Na Seif Mangwangi, Manyara
WAFANYABIASHARA
wanaosafirisha mazao kupitia Mkoa wa Manyara wamelalamikia mamlaka ya
mapato TRA Mkoa wa Manyara kwa kile walichodai kuzuia magari yao na
kuwasababishia hasara kubwa.
Wakizungumza
na waandishi wa habari leo Mkoani humo, wasafirishaji hao wa mazao
kutoka katika mikoa ya Singida, Manyara, Shinyanga, Tabora na Mwanza
wamesema TRA Mkoa wa Manyara wameanzisha utaratibu mpya wa kuwataka
kuonyesha stakabadhi ya ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wadogo
jambo ambalo halipo kisheria na halijawahi kufanyika nchini.
"Tangu
juzi TRA mkoa wa Manyara wameanzisha utaratibu mpya wa kututaka
kuonyesha stakabadhi ya ununuzi wa mazao kutoka kwa mkulima mdogo,
tunajiuliza huyu mkulima yeye anatoa wapi mashine ya TRA hadi aweze
kutoa risiti,"amehoji mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la
Salum Mabewa.
Amesema
kuwa licha ya wao kuonyesha stakabadhi za ushuru waliolipa Halmashauri
kama sheria inavyotaka pamoja na nyaraka mbalimbali za gari ikiwa ni
pamoja na stakabadhi za malipo ya mizani bado magari yao yamezuiwa
kuondoka mpaka wakabidhi risiti za ununuzi wa mazao.
Kutokana
na sakata hilo ambalo limesababisha usumbufu mkubwa kwa wafanyabiashara
hao, wafanyabiashara hao wamemuomba Waziri wa fedha kuingilia kati
kunusuru hali hiyo kwa kuwa wameendelea kupata hasara kubwa kutokana na
magari yao kuzuiwa na bidhaa kuchelewa sokoni.
"
Tunamuomba Waziri wa fedha Dk.Mwigulu Nchemba kuingilia kati suala hili
kutokana na hasara kubwa tunayoendelea kuipata kwa magari yetu kuzuiwa
hapa Manyara...sisi tunajaribu kufuata sheria za nchi lakini kila siku
tunaletewa vikwazo, je, hivi ndio Mh Rais wetu aliagiza sisi
wafanyabiashara tufanyiwe?"Alihoji a Mabewa.
Hata
hivyo Meneja wa TRA Mkoa wa Manyara, Nicco Massawe amesema ofisi yake
haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wasafirishaji hao wa mazao na
kuwataka wafike ofisini.
Massawe
amesema tatizo la ulipaji wa kodi ni kubwa sana kwa wafanyabiashara
lakini pia kuna matapeli wengi wamekuwa wakitumia jina la TRA kunyanyasa
wafanyabiashara hivyo amewataka waliokutwa na tatizo hilo kufika
ofisini ili kueleza tatizo lako na kama kuna maafisa wa mamlaka hiyo
waliokiuka utaratibu waweze kuwajibishwa.
"
Naomba uwaeleze hao walikutwa na tatizo hili wafike ofisi yoyote ya TRA
walipo wataelewa malalamiko yao na sisi tutajulishwa, kama ni suala la
elimu basi watapatiwa elimu lakini kama kuna afisa aliyekiuka taratibu
atawajibishwa kisheria,"amesema.
No comments:
Post a Comment