Na Munir Shemweta, DODOMA
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameagiza wananchi
1,672 waliovamia maeneo na kuyaendeleza katika mtaa wa Mbuyuni kata ya
Kizota mkoani Dodoma kupimiwa na kumilikishwa kulingana na jinsi
walivyoendeleza kuonya tabia ya baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo.
Aidha,
ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Dodoma kuwachukulia hatua
za kisheria watu 51 waliobainika kuhusika katika uuzaji maeneo kwa
wananchi huku wakijua hawana umiliki wala mamlaka ya kufanya hivyo kwa
mujibu wa sheria.
Akizungumza na wananchi wa mtaa wa Mbuyuni leo
tarehe 16 Agosti 2021 Lukuvi alisema, uamuzi huo wa kuwabakisha
wananchi waliovamia unafuatia ripoti aliyopewa na timu aliyoiunda
kuchunguza mgogoro huo uliodumu kwa takriban miaka minne.
"Ninaagiza wananchi 1,672 waliovamia na kufanya maendelezo wapimiwe na
kumilikishwa kulingana na ukubwa wa eneo la kila mmoja na yale maeneo ya
wazi yaliyopimwa basi wapewe viwanja wananchi wengine 671’’ alisema
Lukuvi.
‘’Maeneo mengi yanamilikiwa kwa hati na mtu anayejenga
eneo la mtu ni mvamizi na wengi hapa mtaa wa Mbuyuni mna sifa ya uvamizi
na hata kama mtu hajaendeleza muda mrefu siyo sifa ya uvamizi’’ alisema
Waziri wa Ardhi.
Timu iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo ilipewa
maelekezo ya kupokea na kusikiliza changamoto zote katika mtaa wa
Mbuyuni, kubainisha aina ya vyanzo vya migogoro pamoja na kutambua
uhalali wa nyaraka za umiliki.
Pia Tume hiyo ilikuwa na kazi ya
kuhakiki hali ya maenedelezo yaliyofanyika, kubainisha majina na jinai
iliyofanyika na mwisho kutoa mapendekezo kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, wananchi wote
watakaomilikishwa maeneo waliyoyaendeleza watatakiwa kulipa gharama za
urasimishaji na wengine kulipa gharama kidogo za kufidia maeneo
waliyovamia kwa lengo la kufidia waliochukuliwa maeneo yao kupata maeneo
mengine.
Kuhusu maeneo ya viwanda, Waziri Lukuvi alitaka maeneo
hayo kubaki kama yalivyopangwa na kuagiza wamiliki wake kuomba ujenzi
wa viwanda kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa jiji la Dodoma ndani ya siku
tisini na wasipofanya hivyo watanyang’anywa maeneo hayo kwa mujibu wa
sheria.
Aidha, Waziri Lukuvi aliwaaasa wananchi wa Dodoma
kuhakikisha hawafanyi ujenzi wowote bila kupata kibali sambamba na
kununua maeneo bila kuuliza mamlaka husika kwa kuwa kutofanya hivyo
kunaweza kusababisha kuuziwa maeneo yaliyopangwa kwa matumizi ya huduma
za jamii.
"Msijenge wala kunumua eneo bila kuulizia mamlaka
husika na ujenzi lazima uwe na kibali maana mamlaka ya upangaji ni ya
jiji la Dodoma" alisema Lukuvi.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony
Mtaka alimuahidi Waziri Lukuvi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote
yaliyopendekezwa kwenye ripoti na kumtaka mkuu wa wilaya ya Dodoma Jabir
Shekimweri kuhakikisha anasimamia na kutatua changamoto zote za ardhi
badala ya kuacha changamoto kupelekwa ofisi ya Mkuu wa mkoa.
Mmoja
wa wananchi wa mtaa Mbuyuni katika kata ya Kizota aliyejitambulisha kwa
jina la Mtumishi Yohana ameunga mkono uamuzi wa Waziri Lukuvi kwa
kueleza kuwa ana imani sasa haki itatendeka katika eneo hilo.
Naye Bi. Zainabu Almasi mbali na kushukuru uamuzi wa Waziri Lukuvi
alisema, bado kuna kero nyingine haijaenda sawa kutokana na kudai kuwa
na eneo lilichukuliwa bila kulipwa fidia.
"Ninashukuru kwa
uamuzi huu wa Waziri Lukuvi lakini kuna kero nyingine haijenda sawa,
nimeporwa eneo langu na kujengwa na tajiri usiku na mchana
nimenyanyasika" alisema Bi. Zainabu.
No comments:
Post a Comment