HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 13, 2021

TPSF, WIZARA YA MALIASILI NA UTALII WAJADILIANA MATUMIZI YA FEDHA ZA IMF

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi (kulia) pamoja Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF) Angelina Ngalula wakiwasikiliza viongozi wa wadau wa utalii wakitoa maoni ya namna ya kuboresha sekta ya utalii nchini. WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi wa jinsi itakavyozitumia shilingi Bil. 90.2 ilizopewa kutoka kwenye fungu la fedha za mapambano ya UVIKO 19 ya Shilingi trilion 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuwa sehemu kubwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya kupimia ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya Hifadhi.


Aidha, Wizara hiyo imesema fedha hiyo itatumika pia kwa ajili ya kugharamia kutoa mafunzo kwa wadau wa utalii wakiwemo madereva wa magari ya watalii, waongoza watalii, wabeba mizigo pamoja na wahudumu wa hoteli za kitalii,

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro leo Jijini Arusha wakati wa mkutano wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Sekta binafsi ( TPSF) uliolenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili sekta ya utalii nchini hususani katika kipindi cha UVIKO 19

Katika mkutano huo wadau mbalimbali wa Utalii kwa upande wa Sekta Binafsi kimeongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF) Angelina Ngalula ambapo wameshiriki katika mkutano huo wakiwemo Chama cha Waongoza Watalii (TATO), Baraza la Biashara la Taifa, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Chama cha Waongoza Watalii, Chama cha wadau wa Utalii wa Utamaduni (TACTO) pamoja na Chama cha Mahotelia Tanzania (HAT) na upande wa serikali kikao hicho kimeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro

Waziri Dkt.Ndumbaro amesema Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili ziweze kuinyanyua sekta ya utalii nchini kufuatia janga la UVIKO 19 ambalo limeiacha sekta ya utalii katika hali tete huku watalii wakisitisha safari kuja nchini kwa ajili ya ugonjwa huo

Amefafanua kuwa vifaa vitakavyonunuliwa kwa ajili ya vifaa vya kupimia UVIKO 19 vitasambazwa maeneo yote ya vivutio vya utalii ili kuwasaidia watalii pindi watakapopimwa wapewe majibu yao huko huko tofauti na ilivyo sasa

" Tumedhamiria kuondoa usumbufu ili watalii watakapokuja nchini wasiweze kupata usumbufu kwa kuhakikisha kila hifadhi inaweza kutoa huduma hizo kwa haraka ili kuwafanya watalii wasikae kusubiri matokeo kwa muda mrefu " alisisitiza Dkt.Ndumbaro

Akizungumzia kuhusiana na miundombinu, Dkt.Ndumbaro amesema ujio wa fedha hizo zitasaidia kufungua Hifadhi kama vile Hifadhi ya Taifa ya Nyerere imekuwa na barabara nyingi lakini barabara hizo zimekuwa hazipitiki hivyo fedha hizo zitaboresha barabara ili ziweze kupitika mwaka mzima

Mbali na hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema barabara zitaboreshwa huku barabara nyingine zikifunguliwa katika maeneo ya Hifadhi ambazo hazina miundombinu hiyo ili maeneo hayo yaweze kufikika

" Barabara ikiwa nzuri na wewe una hoteli yako ipo ndani sana Watalii watakuja kulala katika hoteli yako kwa sababu kuna barabara nzuri, hivyo hela hii inakwenda kufanya kazi hiyo" amesema Dkt.Ndumbaro

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi ( TPSF) Angelina Ngalula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kuisaidia sekta ya Utalii nchini ''Tunaomba salamu zifike kwa Mhe. Rais kwa juhudi za kuendeleza utalii kwa kututafutia fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF)

" Tumemuona anavyoipambania sekta ya utalii kupitia kipindi chake maarufu alichokiasisi cha Royal Tour ambacho kimeongeza ujasiri kwa Wawekezaji wa sekta ya utalii nchini, tunampongeza sana Rais wetu" alisema Mwenyekiti wa TPSF, Ngalula

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula amewataka wadau wa utalii nchini kuungana kuwa kitu kimoja ili wanapotaka kuweza kuwasilisha agenda zao Serikalini ziweze kukubaliwa na kufanyiwa kazi.

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara, Dkt.Godwill Wanga aliiomba Wizara kupitia fedha zilizotolewa na IMF za kupambana na UVIKO 19 ili.ziweze kusaidia kuboresha miundombinu zikiwemo barabara pamoja na viwanja vya ndege ili kuwavutia watalii wanapotembelea vivutio vya utalii waweze kusafiri kiurahisi.

Aidha, Dkt. Wanga aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia fedha hizo kusaidia kutoa mafunzo kwa wadau wa utalii ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa watalii nchini ombi ambalo limekubaliwa na litaanza kufanyiwa kazi.
 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Wadau wa utalii mara baada ya mkutano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPS) uliolenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini Kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF) Angelina Ngalula na kulia Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi.
Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza leo Jijini Arusha kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania( TPSF) ameihakikishia Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kushirikiana na katika kutatu changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafrishaji Watalii Tanzania (TATO) Willy Chambulo akizungumza wakati wa mkutano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPS) uliolenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini ambapo amempongeza Waziri Ndumbaro kwa kazi nzuri anayoifanya katika Wizara hiyo.
Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Utalii nchini wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa mkutano kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPS) uliolenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini ambapo amesema fedha iliyotolewa na Shirika la Fedha Duniani itasaidia kunyanyua sekta ya utalii nchini kwa kuimarisha miundombinu
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF) Angelina Ngalula akizungumza leo Jijini Arusha kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania( TPSF) ameihakikishia Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kushirikiana na katika kutatu changamoto zinazoikabili sekta ya utalii nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza leo Jijini Arusha kwenye mkutano baina ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania( TPSF) uliolenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili sekta ya utalii nchini hususani katika kipindi cha UVIKO 19 ambapo akifafanua itakavyozitumia fedha ya kiasi cha shilingi Bil. 90.2 ilizopewa kutoka kwenye fungu la fedha za mapambano ya UVIKO 19 ya Shilingi trilion 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuwa sehemu kubwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya kupimia ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya Hifadhi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad