HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 1, 2021

TANZANIA KUNUNUA MAFUTA MOJA KWA MOJA KUTOKA MITAMBONI

 



SERIKALI ya Tanzania kununua mafuta moja kwa moja kutoka kwenye mitambo ya kusafisha mafuta (refineries) ya nchi rafiki badala ya kuachia watu wa katikati (intermediaries) kununua kwa nchi na kutuuzia kwa bei kubwa.

Hayo yalielezwa katika taarifa iliyotolewa na  Waziri wa Nishati, January Makamba (Mb.) jana Oktoba 31,2021  imeeleza kuwa bei ya mafuta ghafi duniani imeendelea kupanda kwa kasi na kwa kiwango kikubwa, kutoka dola 50 kwa pipa mwezi wa Januari mwaka huu hadi dola 86 kwa pipa jana tarehe 31 Oktoba 2021.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hiyo inapelekea bei kupanda kwenye vituo vya kuuzia mafuta na mitaani hapa nchini.

Wizara ya Nishati imeanza kutekeleza maelekezo hayo na pia kuratibu hatua mbalimbali za Wizara na taasisi nyingine za umma na kufanikiwa kupunguza ongezeko kubwa la bei ya mafuta kwa mwezi wa Oktoba.

"Kutokana na hilo, katika duru la kwanza, kuanzia tarehe 22 hadi 29 Oktoba 2021 nilifanya ziara katika nchi tatu – Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Algeria – ambazo zinazalisha mafuta kwa wingi na kuuza kote duniani. Katika nchi hizo, nilikutana na Mawaziri wenzangu wa Nishati, na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na makampuni 2 ya mafuta ya Serikali za nchi hizo. Vilevile, nilibeba ujumbe maalum wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa viongozi wa nchi hizo."

Katika ziara hiyo, niliongozana na Ndugu Michael Mjinja, Kamishna wa Petroli na Gesi katika Wizara ya Nishati na Ndugu James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC. Pia, mabalozi wetu katika nchi hizo walishiriki katika vikao na mazungumzo niliyoyafanya.

Katika kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba bei za mafuta haziumizi wananchi, na shughuli za uchumi haziathiriki, Wizara ya Nishati ilichunguza na kubaini uwezekano wa unafuu wa bei za mafuta.

Madhumuni ya ziara hiyo yalikuwa ni kama ifuatavyo:-
1. Kuzungumza na nchi rafiki zinazozalisha mafuta ili kuangalia uwezekano wa Serikali, kupitia Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC), kununua mafuta moja kwa moja kwenye mitambo yao ya kuzalisha mafuta (refineries) na hivyo kupunguza gharama zinazowekwa na wanunuzi wa kati.

2. Kubadilishana uzoefu na nchi hizi rafiki kuhusu uendeshaji wa sekta ya mafuta na gesi.

3. Kuimarisha mahusiano yaliyopo na kujenga ushirikiano mpya katika eneo la mafuta ili nchi yetu ipate jawabu la kudumu la kujihakikishia upatikanaji wa uhakika wa mafuta na kwa bei isiyopanda ghafla na kwa kiwango kikubwa.

Katika nchi zote hizo tatu, nilifanikiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri wenzangu wa Nishati, viongozi wengine waandamizi na wakuu wa mashirika ya mafuta ya taifa ya nchi hizo.

Kutokana na heshima ya nchi yetu na Rais wetu, na urafiki wa nchi yetu na nchi hizi, nilipokelewa vizuri na viongozi wote katika nchi zote hizi na walipokea na kukubali hoja na haja ya mashirikiano katika sekta hii ya mafuta. Kwa kifupi, yale yote ambayo nchi yetu iliyapendekeza kwenye nchi hizi yamekubalika.

Baadhi ya mafanikio ya ziara hiyo ni kama ifuatavyo:
1. Serikali yetu imekubaliana na Serikali za nchi hizo na makampuni yao ya Taifa ya mafuta kushirikiana katika masuala ya mafuta na gesi. Katika miezi ijayo, baada ya taratibu za kiserikali na kisheria kukamilika, makubaliano hayo yenye maslahi kwa nchi yetu yatatangazwa.

