Na Teresia Mhagama
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameagiza kuwa, hatua kali zichukuliwe kwa Wataalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waliozembea na kupelekea baadhi ya mitambo ya umeme katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Msamvu kuungua moto.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo tarehe 14 Agosti, 2021 mkoani Morogoro wakati alipokagua athari zilizotokea baada ya kutokea hitilafu iliyopelekea kituo hicho kuwaka moto Agosti 2, 2021 ambapo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigella, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka.
" Hatua ambayo umeshaichukua Waziri wa Nishati ya kuwasimamisha wataalam waliofanya uzembe, naipongeza kwa sababu kama mfumo ulikuwa unaonyesha kuna hitilafu na wataalam walilazimisha kurudisha umeme, huku wakijua hatari iliyopo, haya ni makusudi ambayo yameleta matatizo kwenye mitambo hii ya umeme na hii ni hasara kubwa." Amesema Waziri Mkuu
Ameongeza kuwa "Waya unaoleta umeme kwenye kituo hiki imeelezwa kuwa haukufukiwa kwa kina kinachotakiwa na hivyo kupelekea a kukatwa na greda linalotumika katika mradi wa SGR, nakupongeza Waziri kwa kumsimamisha pia msimamizi wa TANESCO anayetakiwa kuhakikisha kuwa nyaya hizi zinafukiwa kwa kina kinachotakiwa, pia kama kuna mtaalam mwingine anahusika, endelea kuchukua hatua."
Ameagiza kuwa wataalam hao wakibainika kuwa wamefanya makosa, wachukuliwe hatua kali ili iwe funzo kwa wengine kwani matukio kama hayo yanaweza kujitokeza pia katika mikoa mingine.
Aidha amewakumbusha wataalam wa TANESCO katika vituo vya kupoza umeme kutunza mitambo hiyo na wahakikishe kuwa kila kitu kinasimamiwa kwa weledi na umakini mkubwa ili kuepusha uzembe utakaopelekea hasara ikiwemo ya kuunguza vifaa vya wananchi.
Pia ameeleza kuwa kwa sasa wananchi mkoani Morogoro wanalalamika kuhusu changamoto ya upatikanaji umeme wa uhakika ikiwemo viwanda vilivyopo mkoani humo, hivyo amemwagiza Waziri wa Nishati kufuatilia kazi ya upelekaji wa transfoma nyingine katika kituo hicho ili ianze kazi mara moja.
Awali, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alimweleza Waziri Mkuu kuwa, wataalam watano wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi na taarifa ya uchunguzi huo itawasilishwa tarehe 15 Agosti, 2021.
Aidha alieleza kuwa, ameshawaagiza
TANESCO kufunga mifumo itakayobaini hitilafu moja kwa moja mara inapotokea
badala ya kutegemea wataalam wanaosimamia miundombinu ya umeme kuanza kutembea
ili kutafuta chanzo cha hitilafu ya umeme pale inapotokea.
No comments:
Post a Comment