Hayo yamesemwa na Meneja wa Kanda, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Anitha Mshighati wakati wa mafunzo kwa Wafamasia, wataalam wa maabara na wamadaktari wa binadamu na mifugo mkoani Songwe.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watalaam wa kada ya afya waweze kufuatilia ubora wa dawa kwenye masoko pamoja na huduma ya udhibiti ubora ili kuzuia madhara yasiendelee kutokea kwa wananchi.
Amesema washiriki wa mafunzo hayo watapatiwa vyeti kwa ajili ya kufanya shughuli zao za ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika maeneo yao huku wakipewa nguvu ya kuchukua hatua za kisheria pindi wanapobaini ukiukwaji na uingizwaji wa dawa aidha zilizokwisha muda wake au feki.
"Mnalo jukumu la kuhakikisha ukaguzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi unafanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya, maduka na maabara sambamba na kuchukua hatua za kishetia kwa wanaokiuka sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 219," alisema Mshighati.
Mratibu wa Ofisi za Kanda TMDA, Dk. Henry Irunde amesema kwa sababu Mkoa wa Songwe unapakana na nchi Jirani za Zambia na Malawi ni muhimu wataalam hao wakaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo yote ya mipaka na njia za panya ili kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini na kusafirishwa nje zinakuwa salama na kukidhi vigezo vinavyotakiwa.
Amesema wataalam hao waendelee kutoa elimu kwa wafanyabiashara wanahusika na uuzaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na wananchi ili kujiepusha na madhara.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk. Nyembea Hamad amezishauri Halmashauri zote za Mkoa huo kutenga bajeti itakayowawezesha wataalam wa Afya waliopatiwa mafunzo na vyeti kufuatilia na kukagua maeneo yote yanayotoa huduma za dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uuzaji na uingizwaji wa dawa zisizohitaji kwa matumizi ya binadamu.
Amewashauri wataalam wa afya kuzingatia miiko na maadili ya kazi zao huku wakijiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa kufanya ukaguzi hususani maeneo ya mipakani kama vile Tunduma.
Amesema Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na TMDA watahakikisha mafunzo waliyopewa wataalam wa afya yanaleta mabadiliko na kumaliza kabisa uuzaji,uingizwaji na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
No comments:
Post a Comment