2. Kwa mara ya kwanza, ile azma ya miaka mingi ya Serikali, kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji sasa imetimia. Hata kabla ya mwisho wa safari yetu, mnamo tarehe 28 Oktoba 2021, tuliiwezesha TPDC kushiriki zabuni ya kiushindani na makampuni mengine ya kimataifa ambayo kila mwezi hushiriki zabuni ya kuleta mafuta nchini. TPDC imefanikiwa kushinda sehemu kubwa ya zabuni hiyo kwa kutoa bei ndogo zaidi ya kuagiza mafuta ya dizeli nchini kwa mwezi wa Disemba mwaka huu. Hali hii itapunguza makali ya bei ya mafuta ya dizeli kwa mwezi Disemba. Kudhihirisha kwamba hatua hii ina manufaa, kwa mfano, mwezi Agosti 2021, wakati bei ya mafuta ghafi duniani ilikuwa dola 73 kwa pipa, kampuni iliyoshinda zabuni ya kuleta mafuta ya dizeli nchini ilituuzia kwa dola 30 kwa tani za ujazo (premium). Safari hii, pamoja na bei ya mafuta ghafi duniani kupanda na kufikia dola 86 kwa pipa, TPDC italeta dizeli nchini mwezi Disemba kwa wastani wa dola 20 kwa tani za ujazo.

3. Tumefanikiwa kushawishi nchi rafiki tulizotembelea kushirikiana na nchi yetu kujenga kituo kikubwa cha upokeaji na uhifadhi mkubwa wa mafuta (fuel terminal) kwa ajili ya soko la ndani ya nchi yetu lakini kwa mahitaji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati na nyingine za mbali pale itakapohitajika. Kituo hiki kitatuhakikishia kuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ndani ya nchi wakati wote. Kwa sasa, iwapo kutatokea dharura huko duniani na tukashindwa kuagiza mafuta, kiasi cha mafuta yaliyopo nchini yanatutosheleza kwa wastani wa siku 15 tu. Mazungumzo kuhusu taratibu za kuanzisha kituo hiki yataanza mwezi wa Novemba.

4. Baada ya wiki mbili kuanzia sasa, kutakuwa na ziara za viongozi na watalaam kutoka katika nchi tulizotembelea kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utekelezaji wa makubaliano yetu kwenye maeneo tuliyokubaliana kushirikiana. Wizara ya Nishati itaendelea kuratibu na kufuatilia ili kuhakikisha

kwamba mafanikio yaliyopatikana kwenye ziara hii yanadumu na makubaliano na nchi hizi rafiki yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake.

Wakati huo huo, katika kuendelea kurekebisha sekta ndogo ya mafuta, Serikali itatekeleza yafuatayo:-

1. Kama hatua ya muda mfupi, kuiimarisha TPDC kwa kuiruhusu haraka kuajiri watumishi weledi na wajuzi wa biashara ya mafuta ili iendelee kununua mafuta kwa niaba ya Serikali kwa ufanisi zaidi.

2. Kama hatua ya muda wa kati, lakini yenye jawabu la muda mrefu, Serikali itaanzisha Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve) ili kuwa na akiba kubwa ya mafuta wakati wote kwa ajili ya dharura na pale bei duniani itakapopanda kwa kiwango kikubwa.

3. Kupitia mfumo wa uagizaji wa mafuta wa pamoja (Bulk Procurement System) ili kubaini mapungufu na kuboresha kwa maslahi mapana ya Taifa.

4. Kufanya tathmini ya utendaji na watumishi wa taasisi zote za Serikali zinazohusika na biashara ya mafuta ikiwemo TPDC, EWURA na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja (PBPA) ili kuhakikisha kwamba taasisi hizi na watumishi wake wote wanatimiza wajibu wao kwa weledi na uadilifu na kwa maslahi ya nchi.

5. Kuendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais ikiwemo kuendelea kupitia tozo na kodi mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa bei ya mafuta nchini.

6. Kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa biashara ya mafuta nchini, ikiwemo TAOMAC na TAPSOA, na kuweka mazingira mazuri ya biashara ya mafuta nchini kwa sekta binafsi kuendelea kushiriki ili kuwe na ushindani wa haki na wa uwazi kwa manufaa ya watumiaji mafuta na nchi kwa jumla. Serikali itaongeza ufuatiliaji wa karibu zaidi kwenye sekta ya mafuta kwa kutumia vyombo na mamlaka mbalimbali ili kubaini na kudhibiti hujuma na udanganyifu katika biashara ya mafuta na kuweka adhabu kali zaidi, ikiwemo kunyang’anywa leseni, pale itakapobainika hivyo.

7. Kurekebisha miundombinu ya upokeaji na uhifadhi wa mafuta nchini, hasa kwenye bandari zetu ili kuhakikisha kwamba kuna ufanisi zaidi.

8. Kuendelea kuyafanyia kazi na kutekeleza mapendekezo ya tume iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu biashara ya mafuta nchini.

Bei ya mafuta nchini kwa kiasi kikubwa inachangiwa na bei za mafuta duniani, ambazo Serikali ina nafasi ndogo kwenye kuzidhibiti. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba yale yaliyo ndani ya uwezo wa Serikali katika kudhibiti bei ya mafuta tunayafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad