hivyo vinatajwa pamoja na wahusika wake ili kujenga jamii imara ya wanawake na wasichana wanaosema hapana dhidi ya vitendo hivyo.


Bi. Mawinza amesema kampeni hiyo imedumu kwa miaka mitatu chini ya ufadhili wa mfuko wa Women Fund Tanzania na wamefanikiwa kuwafikia walengwa wengi zaidi katika Mkoa wa Dar es Salaam na baada ya mafunzo hayo ya siku moja kesho watatembelea Wilaya ya Temeke na kupiga kambi ya kutoa elimu nyumba kwa nyumba pamoja na vituo vya daladala na bodaboda ili kuihamasisha jamii kupinga vitendo hivyo pamoja na kugawa vifaa kwa makundi ya madereva;


''Wanawake na wanafunzi wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa sana na rushwa ya ngono hasa wanapotoka majumbani na kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo elimu na ajira ambapo wanakutana na wenye mamlaka katikati na kuwataka kutoa rushwa ya ngono ili waweze kupata huduma wanayohitaji....Tumeona mfano wa mdau mmoja hapa kuhusu madereva bodaboda wanapomtamani mtu hutumia nyenzo waliyonayo kuwasafirisha kwa malengo ya kuwalaghai na kupata rushwa ya ngono, hali hii hutokea pia shuleni, majumbani ambapo watu wanaotakiwa kuwapa huduma ndio huwaomba rushwa ya ngono....Tutakwenda Temeke na kutoa elimu zaidi na tunaamini tutafanikisha hili'' Amesema.


Pia amesema kampeni hiyo inakwenda sambamba na kuelimisha jamii kujikinga dhidi ya virusi vya UVIKO-19 kwa kuchukua tahadhari ikiwemo kupata chanjo inayotolewa kote nchini dhidi ya virusi hivyo.


Kwa upande wake Afisa Mchunguzi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Temeke Ester Mkokota amesema, rushwa ya ngono kwa wanawake na wanafunzi limekuwa janga linalokatiza ndoto za wengi na kuipongeza WAJIKI pamoja na WFT kwa kuongeza nguvu zaidi kwa kushirikiana na Serikali katika kupinga vitendo hivyo.


Amesema, TAKUKURU ipo tayari muda wote na wanashirikiana na jamii na wadau katika kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa elimu na kuchukua hatua kwa wenye mamlaka na watoa huduma watakaobainika wanatoa huduma au fursa kwa kuweka mbele rushwa ya ngono kwa wanawake na wanafunzi.


Vilevile Afisa Maendeleo kutoka Wilaya ya Temeke Bi. Regina Chumi amewataka washiriki hao kuishi na kuwa mfano bora kwa jamii kupitia mafunzo hayo ili kujenga jamii imara yenye kusema hapana pindi wanapokutana na vitendo hivyo pamoja na kujenga kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye.


Mradi huo umehusisha makundi maalum ya madereva wa daladala kupitia umoja wao wa UWAMAWIKI (Umoja wa Madereva wa Wilaya ya Kinondoni) na vikundi vyao ikiwemo; Umoja wa Madereva wa Daladala Makumbusho, Tegeta, na Bunju (UWAMATEBU,) Umoja wa Madereva wa Daladala Makumbusho- Posta (UWAMAPO,) Umoja wa Madereva wa Daladala Mbagala (UMDM,) pamoja na Umoja wa Madereva na Pikipiki na Bajaji Gongolamboto.


Mkurugenzi wa Taasisi ya WAJIKI Janeth Mawinza akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo na kueleza kuwa wataendelea kuwafikia wadau wengi zaidi ili kuweza kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono, leo jijini Dar ees Salaam.
Afisa mchunguzi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Temeke Ester Mkokota akitoa mada kwa wadau wakati wa mafunzo maalumu kwa madereva wa daladala na bodaboda kupitia kampeni ya 'Safiri Salama bila Rushwa ya Ngono.'' yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva daladala nchini Abdallah Lubala akizungumza wakati wa mafunzo hayo ambapo ameishukuru WAJIKI kwa kuendelea kuwafikia wadau wengi zaid hasa madereva wa daladala na bodaboda na kuahidi kuwa wataendeelea kutoa elimu hiyo kupitia umoja wao ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad