HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 1, 2021

MABAHARIA WAPEWE HESHIMA INAYOSTAHILI- PROFESA MBARAWA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), akifurahia jambo na wataalam wa masuala ya bahari wakati wa kilele cha maadhimisho yao yaliyofanyika kitaifa Chakechake Pemba.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (katikati), mstari wa mbele katika picha ya pamoja na wadau wa bahari mara baada ya kufunga kongamano la maadhimisho ya siku ya bahari yaliyofanyika kitaifa Chakechake Pemba.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa (kulia), akifafanua jambo kwa wadau wa bahari wakati wa kilele cha maadhimisho yao yaliyofanyika kitaifa Chakechake Pemba (kushoto), ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Bw, Mattar Zahor Masoud.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Bw, Mattar Zahor Masoud akitoa nasaha zake kwa wadau wa bahari wakati wa kilele cha maadhimisho yao yaliyofanyika kitaifa Chakechake Pemba.
Baadhi ya washiriki wa kongamano la maadhimisho ya siku ya bahari duniani wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof, Makame Mbarawa hayupo pichani wakati wa kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa Chakechake Pemba.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa tasnia ya mabaharia nchini kuthaminiwa na kupewa kipaumbele ili kuwezesha juhudi za Serikali kuhusu uchumi wa bluu kufanikiwa kwa wakati.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya bahari duniani ambayo kitaifa yamefanyika Chakechake Pemba Prof, Mbarawa amesema mafanikio yote ya uchumi wa bluu yatatokana na thamani itakayowekwa kwa mabaharia na wadau wengine wa bahari.

“Asilimia tisini ya biashara za kimataifa hutumia bahari, hivyo ni wajibu wa kila taasisi inayohusika na masuala ya mabaharia kuwathamini na kutatua changamoto zinazowakabili ili kufikia malengo ya nchi na dunia kwa ujumla”, amesema Prof. Mbarawa.

Amewataka mabaharia nchini kuendelea kufanyakazi kwa bidii, nidhamu na uadilifu ili kuliletea taifa heshima na kutoa fursa nyingi za ajira kwa mabaharia wa Tanzania.

Waziri Prof. Mbarawa amesema Serikali itaendelea kujenga bandari za kisasa katika mwambao wa bahari ya hindi na maziwa makuu na kuongeza idadi ya meli za kisasa katika mkakati wa kuimarisha huduma za usafiri na uchukuzi majini.

Ametoa wito kwa mabaharia wanawake wanaohitimu Chuo cha Mabaharia cha Dar es Salaam (DMI), kupewa kipaumbele katika kazi ili kuondoa dhana kuwa kazi ya ubaharia ni ya wanaume pekee.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Capt. Musa Mandia ameishukuru Serikali kwa kuamua kuwekeza katika uchumi wa bluu na kusisitiza kuwa mabaharia wakipewa heshima na mahitaji yao yakipatiawa ufumbuzi kwa wakati ni wazi uchumi wa bluu utafanikiwa na kutoa fursa nyingi za maendeleo endelevu nchini.

Siku ya bahari duniani huadhimishwa Alhamis ya mwisho wa mwezi Septemba kila mwaka na ilianza kuadhimishwa miaka 43, iliyopita lengo likuwa kutoa elimu kuhusu umuhimu na usalama wa vyombo vinavyosafiri baharini ambapo mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “mabaharia ni kiini cha maendeleo ya usafirishaji wa baharini siku zijazo”.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad