HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 27, 2021

Alama zinazoonekana ziwekwe katika eneo la mradi wa LNG-Dkt.Kalemani

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiangalia alama iliyowekwa katika eneo la mradi wa kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Likong’o wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi. Pamoja naye ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kushoto kwa Waziri), Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga (kulia kwa Waziri). Wengine katika picha ni Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio na watendaji wengine kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara.Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akiwa katika eneo la mradi wa kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Likong’o wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi. Pamoja naye ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga.


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza wakati wa mkutano wake na Wadau wa Maendeleo mkoani Lindi uliohusu mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG). Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato na kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga.

Na Teresia Mhagama, Lindi
WAZIRI wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuweka alama zinazoonekana kuzunguka eneo la mradi wa Kuchakata na kusindika Gesi Asilia (LNG) katika eneo la Likong’o wilayani Lindi, Mkoa wa Lindi.

Dkt.Kalemani alitoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo hilo akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, Kamishna wa Petroli na Gesi, Adam Zuberi, baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara na wawekezaji wa mradi huo, kampuni ya Equinor na Shell.

“ Eneo tumeligharamia hivyo ni muhimu likawekwa alama zinazoonekana badala ya kuweka bango pekee ili eneo hili liweze kutambulika na wananchi wasije kulivamia au kutumika vibaya, hivyo tuna wajibu wa kulinda eneo hili na kuonesha kuwa kuna kazi inakuja.” Alisema Dkt.Kalemani

Aidha, Dkt. Kalemani alitoa agizo kwa TPDC, ndani ya siku Tano wawe wamekamilisha taratibu za upatikanaji wa mkandarasi kutoka mkoani Lindi atakayeweka alama hizo za mipaka na mkandarasi huyo aanze kazi mara moja.

Aidha, alitoa agizo kwa TPDC kuhakikisha kuwa, eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,071 linasafishwa na kuwaasa wananchi kutovamia eneo hilo kwani limeshatwaliwa na Serikali baada ya wananchi hao kulipwa fidia.

Kabla ya kutembelea eneo hilo, viongozi hao walikutana na wadau wa maendeleo Mkoa wa Lindi pamoja na baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Lindi ambao ni Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete na Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah ili kueleza hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.

Dkt. Kalemani aliwaeleza wadau hao kuwa, Serikali imetoa takriban shilingi bilioni 5.72 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa eneo hilo kazi ambayo ilikamilika mwaka jana.

Alisema kuwa, mwezi Mei mwaka huu majadiliano yameanza na wawekezaji kuhusu utekelezaji wa mradi huo na yanatarajiwa kufikia mwisho mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, alisema kuwa Serikali itaendelea kuwahamasisha wananchi mkoani Lindi kuwa mstari wa mbele katika shughuli za kujiletea maendeleo kutokana na uwepo wa nishati kama vile umeme na Gesi.

Alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha za kutosha ili kufikisha huduma ya umeme na nishati nyingine kwa wananchi na Wizara ya Nishati ipo tayari kwa ajili ya kuwahudumia wananchi hao.
Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Nishati na Wadau wa Maendeleo Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani na kushoto kwake ni Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad